Samia, Mwinyi, kuzindua tovuti nyaraka za Dk Salim

Waziri Mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi wanatarajiwa kuwa wageni rasmi katika uzinduzi wa tovuti ya hifadhi ya nyaraka za Waziri Mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim.
Dar es Salam. Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi wanatarajiwa kuwa wageni rasmi katika uzinduzi wa tovuti ya hifadhi ya nyaraka za Waziri Mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim utakaofanyika jijini Dar es Salaam.
Dk Salim mwanadiplomasia mashuhuri, amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Nane wa Jumuiya ya Muungano wa Nchi za Afrika (OAU) kuanzia mwaka 1989 – 200.
Taarifa iliyotolewa jana Jumanne Septemba 2, 2023 na familia yake imesema uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika Septemba 30 jijini hapa.
Imewataja wageni wengine watakaoshiriki katika uzinduzi huo wametajwa kuwa ni pamoja na viongozi waandamizi kutoka kwenye sekta za umma na binafsi, viongozi wastaafu, na wawakilishi wa washirika wa maendeleo, asasi za kiraia, na taasisi za elimu ya juu.
“Tovuti hiyo inajumuisha video, picha na nyaraka mbalimbali kama vile hotuba, nakala za mawasiliano ya kimaandishi na machapisho ya kitafiti za Dk Salim.
“Inatoa ujuzi wa kipekee juu ya safari yake ya utumishi wa umma, na mchango wake katika mahusiano ya kimataifa na jitihada za ukombozi barani Afrika.
“Aidha, a inaangazia mchango wa nchi za Afrika katika siasa za kimataifa katika kipindi cha miaka ya 1960 hadi 2000,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tovuti hiyo imeandaliwa na familia ya Dk Salim kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na ndugu, jamaa na marafiki.
Aidha, tovuti hii ambayo ni hifadhi ya matukio yaliyotengeneza maisha ya Dk Salim na muhimu zaidi hifadhi ya nukuu na nyaraka zake mwenyewe, inalenga kuimarisha historia ya Tanzania na ile ya Afrika.
“Nyaraka za tovuti hii zitawavutia wale wanaotaka kuelewa mchango wa Tanzania na wa nchi nyingine barani Afrika katika historia ya dunia na siasa za kimataifa,” imesema taarifa hiyo.