Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lala salama CCM, uteuzi kuanza leo

Muktasari:

  • Vikao vya uteuzi vya wagombea udiwnai, ubunge na uwakilishi vinaendelea ili kuwapata wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) watakaoshiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025

Dar es Salaam. Mchakato wa kupatikana wagombea wa udiwani, ubunge na uwakilishi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), umefikia dakika za lala salama, baada ya vikao vya mwisho vya uteuzi kuanza leo.

Hatima ya nani atakayekuwa mgombea wa udiwani katika kata husika itajulikana Agosti 13, huku wale watakaogombea ubunge na uwakilishi kwenye majimbo itawekwa hadharani Agosti 22, 2025 baada ya kukamilika kwa vikao hivyo vilivyoanza leo.

Ni nyakati za lala salama kwa upande mmoja, lakini kupanda na kushuka kwa presha za watiania kwa upande mwingine, hasa ukizingatia vikao hivyo vina mamlaka ya kuteua jina lolote kati ya watiania waliopigiwa kura za maoni, kuwa mgombea.

Kuongoza kwa wingi wa kura, sio hakikisho la kuteuliwa kuwa mgombea wa jimbo au kata kwa mujibu wa miongozo ya chama hicho, ndio sababu presha zaidi inaendelea kuwafukuta miongoni mwa watiania na wapambe wao.

Hata hivyo, baadhi ya wajumbe wamesema ni matamanio yao kuona mapendekezo yao yakizingatiwa, kwa maana walioongoza kwa kura ndio wapewe nafasi zaidi kwa kuwa ndio machaguo yao.

Katika kura za maoni zilizofanyika Agosti 4, 2025 ilishuhudia zaidi ya waliokuwa wabunge 50 wa Bunge la 12 lililovunjwa Agosti 3 mwaka huu wakiangukia pua. Miongoni mwao ni manaibu mawaziri wanane, walioshindwa kwenye kura za maoni wanasubiri kudra za vikao.

Manaibu mawaziri hao ni Geoffey Pinda (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Exaud Kigahe (Viwanda na Biashara), Danstan Kitandula (Maliasili na Utalii), Jumanne Sagini (Katiba na Sheria), Stanslaus Nyongo (Mipango na Uwekezaji).

Wengine ni Alexander Mnyeti (Mifugo na Uvuvi), Khamis Hamza Chilo (Muungano na Mazingira na Cosato Chumi (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki).

Vikao hivyo ambavyo mwisho wake ni kuteua mgombea mmoja wa nafasi hizo vinaanza leo Jumatatu, Agosti 11, 2025.

Vikao vile vya awali, vyenyewe vilishachekecha majina ya wote waliochukua fomu na kurejeshwa majina matatu hadi tisa kwa baadhi ya maeneo.

Lakini vikao hivi ambavyo vimefikia hatua ya mikoa, kwanza vitajadili na kuteua wagombea udiwani na vitapendekeza majina kwa kamati kuu kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar kutoa mapendekezo kwa Kamati Maalumu.

Agosti 13, 2025, vitafanyika vikao vya Halmashauri Kuu za CCM za mikoa kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea udiwani mmoja kwa kila kata/wadi na udiwani wa viti maalumu.

Wabunge  watakaoteuliwa na Halmashauri Kuu Agosti 22, 2025 chini ya Uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan ndiyo watakaokuwa wagombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Katika vikao vya awali vya kuchuja majina ya waliotiania ili kupeleka majina kwa kura za maoni baada ya kuchukua na kurejesha fomu, zaidi ya waliokuwa wabunge 40 kwenye Bunge la 12 majina yao hayakurudi.

Miongoni mwao ni January Makamba (Bumbuli), Mrisho Gambo (Arusha Mjini), Stephen Byabato (Bukoba Mjini), Christopher Sendeka (Simanjiro), Pauline Gekul (Babati Mjini), Flatey Maasay (Mbulu Vijijini) na Luhaga Mpina wa Kisesa ambaye ametimkia ACT-Wazalendo na kupitishwa kuwania urais.

Tayari CCM imeshatangaza silaha za ushindi kwenye uchaguzi huo. Makamu Mwenyekiti Bara, Stephen Wasira mbele ya mamia waliojitokeza kumsindikiza Rais Samia na Dk Emmanuel Nchimbi juzi kuchukua fomu za urais, alisema silaha hizo ni Ilani za uchaguzi 2020/25 jinsi ilivyotekelezwa na ile ya 2025/30 inavyojieleza.


Mitazamo watiania 

Salum Ramadhan, mtia nia Jimbo la Chwaka visiwani Zanzibar amesema anaamini chama kitatenda haki na hakijawahi kukosea na mtu sahihi atapatikana, kupeperusha bendera ya CCM.

“Mategemeo yangu kwamba, chama kitatenda haki na katika hili hakiwezi kukosea kwa sababu ndio kinajua nani anafaa na anaweza kuwasaidia wananchi na chama kukiletea ushindi, kwa hiyo tusubiri tu uamuzi wa chama,” amesema.

Mwingine ni Said Hassan Haji aliyetiania katika Jimbo la Kijini visiwani humo, amesema matarajio yake ni mchakato wa chama hicho kumpata mtu sahihi ili kukisaidia sio tu kuleta ushindi lakini kuleta maendeleo katika maeneo husika.


Matarajio ya wajumbe

“Sasa tunaona kama makubaliano ya chama yanakiukwa na iwapo ikiendelea hivi huenda jambo hili likaleta shida, tunaomba viongozi waliangalie kwa umakini sana,” amesema Kibuyu Mjaka Haji mmoja wa wajumbe.

