Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kauli ya RC Kitwana yazua mjadala

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana akionesha kitambulisho cha mpiga kura kilichowasilishwa kwake kwa ajili ya kukikagua

Muktasari:

  • Ni ile aliyoitoa Aprili 28, 2025 kuhusu kufanya ukakguzi kwa watumishi wa umma Mkoa wa Mjini Magharibi kama wanakadi ya mpigakura.

Unguja. Siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana kuwataka watendaji wa Serikali waliopo chini yake kuwasilisha kadi zao za mpigakura azikague, wadau wa uchaguzi wamesema hatua hiyo ni kuingilia majukumu ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Pia, wamesema inalenga kutoa vitisho na kuwapa hofu watumishi wa umma na kuwaelekeza nini cha kufanya wakati wa uchaguzi.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Joseph Kazi amesema  kitambulisho cha mpigakura ni mali ya raia na hapaswi kumpatia mtu yeyote isipokuwa kwa mamlaka husika.

Aprili 28, 2025 Kitwana alisema amefikia hatua hiyo akilenga kubaini wafanyakazi wa Serikali ambao hawakujiandikisha kwenye Daftari la Mpigakura.

“Kila mfanyakazi ndani ya mkoa huu ahakikishe anawasilisha kitambulisho chake cha mpigakura, tunaweka rekodi kweli, huyu anakwenda kupiga kura, kama kweli upo ambaye hauna kitambulisho basi ujitathimini mwenyewe,” alisema.

“Tukishafanya hivi, nitatoa ripoti yangu kwa mheshimiwa Rais (Dk Hussein Mwinyi)…kwa hiyo viongozi wao wenyewe kwa busara yao wataona cha kufanya.”

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu hatua watakazochukua baada ya kubaini wasiokuwa na vitambulisho hivyo, Kitwana alisema wanachotaka ni kufahamu mwenye nacho.

Kauli ya ZEC

Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Joseph Kazi, amesema mtu akishapewa kadi hiyo ni yake mwenyewe na ni mali ya tume, ndio maana mtu akipoteza na mtu mwingine akaiokota, anapaswa kuirejesha ofisi za tume.

“Mtu anatakiwa akae na kadi yake asimpatie mtu mwingine yeyote na kubwa ambalo naweza kusema, masuala ya kujiandikisha na kupiga kura hizi ni haki za wananchi kikatiba ana uamuzi wake, akiamua kwenda kujiandikisha na ni uamuzi wake kupiga kura, kumchagua mtu anayemtaka na sio suala la lazima,” amesema.

“Na ndio maana watu wanahamasishwa kujitokeza kujiandikisha lakini hawalazimishwi kujiandikisha, kwa hiyo haki hiyo mtu anaweza kuamua kuitumia au kutoitumia, tunawahamasisha wajiandikishe lakini hatuwalazimishi,” amesema Jaji Kazi.

Amesema anayetaka kumuita mtumishi akague kadi yake akilenga kutaka kujua kama kajiandikisha au la, si utaratibu.

 “Labda ni utaratibu wake huyo mkuu wa mkoa, lakini sijui sasa kama huyo mtu asipompelekea atachukuliwa hatua gani maana hilo sio suala la lazima.”

Wadau wa uchaguzi

Katibu wa Itikadi na Mawasiliano kwa Umma wa Chama cha ACT - Wazalendo, Salim Bimani amesema alichokifanya mkuu huyo wa mkoa ni makosa na wanapinga mchakato huo.

Amesema mkuu huyo wa mkoa hana mamlaka hayo kikatiba huku akisisitiza kuwa,hivyo ni viashiria ambavyo si vya kawaida nyuma ya jambo hilo.

Ameiomba ZEC iingilie kati na kuzuia jambo hilo lisifanyike.

“Tutachukua hatua za ziada kuiandikia ZEC kupinga jambo hili na tutaitisha mkutano wa waandishi wa habari kupinga jambo hili hadharani,” amesema Bimani.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Khamis Mbeto alisema huo sio msimamo wa chama bali ni wa mkuu wa mkoa mwenyewe.

