Z’bar kutumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuimarisha mifumo

Rais wa Zanzibar akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma ya dharura ya mama na mtoto Mchanga itakayotumiwa na wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii wakati wa mahafali ya kwanza ya wahudumu hao yaliyofanyika katika Chuo Kikuu Cha Taifa Zanzibar(Suza)
Muktasari:
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Juni 30, 2025 wakati wa mahafali ya kwanza ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza) Mkoa wa Kusini Unguja
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameitaka Wizara ya Afya kuwa na mipango endelevu kuwapata wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHWs) akisema kutachochea mabadiliko chanya ya utoaji wa huduma.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Juni 30, 2025 wakati wa mahafali ya kwanza ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza) Mkoa wa Kusini Unguja.
“Utoaji wa huduma kupitia wahudumu hawa wa afya ngazi ya jamii utachangia sana katika kuchochea mabadiliko chanya ya kiafya na kusababisha maendeleo endelevu nchini, kwa hiyo wizara isibweteke iendeleze mkakati huu kuhakikisha tunakuwa na wahudumu wa afya kama mipango yetu inavyotutaka,” amesema.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, wahudumu hao ngazi ya jamii wanahitajika 3,000 na waliohitimu kwa awamu ya kwanza ni 1,242.
Dk Mwinyi amesema wizara inapaswa kuongeza kasi ili jitihada hizo zisiishie njiani ili kufikia lengo la kuwa na wahudumu ngazi ya jamii 3,000 kwa kuwa, tayari mfumo huo umeanza kuonesha matunda.
Katika hatua nyingine , Rais Mwinyi amezindua huduma za rufaa ya dharura kwa wajawazito na watoto wachanga (M-mama) kutoka kwenye jamii kwenda kwenye vituo vya afya huduma hiyo, pia itatekelezwa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
“Kufuatia uzinduzi huu wanajamii na wahudumu wa afya ngazi ya jamii watapaswa kuitambua na kuitumia vyema huduma ya namba 115 kwa ajili ya huduma hizi za rufaa ya dharura kwa makundi yaliyotajwa, hii ni hatua kubwa katika utekelezaji wa mpango wa wizara katika azma ya kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga nchini,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema ni faraja kubwa kuona wamesimamia mfumo wa teknolojia katika kutoa huduma za afya kwa wananchi kwa kuwa, inaonesha mafanikio mengi kuhusiana na ukusanyaji pamoja na upokeaji wa taarifa.
Amesema hilo litafanya wapate takwimu sahihi na kwa wakati muafaka kwa ajili ya utekelezaji wa mipango na afua mbalimbali za kiafya nchini.
Waziri wa Afya, Ahmed Nassor Mazrui amesema kuhitimu kwa vijana hao kumeipa nguvu na ujasiri Wizara ya Afya na kuona kwamba sasa ni wakati sahihi kupeleka huduma za usafiri wa dharura kwenye ngazi ya jamii kupitia namba 115.
“CHW watakuwa waratibu wa huduma hiyo muhimu. Naomba kuchukua fursa hii kusisitiza kwamba, huduma ya 115 ni kwa mama wajawazito na watoto wachanga wenye dharura,” amesema Mazrui.
Amesema wamehitimu wahudumu wa afya ngazi ya jamii 1,242, kati ya hao 898 ni miongoni mwa waliokuwa wahudumu wa afya wa kujitolea (CHVs).
Mazrui amesema wahitimu hao wataanza kazi baada ya mahafali na watalipwa Sh150,000 mara tatu ya posho walioyokuwa wakilipwa awali ya Sh50,000.
“Serikali kwa sasa inawatambua rasmi wahudumu hawa kama ni watendaji wa afya katika ngazi ya jamii. Tunaweza kujivunia kwa sasa kuwa tuna majeshi mahiri, wakomavu na wazalendo katika kupigania afya za wananchi kwenye kila shehia, kitongoji hata kwenye ngazi ya familia,”amesema.
Awali, katibu mkuu wizara hiyo, Dk Mngereza Mzee Miraji amesema wizara imedhamiria kuwa na mifumo madhubuti ya kukusanyia taarifa za afya katika jamii kupitia wahudumu wa afya ngazi ya jamii na wizara kutumia taarifa hizo kuimarishia mipango ya afya ya msingi na kupunguza msongamano katika vituo vya afya.
“Kupitia CHWs pamoja na huduma zinazotolewa kupitia kambi mbalimbali za matibabu na huduma za uchunguzi zinazotolewa na tiba tembezi ambazo kwa sasa zimeimarika kwa kiasi kikubwa kupitia washirika wa maendeleo,” amesema.
Kauli mbiu ya mahafali hiyo inasema “Wezesha Jamii, Kuimarisha Ubora wa Huduma za Afya ya Msingi.”