Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ambulensi iliyobeba maiti yawaka moto



Muktasari:

  • Ndani ya ambulensi iliyobeba maiti kulikuwa na watu wengine wanane waliokuwa wakienda makaburini kuzika.

Unguja. Watu wanane waliokuwa wanakwenda makaburini kuzika pamoja na mwili wa marehemu wamenusurika kuteketea baada ya ambulensi walimokuwamo kuwaka moto.

Tukio hilo limetokea leo Aprili 24, 2025 saa 5:00 asubuhi eneo la Saateni, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa Operesheni wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar, Kamishna Msaidizi Haji Pandu Hamad amesema hakuna aliyejeruhiwa zaidi ya gari hilo pekee.

Amesema walipofika eneo la tukio walikuta moto umeshadhibitiwa na wananchi.

“Gari hili (ambulensi) lilikuwa halijatembea umbali mrefu likiwa na maiti wanakwenda kuzika. Dereva alisikia kitu kinapasuka, kisha likaanza kuwaka moto. Hakuna aliyepata tatizo,” amesema.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema walisikia kelele wakakimbia kusaidia kuuzima moto.

Salama Mohamed Salum,  mwalimu wa shule ya awali (maandalizi) ya Saateni iliyopo jirani na eneo lilipopata hitilafu gari hilo amesema:

“Baada ya kuona kuna moto tulitoa mpira wa maji ili kulimwagia gari, lakini tukaona haitoshi tukachukua ndoo za maji kwenda kulimwagia kwa kushirikiana na wananchi wengine,” amesema.

Mwalimu mwingine wa shule hiyo, Said Abdallah Shaaban amesema: “Tulitoa msaada wa kulimwagia maji gari ili lisiendelee kuteketea baada ya kuona hakuna msaada mwingine.”

Dereva wa gari hilo, Sheikh Jamal Murtaza amesema maiti ilichukuliwa Mbweni kwenda kuzikwa.

Amesema walipofika eneo hilo ghafla walisikia mlio ulioashiria hatari.

“Wakati tunatazama vitu vyetu na mfumo wa maji tukakuta upo sawa lakini liliendelea kupiga alamu ikiashiria kuna tukio lingine linakuja, ghafla tukaona moto kwa chini. Tukazima gari na kushusha maiti. Tunashukuru wakazi wa eneo hili wametusaidia kuuzima,” amesema.

Amesema mtungi wa kuzima moto ni mdogo, wasingepata usaidizi wasingefanikiwa kuuzima.

“Tunashukuru sana Shule ya Saateni wametusaidia maji kuzima moto na tumefanikiwa,” amesema.