Prime
Dk Mwinyi ajibu hoja, tuhuma dhidi ya Serikali

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi
Muktasari:
- Dk Mwinyi ambaye pia ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) amesema ataendelea kuwa mvumilivu licha ya kutukanwa hadharani.
Unguja. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametumia ziara ya chama hicho kujibu hoja zinazotolewa kuhusu miradi ya Serikali na yeye binafsi.
Dk Mwinyi ambaye pia ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) amesema ataendelea kuwa mvumilivu licha ya kutukanwa hadharani.
Licha ya Dk Mwinyi kutotaja chama, lakini kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara, viongozi wakuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, akiwamo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Ismail Jussa wamekuwa wakiibua hoja kuhusu Serikali inayoongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk Mwinyi wakidai kumekuwa na kutofuatwa sheria za ununuzi na kufanya ufisadi katika baadhi ya miradi, ukiwamo wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Uwanja wa Mpira wa Amani Complex na uingizaji wa mafuta.
Mengine ni ubinafsishaji wa Bandari ya Malindi, ujenzi wa barabara na mikopo isiyokuwa na tija, hivyo wakidai kuna hatari ya kuingiza nchi katika madeni makubwa.
Katika mikutano, Jussa mara kadhaa amesema wanataka Serikali itoke hadharani kujibu hoja hizo na kazi kubwa ya chama cha siasa ni kuonyesha matobo na kasoro dhidi ya chama tawala.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara ya CCM aliyofanya kwenye mikoa yote mitano akizungumza na kamati za siasa za matawi, kata na majimbo kwa takribani wiki mbili iliyomalizika Agosti 22, 2024 kisiwani Pemba, Dk Mwinyi pamoja na kueleza mipango ya chama na Serikali ametumia fursa hiyo kujibu hoja, huku akiwataka wananchi na wanachama kuwa watulivu.
“Nasikiliza sana mikutano yao fitina ni nyingi, uongo ni mwingi wamefikia hatua ya kunitukana binafsi, nasema maneno yamekuwa mengi lakini sisi tuwe wavumilivu, mimi hawaniwezi kwa sababu nina chama kikubwa nina jumuiya imara, twendeni tukafanye kazi za uchaguzi na chama chetu kishinde kwa kishindo,” amesema Dk Mwinyi.
Katika ziara hiyo, pia amesisitiza mambo matatu ambayo ni hali ya kisiasa, utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 na maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Hali ya Kisiasa
Amesema kila ukikaribia uchaguzi mkuu baadhi ya vyama vya upinzani vinaanzisha harakati za kuchafua hali ya kisiasa kwa kutoa kauli za chuki, fitina, ubaguzi na upotoshaji juu ya masuala mbalimbali ya nchi.
Dk Mwinyi amesema dhamira yake ni kuona nchi inaendelea kuwa na amani na utulivu, huku wananchi wakiendelea kufanya kazi zao kwa utulivu.
Amefafanua kuwa siasa zinazofanywa na baadhi ya vyama vya upinzani ni za kizamani zilizojaa chuki na visasi na zisizo na nguvu za hoja.
Amesema baadhi ya wanaofanya siasa hizo hawana takwimu na uhalisia, na kusahau siasa za sasa zinaendana na ushindani wa sera za maendeleo.
“Siasa za sasa zinahitaji ushindani wa sera za maendeleo unaombatana na takwimu kuonyesha uhalisia na siyo za kizamani zilizojaa chuki, fitina, visasi na zisizo na nguvu ya hoja,” amesema.
Dk Mwinyi amesema mfano wa upotoshaji unaofanywa na wanaofanya siasa za kizamani bila kuwa na takwimu na ufafanuzi wa mambo ni kuhusu mikataba ya bandari na viwanja vya ndege.
Amesema maeneo hayo licha ya upotoshaji wao yamewekewa mazingira mazuri ya uendeshaji yaliyosaidia kupata mafanikio makubwa kuliko ilivyokuwa awali.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa kisisa na Serikali, wanaokosoa mikataba hiyo wakidai kuna ufisadi wakitaja changamoto bila kufafanua mafanikio yaliyofikiwa, wanapotosha umma kwa makusudi ili kuwachonganisha wananchi na Serikali yao.
Anaeleza mkataba wa uendeshaji wa viwanja vya ndege Zanzibar kuanzia alipoingia madarakani mwaka 2020 mapato aliyakuta yakiwa Sh12 bilioni lakini matumizi yalikuwa Sh14.5 bilioni kwa mwaka, hivyo walikuwa wanapata hasara ya Sh2.5 bilioni.
“Baada ya kuanza kusimamiwa mwaka 2023/24 Mamlaka ya Viwanja vya Ndege(ZAA), wanakusanya Sh40 bilioni, sambamba na kuimarika kwa huduma mbalimbali zilizoongeza ufanisi na kuwa kiwanja cha ndege bora nchini kinachopokea ndege nyingi kuliko viwanja vingine,” amesema.
Amesema kutokana na ufanisi huo ZAA imepata tuzo nne ikiwemo ya kiwanja cha ndege bora barani Afrika kinachopokea na kuhudumia vizuri abiria zaidi ya milioni mbili.
“Najiuliza sana hao wanasiasa wanaodai eti unafanyika ufisadi wanakuwa na dhamira gani, naombeni endeleeni kuwapuuza hawana hoja na badala yake wameanza kutengeneza uzushi,” amesema.
