Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UPDP yaahidi mapinduzi sekta ya elimu, ajira kwa vijana

Muktasari:

  • Msingi wa pendekezo la UPDP ni kurekebisha mfumo wa elimu.

Dar es Salaam. Suala la elimu haliwezi kutenganishwa na mjadala wa ajira, kupunguza umaskini na mustakabali wa vijana wa Taifa hili.

Tanzania ikiwa na zaidi ya asilimia 60 ya watu walio chini ya umri wa miaka 25, imekuwa na ongezeko la uhitaji wa mfumo wa elimu unaofundisha si tu masomo ya darasani bali pia kuandaa vijana kwa stadi za maisha na kazi.

Hata hivyo, changamoto ni nyingi,  upungufu wa walimu wenye sifa, idadi kubwa ya wanafunzi ukilinganisha na walimu, miundombinu duni na kutokuwepo kwa uwiano kati ya elimu darasani na mahitaji ya soko la ajira.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, zaidi ya vijana 800,000 wa Kitanzania huingia katika soko la ajira kila mwaka, lakini ni wachache hupata ajira rasmi. Wengine huishia kwenye sekta isiyo rasmi au kubaki wasio na kazi.

Katika muktadha huo, Chama cha United People's Democratic Party (UPDP|) kimewasilisha dira mpya ya elimu kupitia ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2025–2030, inayotajwa kuwa ya kiubunifu na ya kimageuzi.


Muundo mpya wa elimu

Msingi wa pendekezo la UPDP ni kurekebisha mfumo wa elimu. Badala ya miaka saba ya shule ya msingi, chama kinapendekeza mpango wa miaka 10; huku miaka saba ya masomo darasani ikifuatiwa na mitatu ya mafunzo ya ufundi stadi.

“Mtoto ataingia shule kuanzia darasa la kwanza hadi darasa la 10. Miaka saba ya kwanza atasoma masomo ya kitaaluma, na miaka mitatu inayofuata atajikita kwenye elimu ya ufundi stadi,” inaeleza ilani.

Wenye uwezo wataendelea na elimu ya sekondari na vyuo vikuu, lakini kwa wanaomaliza baada ya miaka 10, Serikali itawawezesha kupitia vikundi vya ushirika vitakavyosaidiwa na Serikali.

“Vikundi hivi vitapatiwa mikopo ya kununua zana, kufanya kazi katika karakana na viwanda vidogo vya Serikali, na kuzalisha bidhaa kwa soko la ndani na nje ya nchi,” inaeleza zaidi ilani hiyo.


Mfumo wenye changamoto

Wataalamu wanasema mageuzi hayo yanalenga kuziba mapengo ya muda mrefu. Mfumo wa elimu wa Tanzania umekuwa na kiwango kikubwa cha wanafunzi kuacha shule, hasa baada ya elimu ya msingi.

Takwimu za Wizara ya Elimu zinaonesha kuwa licha ya ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi wa msingi katika miongo miwili iliyopita, chini ya asilimia 35 tu ya wanafunzi, huendelea sekondari kwa masomo ya kidato cha kwanza.

“Wengi, hususan vijijini, huacha shule kwa sababu familia zao haziwezi kumudu sare, vitabu au nauli,” anasema Dk Agatha Komba, mtafiti wa elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Hata wanaomaliza elimu ya msingi, mitalaa ni ya kitaaluma zaidi bila maandalizi ya ujuzi wa maisha au ajira.

"Pengo lililopo ni kubwa zaidi katika elimu ya juu, ambapo vyuo vikuu huzalisha wahitimu wengi wa sayansi ya jamii na biashara, huku viwanda vikilalamikia upungufu wa wahandisi, wataalamu wa kilimo na ufundi," anasema Dk Komba.


Kuunganisha shule na viwanda

Kinachofanya mpango wa UPDP kujitofautisha na vyama vingine ni dhamira yake ya kuunganisha shule, mafunzo ya ufundi na viwanda vidogo.

Wahitimu wa elimu ya msingi ya miaka 10 wataunda vikundi vya ushirika vitakavyopata mikopo, kuwa na akaunti za benki, kuuza bidhaa kupitia masoko rasmi na kujilipa mishahara.

