Wananchi watahadharishwa kujiepusha na rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025

Dar es Salaam. Wakati joto la maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025 likizidi kupanda, wananchi wametakiwa kuchukua nafasi ya kipekee katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa, wakihimizwa kuepuka ushawishi wa fedha na zawadi zinazolenga kununua dhamira zao za kisiasa.
Wito huo umetolewa leo Julai 4, 2025 jijini Dar es Salaam katika mjadala wa wadau kuhusu rushwa kwenye uchaguzi, ulioandaliwa na Asasi ya Kiraia ya JamiiAfrica (zamani JamiiForums), kwa kushirikisha viongozi wa taasisi za umma, wanaharakati na wananchi.
Akizungumza nje ya mjadala huo, Mkuu wa Programu wa JamiiAfrica Ziada Seukindo amesema lengo kuu ni kumuwezesha mwananchi kufahamu wajibu wake wa kuwa mstari wa mbele kupinga rushwa badala ya kusubiri hatua za mamlaka pekee.
"Mwananchi lazima akae katikati katika mapambano ya rushwa. Ajue nafasi yake ni ipi na siyo kila kitu kumwachia Serikali au sheria peke yake," amesema Seukindo.
Ameongeza kuwa mara nyingi rushwa huonekana kama faida ya muda mfupi pasipo kuzingatia madhara yake ya muda mrefu kwa jamii nzima.
"Rushwa inatazama sasa na siyo baadaye. Tunaangalia namna ya kuwashirikisha wananchi kuona athari za kupokea fedha au zawadi ili wachague viongozi wasiofaa, hasa kipindi hiki cha uchaguzi," amesema.
Kwa upande wake, Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Nyanda Shuli, amesema mikutano na mijadala ya aina hii ni sehemu muhimu ya mkakati wa kuhakikisha wananchi wanapata uelewa sahihi kabla ya kupiga kura.
"Tunataka wananchi wajitambue na wajitenge mbali na viongozi wanaojaribu kujipatia uhalali kwa njia zisizofaa. Kuna sheria kali za kupambana na rushwa, lakini pia tunahitaji maarifa na uhamasishaji," amesema Kamishna Shuli.
Amesisitiza kuwa iwapo wananchi wataendekeza rushwa, wanaweza kukosa wawakilishi bora watakaowatetea kwa dhati.
"Watu wanapaswa waelewe kuwa shilingi elfu ishirini unayopewa sasa haiwezi kukusaidia kwa miaka mitano ijayo. Uchaguzi ni haki ya msingi, unapaswa kutumika kwa umakini," ameongeza.
Ameeleza pia kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inayo wajibu wa kisheria kushiriki mijadala na kampeni za kuongeza uelewa kwa umma kuhusu uadilifu na utawala bora.
Mkazi wa Dar es Salaam, Agatha Gerald amesema rushwa wakati wa uchaguzi huonekana kama jambo dogo lakini madhara yake hujitokeza baadaye.
"Unaweza ukapokea Sh20,000, kisha huyo kiongozi akapotea miaka yote mitano, mkabaki mnateseka bila huduma muhimu," amesema Agatha.
Ushindani wa siasa na mvuto wa maslahi
Mchambuzi wa masuala ya siasa na Mwalimu Deus Kibamba, akizungumza katika mjadala huo, amesema ushindani mkubwa unaoshuhudiwa kwenye siasa unatokana pia na mvuto wa masilahi makubwa yanayopatikana kwenye nafasi za uongozi.
"Nafasi za kisiasa zina unono wa hali ya juu. Hali hii imewafanya watu wa kada mbalimbali kama wasanii, wanahabari, madaktari na watumishi wa umma kukimbilia siasa," amesema Kibamba.
Hata hivyo, amesema Mahakama kuondoa baadhi ya wagombea waliopita bila kupingwa kumeleta ushindani wenye maana na umakini zaidi wa uchaguzi.
Kuhusu ulipaji wa posho na mishahara ya wanasiasa, Kibamba amesema haufai kupangwa na wanasiasa wenyewe bali na tume huru za utumishi wa umma.
"Masuala ya maslahi lazima yadhibitiwe ili siasa ibaki kuwa wito wa kuhudumia wananchi, siyo njia rahisi ya kujipatia kipato," amesisitiza.