Amesema CCM haitarajii wala kuagiza jambo kama hilo lifanyike kwa sababu wanaheshimu misingi ya demokrasia.

Mbeto amesema chama chao kinatambua si kosa la jinai kwa mtu kutojiandikisha kwenye Daftari la Mpigakura.

Amesema jukumu la vyama vyote vya siasa ni  kuwahamasisha wanachama wao na wananchi wajitokeze kujiandikisha na kupiga kura na si kuwalazimisha.

Kiongozi huyo amesema kupiga kura au kutopiga kura sio kosa la jinai ni hiyari ya mtu kufanya hivyo.

“Mimi ndiye msemaji, CCM haihusiani na kauli hiyo ya RC, kaitoa mwenyewe, tunaijua vema Katiba na suala la kujiandikisha na kupiga kura ni la mtu binafsi, chama kinaheshimu uamuzi wa mtu katu hatuwezi kumshinikiza,” amesema Mbeto.

Mwenyekiti Chama cha AAFP Taifa, Said Soud Said amesema mtu aliyejiandikisha ana hiyari ya kupiga kura sio kwa shinikizo.

“Unapowachukua watu kwa maana kwamba uwakague, maana yake tayari unawatishia ajira zao, ajira ni haki yao, lakini anachotaka kukitumia huyu mkuu wa mkoa ni  kama ngao ya kutaka kuwapeleka watumishi wa umma anapotaka yeye, hii sio haki,” amesema Said.

Amesema ZEC haipaswi kulifumbia macho jambo hilo katika mazingira ya kuendeleza demokrasia nchini na katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

“Sisi kama wanasiasa hatupendi kuona kitu kama hicho, inatakiwa tume ikemee mambo yanayojitokeza yanayoharibu nia na dhamira ya uchaguzi. Tunapinga kauli hii ya kuwalazimisha watumishi waoneshe watapigakura kwa chama gani, sio haki,” amesema.

Mwenyekiti huyo alisema kufanya hivyo ni kukiuka msingi wa Katiba na demokrasia nchini.

Said alisema ZEC  ikemee utaratibu wa namna hiyo unaoelekea kuwanyima haki watumishi kuwachagua viongozi wawatakao.

Amesema tume itakuwa huru na haki kuchunga kura za wananchi bila kujali itikadi za kisiasa.

“Inawezekana siku zote ulikuwa mpenzi wa chama fulani, lakini siku ya kupiga kura ukakipigia chama kingine na hii ndio haki ya mpigakura hapaswi kufuatiliwa kwenye maamuzi yake. Tume zikemee kuona viongozi wanataka kuwalazimisha watu waelekee upande wanaoutaka wao,”alisema Said.

Hata hivyo, mwanasiasa mkongwe na mchambuzi wa masuala ya siasa Zanzibar, Ali Makame amesema haoni shida akisisitiza kukaguliwa sio kupiga kura.

Amesema inaonekana kuna watendaji wengine wenye nyadhifa kubwa licha ya Serikali kuhamasisha, lakini hawapigi kura sasa katika mazingira kama hayo ameona bora afuatilie kuwabaini.

“Alichokizungumza RC ni jambo sahihi na hilo litawafanya watendaji wa Serikali wawe mfano, hivyo ni jambo zuri binafsi nakubaliana naye,” amesema Makame.

Pia, amesema kitendo cha kukusanya kadi za mpigakura hakijavunja haki.

 “Huwezi ukasema leo unaonesha mapenzi katika utendaji lakini huonyeshi mapenzi kwenda kuchagua viongozi watakao kuongoza, kwa hiyo kunakuwa na mapenzi ya kinafiki, pengine kura moja ndio inaweza kumsababishia ashindwe,” amesema.

Amesema kitendo alichokifanya Kitwana amejiongeza na huo ni ubunifu wake kama wanavyoambiwa wawe wabunifu kufanya mambo mbalimbali.