Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Malalamiko ya umeme, huduma za afya yashughulikiwe’

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Muhamed Said Dimwa akizungumza na wajumbe wa Kamati za siasa, za matawi, wadi, majimbo na Wilaya ya Micheweni Kaskazini Pemba.

Muktasari:

  • Imedaiwa kuwa, baadhi ya watendaji na viongozi wamekuwa wakichelewesha huduma kwa makusudi ili kuonesha kuwa, Serikali haitekelezi ahadi zake kwa wakati

Unguja. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, amezitaka wizara nne kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu urasimu wa kuunganishiwa umeme na huduma duni za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Micheweni.

Wizara zilizotakiwa kuchukua hatua ni wizara ya Afya, Maji, Nishati na Madini Zanzibar.

Dk Dimwa ameagiza kuwa ndani ya wiki moja, wizara hizo ziwe zimewasilisha ripoti ya utekelezaji wa maagizo hayo, ili kuhakikisha wananchi wa Pemba wanapata huduma bora kama ilivyokusudiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Leo Jumatatu, Aprili 28, 2025, katika mwendelezo wa ziara ya Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya NEC ya CCM Taifa, Zanzibar ya kuimarisha uhai wa chama, Dk Dimwa amekutana na wajumbe wa kamati za siasa ngazi za matawi, wadi, majimbo na Wilaya ya Micheweni.

“Baadhi ya watendaji na viongozi wa Serikali wamekuwa wakichelewesha huduma kwa makusudi ili kuonesha kuwa, Serikali haitekelezi ahadi zake kwa wakati,” amesema Dk Dimwa.

Amesema Pemba kuna malalamiko mengi ya kukatika kwa umeme mara kwa mara, urasimu wa kuunganishiwa umeme, pamoja na huduma hafifu za afya licha ya kuwepo kwa vifaa vya kisasa, madaktari wa kutosha na dawa katika hospitali.

Dk Dimwa amesisitiza kuwa CCM ipo kwa ajili ya kuhakikisha Serikali inatoa huduma bora kwa wananchi bila ubaguzi na kwamba, chama hakitavumilia kusikia wananchi wanabaguliwa au kupokea huduma chini ya kiwango.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib amesema baadhi ya wananchi wanapendelea kwenda Hospitali ya Wilaya badala ya vituo vya afya vilivyopo karibu nao, hali inayosababisha msongamano mkubwa na malalamiko.

Kuhusu ucheleweshaji wa kuunganishiwa umeme, amesema Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) linaendelea na juhudi za kuboresha huduma na kutatua changamoto hizo kwa wakati.

“Tumezipokea na tutayafanyia kazi kwa wakati maelekezo yaliyotolewa na sekretarieti. Pia, tunawashauri wananchi kutumia vituo vya afya vilivyopo,” amesema Salama.

Katika ziara hiyo, Dk Dimwa amewataka viongozi wa chama kuhamasisha wanachama wenye nia ya kugombea katika uchaguzi wa ndani kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu ili kutimiza haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa.

Aidha, amekemea vikali vitendo vya rushwa na migogoro inayoweza kuibuka wakati wa uchaguzi huo, akisisitiza kuwa wanachama wanapaswa kuungana badala ya kugawanyika.

Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar, Khamis Mbeto amewataka wananchi wa Pemba kupuuza madai kutoka kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wanaosema Serikali haijafanya maendeleo yoyote.

“Badala yake, wananchi wanapaswa kupima maendeleo yaliyopo sasa ukilinganisha na hali ya zamani,” amesema Mbeto.

Amesema Serikali imeendelea kuleta maendeleo makubwa Pemba ikiwamo ujenzi wa barabara, shule za kisasa za ghorofa, uwanja wa ndege wa kimataifa, uwekezaji katika sekta ya utalii, boti za uvuvi na huduma bora za afya.

Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Khadija Salum Ali, amewahimiza wanachama wenye sifa za kugombea nafasi za uongozi kwa kuwa ni haki ya kikatiba ya kuchaguliwa na kuchagua.

Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Organisation CCM Zanzibar, Ibrahim Omar Kilupi amewaonya baadhi ya wanachama na viongozi wanaotoa vitisho kwa wenzao wanaotaka kugombea, akisisitiza kuwa hakuna mtu aliye na hati miliki ya uongozi wa kudumu ndani ya chama hicho.

Kilupi amesema CCM tayari imetangaza ratiba ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu kupitia wilaya na mikoa na amewahimiza wanachama kuchagua viongozi wachapakazi, waadilifu na wazalendo watakaotetea masilahi ya wananchi wengi badala ya wao binafsi.