Serikali itatoa msaada wa kiufundi na kuwahakikishia upatikanaji wa masoko ndani na nje ya nchi.

“Ikiwa mpango huu utafanikiwa, utabadili namna elimu inavyohusiana na uchumi — badala ya kuzalisha watafuta ajira, mfumo utazalisha wajasiriamali,” inaeleza ilani hiyo.

Mfumo wa kuunganisha elimu na ufundi si mpya; nchi kama Ujerumani na Uswisi zimefanikiwa kupitia mfumo wa mafunzo ya pamoja. Hata Rwanda imepiga hatua kupitia mkakati wa TVET kwa ushirikiano na sekta binafsi.

"Mpango wa UPDP unafanana na miundo mingine iliyofanyika kwa mafanikio kwingineko," anasema mchambuzi huru wa masuala ya elimu, Dk Johnson Mrema.

"Lakini changamoto kubwa itakuwa ni kuhakikisha kwamba viwanda vinakuwepo ili kuwaajiri hawa vijana. Vinginevyo, tunaweza kuwapatia mafunzo kwa ajili ya soko ambalo halipo.”


Changamoto ya kifedha

Swali kubwa la kujiuliza ni kama mpango huu unaweza kufanikishwa kifedha. Kujenga karakana, kutoa mikopo na kuhakikisha masoko yanapatikana, kunahitaji uwekezaji mkubwa wa umma.

Hivi sasa Tanzania inatumia takribani asilimia 4 ya Pato la Taifa kwenye elimu, chini ya kiwango kinachopendekezwa kimataifa cha asilimia 6.

Mchambuzi wa sera na uchumi, Samuel Mushi, anasema: “Maono hayo ni mazuri, hakuna anayehoji umuhimu wa mafunzo ya ufundi. Lakini Serikali lazima ieleze itafadhili vipi, sio tu ufundishaji, bali pia mitaji ya vikundi vya vijana na viwanda vya kuwaajiri. Bila mkakati wa wazi wa fedha, inaweza kubaki ahadi nzuri tu.”

UPDP inadai mapato yatapatikana kupitia ukusanyaji bora wa kodi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini.


Uhaba wa walimu

Utekelezaji wa mpango huu unahitaji walimu wengi wa masomo ya ufundi. Kwa sasa upungufu ni mkubwa, zaidi ya walimu 100,000 wanahitajika katika shule za msingi na sekondari.

“Mafunzo ya ufundi yanahitaji walimu maalumu, mfano useremala, ufundi magari, Tehama, ushonaji, uchomeleaji. Tunawatoa wapi walimu hawa?” anauliza mtaalamu wa elimu, Martha Lyimo.

Anaongeza kuwa, UPDP italazimika kuanzisha vyuo vipya vya ualimu vya masomo ya ufundi sambamba na kuboresha vilivyopo.

 “Nilikamilisha kidato cha nne miaka mitatu iliyopita na sasa naendesha bodaboda,” anasema Joseph Michael (23) kutoka Morogoro. “Kama ningepata mafunzo sahihi na zana, ningependelea kufungua karakana. Lakini mara nyingi tunaahidiwa wakati wa uchaguzi na hatuoni utekelezaji.”


Mustakabali wa Taifa

Mabadiliko ya elimu yamekuwa ajenda ya muda mrefu. CCM hivi karibuni iliboresha sekta hiyo kupitia mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, toleo la 2023.

Sasa, ilani ya UPDP inaleta mwelekeo mpya wenye lengo la kuoanisha elimu na ajira kwa namna inayoweza kubadili mfumo wa kijamii na kiuchumi wa Tanzania.

Lakini wataalamu wanatahadharisha: bila fedha za kutosha, mafunzo ya walimu na ushirikiano na sekta za viwanda, ndoto ya kugeuza wanafunzi kuwa wazalishaji inaweza kuyeyuka.

Hata hivyo, katika nchi yenye vijana wengi wasio na ajira, mjadala huu wa UPDP ni muhimu na umekuja wakati mwafaka.

Kama asemavyo Mushi:  “Chama kinauliza maswali sahihi. Swali ni kama kitaweza kutoa majibu. Hapo ndipo Watanzania wataamua siku ya uchaguzi.”