Mjumbe wa chama hicho kutoka Kinondoni, Abdallah Siraji amesema matarajio yake kwa vikao ni kuona aliyepigiwa kura nyingi za maoni ndiye anayeteuliwa kugombea.

“Wasipoturudishia huwa hatufurahii, hatua inayokuwa imechukuliwa, sasa hatujui lakini hizo mamlaka zinazopitisha zinaangalia mbali inawezekana mtu alipata kura nyingi kwa wajumbe zinaweza kuwa halali au zinatokana na mchezo aliocheza,” amesema.


Mchakato wa kura za maoni

Mchakato wa kura za maoni kwa watiania ndani chama hicho ulianza siku moja baada ya majina kurudi kutoka Kamati Kuu na ulichukua siku tatu kwa watiania kupita kujitambulisha na kunadi sera zao kwa ngazi ya matawi.

Ni hatua ambayo watiania wa ubunge na udiwani walikuwa wanaambatana pamoja kwa kutumia usafiri mmoja, kuzunguka maeneo mbalimbali kujitambulisha kwa wajumbe na siku ya nne zilipigwa kura za maoni kuna walioongoza kwa wingi wa kura na wengine kudondoka.

Baadhi ya maeneo, kulikuwa na changamoto ndogondogo kama ucheleweshwaji wa vifaa vya kupigia kura na malalamiko ya baadhi ya wagombea kuhusu orodha ya wapiga kura.

Hata hivyo, kamati za uchaguzi za chama hicho zilichukua hatua kuhakikisha haki na uwazi vinaimarishwa katika kila hatua ya mchakato huu.

Ingawa kuna  maeneo watiania walikuwa wanalalamikia watiania wenzao kushiriki vitendo vya rushwa ikiwamo Jimbo la Bumbuli kwa kile walichodai chama hicho kiliandaa usafiri mmoja, lakini kulikuwa na magari binafsi yanayodhaniwa kutumika kugawa fedha kwa wajumbe.

Vilevile, baadhi ya maeneo kulikuwa na vitendo vya utekaji mathalani Kata ya Sirari aliyekuwa anaongoza kwenye kura za maoni katika mchakato ametoweka na hadi sasa haijulikani aliko na vyombo vya usalama vinaendelea kuchunguza.


Kauli ya Samia

Akizungumza Agosti 9, 2025 wakati anatoka kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya urais wa Tanzania, Mwenyekiti wa chama chicho, Samia aliwataka wanachama kuwa wamoja baada ya mchakato wa uteuzi kukamilika.

“Kama ilivyo desturi yetu ya CCM, mchakato wa uteuzi unapoisha na makundi nayo yaishe na ushindani ndani ya chama nao uishe, tunarudi kuwa kitu kimoja ili tuingie kwenye uchaguzi tukiwa wamoja na mshikamano,” alisema.

Pia Samia alisema ni muhimu kudumisha desturi hiyo na vilevile wajitokeze katika maeneo yao kuwaunga mkono wagombea wao wanapoenda ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuchukua fomu za kuwa wagombea.

“Hawa ni wagombea wa chama chetu na sote tupo kwenye timu moja, hivyo twendeni kwa umoja na mshikamano kama timu ili tuhakikishe ushindi wa kishindo kwa chama,” alisema Samia.


Maoni ya wachambuzi

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk George Kahangwa amesema kwa sababu kamati hizo zinaundwa na binadamu, kuna uwezekano zikakosea kwa makusudi au zikapendelea.

Hata hivyo, amesema kinachotakiwa ni vikao hivyo kuwasikiliza watu na kama kutakuwa na tatizo vinawajibika kuyaweka wazi kwa wajumbe na wanachama.

“Wasipowaambia chochote na wakafanya uamuzi ambao ni kinyume na matarajio yao, hawawezi kuepuka lawama na malalamiko kutoka kwa wajumbe na kutoka kwa aliyepigiwa kura nyingi,” amesema.

Aliyepigiwa kura nyingi akiona amefyekwa, Dk Kahangwa amesema mara nyingi huwa wanachagua jukwaa lingine, lakini kuna watakaobakia ndani ya CCM na watakuwa chanzo cha uhasama na mifarakano.

“Namna mchakato ulivyoenda na malalamiko yaliyoanza kujitokeza uwezekano wa ndani ya CCM, kuwa na migogoro ni mkubwa hasa majina yatakapoanza kutoka,” amesema.

Dk Kahangwa amesema kauli ya Samia kuhusu uteuzi ukiisha watu wavunje makundi, inapaswa iendane na utendaji haki ili kuyaepusha hayo.

“Lakini mtu akijua hapa kadhulumiwa hapa wamepindisha unamtulizaje ni rahisi kumtuliza mwanadamu kama haki imetendeka, ni lazima viongozi wahakikishe haki inazingatiwa,” amesema.

Mhadhiri kutoka Chuo cha Sauti Mwanza, Dk Ntui Ponsian amesema hakutakuwa na mapya zaidi katika uteuzi wa wagombea, kwa kuwa machakato wa kura za maoni umelalamikiwa na wengi bila majibu.

“Huwezi kuvunja makundi kama malalamiko ya watu hayajaondolewa. Watu wanalalamika rushwa, ubabe umetumika, uvunjaji makundi unaambatana na kuwasikiliza watu kabla ya kwenda kutoa hilo jina moja,” amesema Dk Ntui.