Manispaa yawandoa wafanyabiashara eneo la Mtopepo

Eneo la Mtopepo, Mkoa wa Mjini Magharibi ambalo wafanyabiashara wanaendelea kufanya biashara na hawatakiwi kufanya biashara zao katika eneo hilo. Picha na Zuleikha Fatawi
Muktasari:
- Hatua hiyo imechukuliwa baada ya wafanyabiashara hao kukaidi agizo la awali la manispaa la kuondoka eneo la Mtopepo
Unguja. Baraza la Manispaa ya Magharibi A limewaondoa wafanyabiashara wadogo wadogo kando ya barabara eneo la Mtopepo, Mkoa wa Mjini Magharibi na kuwataka kuhamia katika Soko la Makufuli.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya wafanyabiashara hao kukaidi agizo la awali la manispaa, licha ya juhudi zilizofanyika kuwaelimisha na kuwashauri kuhusu umuhimu wa kufanya biashara maeneo rasmi yaliyotengwa kwa shughuli hiyo.
Akizungumza leo Jumapili Aprili 27, 2025, Mkuu wa Idara ya Huduma za Jamii na Mazingira wa Manispaa ya Magharibi A, Tatu Hussein Abdalla, amesema licha ya vikao vingi kufanyika kati ya manispaa na wafanyabiashara hao, bado wameendelea kukaidi maagizo hayo.
"Tumeshafanya vikao vya pamoja, kutoa barua na kubandika matangazo ya mara kwa mara kuwahimiza waondoke, lakini bado wengi wamepuuza maagizo hayo," amesema Tatu.
Ameongeza kuwa, wafanyabiashara wameendelea kufanya shughuli zao kama kawaida, jambo lililosababisha baraza kuchukua hatua kali zaidi.
Tatu ameonya kuwa, ni marufuku kwa mfanyabiashara yeyote kuendesha shughuli katika eneo hilo na atakayekaidi atachukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kutozwa faini au kuondolewa kwa nguvu.
Pia, amesisitiza kuwa biashara holela zinaathiri mazingira ya mji, jambo ambalo halikubaliki katika juhudi za kuendeleza miji safi na yenye mvuto.
“Baraza la Manispaa ya Magharibi A limesema linaendelea kusimamia dhamira ya kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama kwa ustawi wa wananchi,” amesema.
Amewataka wafanyabiashara kuheshimu sheria na taratibu zilizowekwa.
Baadhi ya wafanyabiashara wamekiri kuhudhuria vikao hivyo na kutakiwa kuondoka, lakini wameomba kuendelea kubaki katika eneo hilo kwa muda.
Mmoja wa wafanyabiashara hao aliyezungumza na Mwananchi, Ahmed Ibrahimu amesema eneo la Mtopepo linafaa zaidi kwa biashara kutokana na wingi wa wateja.
"Kwa kweli hapa ni pazuri kwa biashara. Ukilinganisha na huko wanapotutaka kwenda, hakuna wateja wa kutosha. Hapa hata mtu ambaye hakuwa na mpango wa kununua anaweza kubadili nia kwa kuona bidhaa barabarani," amesema Ahmed.
Naye Mohammed Issa amesema, si kwamba wanakaidi kuondoka, bali mazingira ndiyo yanawalazimisha kubakia hapo.
“Ila naona Manispaa imeshindwa kutusaidia kiutu, ngoja tuone itakuwaje, lakini tutaathirika sana,” amesema.