Polisi wataka kila mtu abebe jukumu la ulinzi

Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar ( CP), Hamad Khamis Hamad akisisitiza jambo wakati alipokua akizungumza na wajumbe wa mafunzo hayo. Picha na Muhammed Khamis
Muktasari:
- Polisi Zanzibar limewataka wananchi kujiunga katika vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuzuia uharifu na kuilinda amani.
Unguja. Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamad Khamis Hamad amesema kuwa jukumu la ulinzi na kulinda amani ni la wananchi wote hivyo kila Mtanzania awe chanzo cha kuzuia na kudhibiti uhalifu.
Kauli hiyo ameitoa leo, Novemba 29, 2023 wakati akifunga kongamano la ulinzi shirikishi katika ukumbi wa Shule ya Dk Ali Muhammed Shein.
Amesema jukumu la usalama wa wananchi si la Jeshi la Polisi pekee hivyo uwepo wa vikundi vya ulinzi shirikishi vinavyoanzishwa na wananchi husaidia kupunguza ongezeko la vitendo vya kihalifu katika jamii.
Amesema kongamano hilo litaisaidia jamii kujua lengo la kuanzishwa kwa vikundi vya polisi jamii pamoja na kufanya kampeni ili watu wengi zaidi wajiung navyo na kusaidia vita dhidi ya vitendo viovu.
Pia Hamad amewataka wananchi kushirikiana na jeshi hilo katika kutoa ushahidi wa kesi mbalimbali zinazojitokeza katika jamii.
“Sisi Jeshi la Polisi tuna haki na wajibu wa kuwalinda raia na mali zao ila na nyinyi mna haki ya kujilinda kwa kudumisha amani iliyopo katika jamii zetu. Tunahitaji kukimbiza wahalifu na tuweke usalama katika nchi yetu,” amesema
Naye Mratibu wa Polisi kutoka makao Makuu ya Polisi Dodoma, Dk Ezakiel Kyogo amewataka wazazi na walezi kuwapa watoto mafundisho waliyokuwa wakipewa zamani ili kuzuia mmomonyoko wa maadili katika jamii ya Zanzibar kwa masilahi ya Taifa la kesho.
Kongamano hilo la siku moja liliwashirikisha wazazi walezi, masheha wa shehia zaidi ya 50, wanafunzi wa skuli mbalimbali, vikundi vya ulinzi shirikishi na maafisa wa Jeshi la Polisi wakijadili umuhimu wa uwepo wa Ulinzi shirikishi katika Jamii.
Miongoni mwa washiriki hao wamesema watayachukua vyema na kutafanyia kazi maendekezo hayo kwa lengo la kuimarisha amani zaidi.