Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mikakati yaandaliwa kumaliza malaria Zanzibar

Ofisa Mdhamini Wizara ya Afya Khamis Bilali Ali akizungumza na watendaji wa Wizara hiyo katika maadhimisho ya siku ya malaria duniani Pemba.

Muktasari:

  • Zanzibar imejipanga kuhakikisha ifikapo mwaka 2029 inatokomeza kabisa ugonjwa wa malaria.

Pemba. Wizara ya Afya Zanzibar imesema inaendelea kuandaa mikakati kuhakikisha ifikapo mwaka 2029 inatokomeza kabisa ugonjwa wa malaria.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni ugawaji wa vyandarua ambavyo 340,895 viligawiwa mwaka 2024 sawa na asilimia 99.86.

Ofisa Mdhamini Wizara ya Afya (Pemba), Khamis Bilali Ali amesema hayo leo Aprili 26, 2025 katika madhimisho ya Siku ya Malaria Dunia yaliyofanyika Samail Gombani, Chake Chake mkoani Kusini Pemba.

Ametaja mikakati mingine ni kunyunyuzia dawa majumbani na kutoa matibabu sahihi katika vituo vya afya.

Amesema malaria ilikuwa tatizo kubwa kabla ya mwaka 2005, takwimu zikionyesha zaidi ya asilimia 40 ya wagonjwa waliolazwa hospitali walikuwa wanasumbuliwa na malaria. “Kwa sasa taarifa zinaonyesha ugonjwa wa malaria hapa Zanzibar uko chini ya asilimia moja kuanzia mwaka 2011,” amesema.

Kati ya Aprili 2024 hadi Machi 2025 amesema watu 828,818 walihudhuria hospitali kwa huduma tofauti za afya.

“Watu 135,894 sawa na asilimia 16.3, walichunguzwa vimelea vya malaria, kati ya hao wagonjwa 270 sawa na asilimia 32 walikutwa na maambukizi ndani ya Zanzibar, wagonjwa 131 sawa asilimia 48 wamepata maambukizi kutoka Unguja na wagonjwa 139 sawa na asilimia 52 wamepata maambukizi Pemba,” amesema.

Amesema kulingana taarifa hizo ugonjwa wa malaria umepungua ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hivyo wananchi wanapaswa kuchukua hatua na tahadhari kujikinga na malaria, ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya vyandarua.

Amewataka kuachana na uvumi kuwa Zanzibar hakuna malaria, badala yake waendelee kuchukua tahadhari.

Mkuu wa Idara ya Kinga na Elimu ya Afya Pemba, Msanifu Othman Massoud amesema kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha anachukua tahadhari za kutosha juu ya kujikinga na ugonjwa huo.

Amesema njia mojawapo kwa wananchi ni matumizi sahihi ya vyandarua vinavyotolewa na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.

“Tumekuwa tukichukua juhudi mbalimbali katika mapambano hayo, ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi sahihi ya vyandarua na upigaji dawa,” amesema.

Awali, mratibu wa kitengo cha kumaliza malaria Pemba, Makame Moh’d Kombo amesema wanahakikisha wanafanya jitihada ili ifikapo mwaka 2029, asilimia moja iwe imetokomezwa kabisa.

Tafiha Hassan Musa, mkazi wa Pemba amesema licha ya jitihada hizo, bado wananchi hawachukui tahadhari, wengine wakishindwa kutumia vyandarua kama inavyotakiwa.