Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtaala mpya wa ufundi kuibua ajira kwa vijana, kuimarisha viwanda

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Emirates Aluminium and Glass Co. Ltd, Deogratius Marandu (wa tatu kulia), wakizindua mtaala mpya wa ufundi stadi wa aluminium na glass uliotayarishwa na kampuni hiyo kwa kushirikiana na VETA, jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Veta kwa kushirikiana na kampuni ya Emirates waandaa mtaala wa aluminium na glass kuziba pengo la ujuzi; Serikali yasema utaongeza ajira, ubunifu na tija viwandani.

Dar es Salaam. Serikali imezindua mtaala mpya wa mafunzo ya ufungaji wa alumini na vioo pamoja na utengenezaji wa miundo ya metali (Aluminium and Glass fitting with metal fabrication), hatua inayolenga kuziba pengo la ujuzi kati ya wahitimu na mahitaji halisi ya soko la ajira.

Mtaala huo umeandaliwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) kwa kushirikiana na kampuni ya Emirates Aluminium and Glass Co. Ltd, ukiwa sehemu ya juhudi za kuimarisha sekta ya ufundi na kuongeza mchango wake katika uchumi wa viwanda.

Akizungumza wakati wa uzinduzi uliofanyika Aprili 23, 2026, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, ameielekeza Veta kuendelea kubuni mitaala inayokwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira.

Amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika elimu inayozingatia ujuzi ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa tayari kujiajiri, kuajiriwa na kuchangia maendeleo ya taifa.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir akizungumza wakati wa uzinduzi wa mtaala mpya wa ufundi stadi wa aluminium na glass uliotayarishwa na kampuni hiyo kwa kushirikiana na VETA, jijini Dar es Salaam.

“Utekelezaji wa mtaala huu utaongeza ajira kwa vijana, kuimarisha tija katika uzalishaji na kuweka msingi imara wa ubunifu na ushindani wa uchumi,” amesema Ameir.

Ameongeza kuwa mtaala huo umezingatia mahitaji halisi ya soko, hivyo unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa pengo kati ya elimu inayotolewa na ujuzi unaohitajika kazini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Anthony Kasore, amesema mtaala huo utazalisha wahitimu wenye ubunifu na ujuzi watakaoweza kushiriki kikamilifu katika uchumi wa viwanda.

“Tunaamini kupitia mtaala huu tutapata wataalamu watakaozalisha bidhaa bora, jambo litakaloongeza imani ya watumiaji na kupanua soko la bidhaa za ndani,” amesema Kasore.

Baadhi ya wadau mbalimbali wa elimu ambao wamejitokeza katika uzinduzi wa mtaala mpya wa ufundi stadi wa aluminium na glass uliotayarishwa na kampuni hiyo kwa kushirikiana na VETA, jijini Dar es Salaam.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Emirates Aluminium and Glass Co. Ltd, Deogratius Marandu, amesema uzinduzi wa mtaala huo unaonyesha dhamira ya pamoja ya kuinua ujuzi wa vijana na kuifanya sekta ya ufundi kuwa rasmi na yenye mchango mkubwa katika pato la taifa.

Amesema ushirikiano huo utawezesha vijana kuanza kunufaika mapema kwa kujiunga na mafunzo ya ufundi mara baada ya kumaliza elimu ya msingi au sekondari, hivyo kuongeza fursa za kujiajiri kupitia kazi za aluminium na glass.

“Tunapokuwa na wataalamu wenye ujuzi, viwanda vitazalisha bidhaa bora zaidi, mahitaji ya soko yataongezeka na mafundi watapata ajira nyingi,” amesema Marandu.

Amesisitiza pia umuhimu wa kuwepo kwa mazingira rafiki ya uwekezaji, yakiwemo amani na utulivu, ili kuhakikisha juhudi hizo zinaleta matokeo chanya kwa taifa.