Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Mwinyi ataja mafanikio ya ziara yake Indonesia

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Muktasari:

  • Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema akiwa Indonesia alihamasisha wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta za utalii, mafuta na gesi, bandari, uvuvi, mwani, karafuu, usafirishaji baharini na ufuatiliaji wa mafuta

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amerejea nchini Tanzania akitokea Indonesia huku akitaja maeneo wanayotaka kupata wawekezaji pamoja na biashara zinazoweza kufanywa kati ya mataifa hayo mawili.

Maeneo waliyoyalenga kwa uwekezaji Zanzibar ni utalii, mafuta na gesi, bandari, uvuvi, mwani, karafuu na usafirishaji baharini. 

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume, usiku wa kuamkia Septemba 9, 2024 Dk Mwinyi amesema wamejifunza mambo mengi kutoka Indonesia katika sekta ya uchumi wa buluu kwa kuwa Taifa hilo limepiga hatua kubwa zaidi.

“Kikubwa tulichojifunza ni uzoefu waliokuwa nao katika masuala ya uchumi wa buluu wametumia maji waliyonayo kwa manufaa ya kiuchumi,”amesema Dk Mwinyi aliyeondoka nchini Agosti 31, 2024 kuelekea Indonesia kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano na nchi za Afrika kuhusu biashara na uwekezaji kisha kupitia Msumbiji kuhudhuria sherehe za uhuru wa nchi hiyo. 

Katika sekta ya utalii amesema Indonesia ina watalii milioni nne kwa mwaka, hivyo wameomba kupatiwa uzoefu katika eneo hilo na kuwapatia fursa za masomo vijana ili wakajifunze nchini humo.

 “Hapa kwetu tuna hoteli zaidi ya 600, lakini ukitazama uongozi wa hizo hoteli wote wanatoka nje, sasa wakati umefika tupate mameneja kwenye hoteli zetu kutoka hapahapa Zanzibar kwa hiyo tumeomba watusaidie kupata uzoefu,”amesema.

Sekta nyingine ni ya mwani, amesema Indonesia wapo mbali hawauzi mwani kama wanavyouza Zanzibar bali wao wameenda mbali na kuchakata, hivyo utaratibu huo unawapatia kuuza kwa bei kubwa tofauti na kuuza mali ghafi.

“Napo tumewaomba waje watutazame kuona namna gani wanaweza wakatusaidia kukuza sekta yetu hii,” amesema Dk Mwinyi.

Kingine amesema wamepata fursa ya kutembelea kiwanda cha kuchakata bidhaa za karafuu cha Indesso  na kuona namna ya kupata mafuta ya majani ya karafuu. 

“Nimepata fursa ya kuzungumza na mwenye kiwanda hicho cha Indesso, wametuonyesha jinsi gani wanafanya kazi wanapata mafuta wanauza Ulaya kwa bei nzuri sana wakasema wapo tayari na wametuonyesha mfano wa vinu ambavyo wanataka vije Zanzibar zaidi ya 200,”amesema Dk Mwinyi. 

Hata hivyo, amesema wamewapa sharti kwamba ni vizuri wakijenga vinu hivyo viwe ni vya wananchi wazawa.

Kutokana na hilo, Dk Mwinyi amesema Serikali imekuja na mpango wa kuanzisha vikundi vya wanawake wajasiriamali na itawawezesha ujenzi huo kwa kuwa soko lipo tayari katika kampuni hiyo.

“Kwa hiyo haya ndio tunapaswa kufanya ili kuachana na kuuza bidhaa ghafi tuongeze thamani ndio tutapata bei nzuri kwa wakulima,” amesema Dk Mwinyi. 

Amesema katika uchumi, Indonesia ipo mbali kwa kuwa ina visiwa takribani 17,000 kwa hiyo wanayojifunza wenyewe na wanauzoefu wa kutosha.

 Licha ya kusema kuna mafanikio makubwa kati ya nchi hizo mbili katika biashara, ameeleza kuwa, bado kuna fursa kubwa inayopaswa kutumiwa. 

 “Kiwango cha fedha ambacho tunafanya biashara ni Dola za Kimarekani 33 milioni zaidi ya Sh89.9 bilioni  kutoka Dola 13 milioni zaidi ya Sh35.4 bilioni za kipindi cha nyuma, haya ni mafanikio lakini bado kuna haja ya kuongeza, kwa hiyo sisi tulipata fursa ya kuwaeleza fursa zilizopo za kibiashara,”amesema Dk Mwinyi. 

Akizungumzia kuhusu mafuta na gesi amesema wamepiga hatua kubwa katika sekta hiyo, “tumewakaribisha waje waone uwezekano wa kushirikiana na sisi katika utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi. 

Dk Mwinyi amesema wamefanya hivyo kwa sababu Serikali imeshaanza kutangaza vitalu kwa ajili ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta, hivyo vinahitaji uwekezaji.

 Eneo lingine ambalo kiongozi huyo wa nchi na ujumbe wake wamekaribisha wawekezaji kutoka Indonesia ni Bandari ya Mangapwani akisema Serikali ina nia ya kupata wawekezaji wengi katika bandari hiyo kwa kuwa ni jumuishi.

 Bandari hiyo itakuwa na bandari ya makontena, bandari ya mafuta na gesi, nafaka, chelezo, uvuvi kwa hiyo wanahitaji uwekezaji mkubwa ndiyo maana wamewaalika waje waone.

 Katika safari yake hiyo, Dk Mwinyi pia alishuhudia utiaji saini mkataba baina ya mamlaka za dawa na vipodozi za Indonesia na Tanzania, akisema kwa sasa kuna dawa ambazo zitakuwa zinanunuliwa na Tanzania lakini kwa ajili ya matumizi ya eneo zima la Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

 Amesema baada ya mazungumzo hayo na kuonyesha maeneo wanayotamani kupata uwekezaji, sasa kinachosubiriwa wanategemea kupata timu katika sekta hizo kutoka Indonesia kufika kisiwani hapa kuona maeneo hayo ili kuanza safari ya kushirikiana.


Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.