Akitoa ufafanuzi wa uendeshaji wa Bandari ya Malindi, amesema mwaka 2020/21 walikuwa wanakusanya Sh36 bilioni matumizi yakiwa Sh14 bilioni lakini ndani ya takribani mwaka mmoja baada ya bandari hiyo kuendeshwa na mwekezaji kampuni ya Ufaransa, mapato yameongeza zaidi na tayari wamekusanya Sh51 bilioni.
SMZ chini ya Shirika la Bandari imeingia makubaliano ya kuedesha bandari hiyo tangu Septemba mwaka jana na kampuni ya Ufaransa. Serikali inapata asilimia 30, kampuni hiyo ikipata asilimia 70, huku gharama za uendeshaji zote zikibebwa na kampuni hiyo.
“Baada ya kuingia mkataba wa kusimamia uendeshaji wa Bandari Zanzibar na siyo ubinafsishaji kama inavyopotoshwa, meli zilikuwa zinakaa siku 40 zikisubiri huduma, lakini kwa sasa zinakaa siku saba hadi 11 tu. Sasa hao wanaodai ufisadi wana lao jambo, uongo utabaki uongo na ukweli utasimama sehemu yake,” amesema.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, kutokana na mafanikio hayo, uchumi wa nchi unaimarika zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzo kabla ya mkataba huo.
Kauli za kibaguzi
Amesema moja ya chama cha upinzani Zanzibar viongozi wake wamekuwa wakitoa kauli za ubaguzi za kuangalia nani Mzanzibari zaidi kuliko mwingine.
Amesema Zanzibar ni nchi ya kisiwa kila mtu ana nasaba yake na wengi wao asili yao ni kutoka Tanzania Bara, huku wakiwapo pia wa kutoka Comoro, Oman, China na India.
“Tukemee kwa nguvu zote tabia hii ya ubaguzi kwani mfano mzuri ni mimi wakati ninapoteua viongozi na watendaji wa kunisaidia serikalini huwa sibagui wala kuangalia mtu anatoka wapi, ninachoangalia ni vigezo vya kitaaluma na utendaji wa mtu,” amesema.
“Wenzetu wakiwa katika majukwaa ya kisiasa wanatamba na kujivunia eti wao ni Wazanzibari halisi wakidai wengine ni wa kuja siyo Wazanzibari je, haki hiyo ya kujiona wao ni bora kuliko wengine wameipata wapi,” amehoji.
Amesema katika utawala wake akiwa Rais wa Zanzibar, ataendelea kuwa mvumilivu licha ya kutukanwa hadharani na baadhi ya wanasiasa na kwamba, ataendelea kulinda amani kwa masilahi mapana ya wananchi wote.
Mikopo utekelezaji miradi
Dk Mwinyi amesema baadhi ya wanasiasa wanakosoa suala la Serikali kukopa fedha nje ya nchi, akisema uongozi wake umekuja na ubunifu wa kutekeleza miradi mikubwa kwa haraka ili wananchi wapate huduma.
Amezungumzia ujenzi wa hospitali ya kisasa ya Binguni, Mkoa wa Kusini Unguja akisema baada ya kuingia madarakani alienda kuikagua akaambiwa zinahitajika Sh50 bilioni kuijenga, hivyo Serikali imekopa na kuijenga lakini itakuwa inarejesha Sh5 bilioni kila mwaka mpaka mkopo huo ukamilike.
Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, iwapo Serikali ingetaka kujenga kwa fedha zake yenyewe ingeichukua zaidi ya miaka 10 kuikamilisha.
Amesema ubunifu huo umewaumiza wapinzani kwani kulikuwa na shule nyingi, hospitali na miradi mingine haijajengwa kwa hiyo wanapata shida wanapoona imejengwa kwa kipindi kifupi.
Amesema wananchi walipokuwa wanahitaji huduma ya afya walilazimika kwenda Hospitali ya Mnazi Mmoja, lakini kwa sasa kila wilaya na baadhi ya mikoa nchini zina hospitali zenye huduma zote na vifaatiba vya kisasa.
“Wao hawataki tujenge ili wapate maneno na hoja za kusema, sasa nawaambia hivi, sisi tutaendelea kuijenga Zanzibar iwe ya kisasa na yenye hadhi ya nchi za visiwa zinazoendelea kiuchumi duniani,” amesema.
Ulipaji mikopo
Dk Mwinyi anafafanua namna Serikali ilivyojipanga kulipa mikopo, akisema inaweka Dola 10 milioni za Marekani kila mwezi katika akaunti ya kulipa madeni, hivyo kwa mwaka zitakusanywa Dola 120 milioni (Sh300 bilioni)kwa mwaka.
Amesema, “kwa sasa tayari kuna Dola milioni 150 katika akaunti hiyo na kuna Dola milioni 100 katika benki mbili za NBC na CRDB, zote ni Dola za Marekani ambazo ni zaidi ya Sh600 bilioni.”
“Tulivyojipanga hata tukikopa trilioni moja, mbili na zaidi hatuna shida ya kulipa, hivyo wanaosema tunakopa sana hawajui wanachosema, kwani ukweli ni huu ninaosema lengo letu ni kuijenga nchi kwa manufaa ya wananchi wote. Wakitaka ushahidi wataonyeshwa na vitabu vya risiti zote za benki zinapowekwa fedha hizo vipo,” amesema.
Ununuzi wa mafuta
Kuhusu vyama vya upinzani kuhoji suala la ununuzi wa mafuta, Dk Mwinyi amesema Serikali iliamua mafuta yanunuliwe kwa pamoja ili wenye vituo vidogo wanunue sehemu moja, lengo likiwa ipate mapato ya uhakika na yakusanywe sehemu moja.