Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ilani ya ACT-Wazalendo na mchakato wa Katiba mpya ndani ya miezi sita

Moshi. Chama cha ACT-Wazalendo, kimeahidi kuwa, endapo Watanzania watakipa ridhaa na kushika dola katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa Oktoba 2025, kitahakikisha kinafufua mchakato wa Katiba mpya ndani ya miezi sita.

Kupitia ilani yake ya uchaguzi mkuu, chama hicho kimeahidi pia kitahakikisha ndani ya kipindi hicho kinaanzisha Tume Huru ya Uchaguzi na kuhakikisha kila raia analindwa na kupata haki bila ubaguzi wowote.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe, alisema mipango hiyo ni mizuri inayowezekana kama Tanzania ingekuwa na mazingira sahihi ya kidemokrasia tofauti hivyo inabaki kuwa ndoto za alinacha.

Mkurugenzi wa Shirika la Uraia na Msaada wa Kisheria (Cilao), Odero Charles Odero alisema jambo la msingi si kuanzisha mchakato wa Katiba mpya, bali ni aina gani ya Katiba wananchi wanaitaka.

Kilio cha Katiba mpya kimekuwa ni cha muda mrefu kabla hata ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992, lakini ndoto ya kuipata Katiba mpya imekuwa haitimii licha ya ahadi na maneno matamu katika ilani za uchaguzi.

Tume mbalimbali zilizoundwa juu ya suala hilo zote zilikuja na mapendekezo ya wananchi ya haja ya kuwa na Katiba mpya kutokana na Katiba ya mwaka 1977 kuonekana haikidhi mazingira ya sasa ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Katiba hiyo ilitungwa mwaka 1977 wakati huo nchi ikiwa chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa, Chama cha Mapinduzi (CCM) na inalalamikiwa na wadau wa siasa kuw,  inakandamiza uhuru wa kidemokrasia na kuminya upinzani.

Mwaka 2011, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, alitangaza kuwaachia Watanzania kumbukumbu inayoishi kwa kuwapa Katiba mpya na kuanzisha mchakato wake kwa kuanzisha Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Tume hiyo iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba ilikusanya maoni ya wananchi na kuandika rasimu ya Katiba na kuiwasilisha katika Bunge Maalumu la Katiba, lakini utungwaji wake ulivurugika kutokana vyama kuingiza masilahi yao.

Serikali ya CCM nayo imeahidi kufufua mchakato wa kuandika Katiba mpya na tayari imetunga sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kuchukua nafasi ya Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi (NEC), huku wadau wakisema hakuna kipya.


ACT na Katiba na Tume Huru

Serikali ACT Wazalendo, ndani ya miezi sita, itafufua mchakato wa kuandika Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano kwa kuwashirikisha Watanzania kikamilifu na itahakikisha mchakato unakamilika ndani ya mwaka mmoja.

Katiba hiyo mpya itapunguza madaraka ya Rais na itaboresha muundo wa Muungano ili kuwa na Muungano wa usawa, haki na wenye kuheshimiana na kusimamia uundwaji wa muundo wa Serikali tatu.

Ndani ya muda huo, itatamka na kuanzisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambayo mchakato wa upatikanaji wa watumishi wake hautawajibika kwa Rais na pia itaainisha na kuimarisha misingi ya haki na usawa kisheria.

Pia, itaimarisha uhuru na uimara wa mihimili yote ya dola, itajali masilahi mapana ya Taifa letu na kuimarisha uwajibikaji kwa kurejeshea mamlaka ya uamuzi kwa wananchi na itasimamia uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Pia, italeta mfumo bora wa kuendesha Serikali hasa za mitaa kwa kuwezesha ugatuaji, itawafuta wakuu wa wilaya na kuweka utaratibu wa wananchi kuwa na haki na wajibu wa kuchagua wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa


Mapambano ya rushwa, kudai haki

Katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake (2025-2030), kama itapewa ridhaa ya dola, Serikali ya ACT- Wazalendo itapiga marufuku viongozi na watumishi wa Serikali kupewa zabuni katika miradi ya Serikali.

Pia, itaandaa na kuchapisha orodha ya kampuni na taasisi zinazotoa rushwa kupata miradi ili kuondoa mianya ya rushwa katika ununuzi hasa za nje, kwa kushirikiana na mataifa ya jirani na rafiki.

Mbali na ahadi hiyo,  ACT-Wazalendo itaifanya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwa chombo huru na cha kitaalamu kisichofungamana na siasa katika utendaji wake na itapiga marufuku mtu yeyote aliyepatikana na hatia za rushwa kufanya kazi na au biashara katika taasisi ya Serikali.

Pia, itawafukuza uanachama, kuwafuta uongozi na kuwachukulia hatua nyingine za kisheria viongozi wa kuchaguliwa, watakaojihusisha na vitendo vya rushwa na ubadhirifu na itawachukulia hatua kali za kisheria watumishi wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa na ubadhirifu.

Serikali ya ACT-Wazalendo itaimarisha na kulinda uhuru wa mihimili mitatu ya dola ili kuhakikisha inatimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi yetu na itahakikisha Serikali inatii na kutekeleza hukumu na maagizo ya Mahakama dhidi ya Serikali ndani ya siku 60.

ACT-Wazalendo imedhamiria kuhakikisha Tanzania inakuwa sehemu salama kwa wananchi kufanya shughuli zao, kuishi na kupiga hatua za maendeleo bila hofu, wasiwasi na shaka na itakomesha vitendo vya utekaji, utesaji na mauaji ya raia na kuvunja magenge yote ya uhalifu yanayohusika na vitendo hivyo.

Imeahidi kuhakikisha inafanya uchunguzi wa matukio yote ya utekaji, utesaji na mauaji ya raia na kutoa ripoti ya kina kwa umma na kuchukua hatua dhidi ya wote wanaohusika ndani ya siku 100 za utawala wake.


Kauli za wadau

Mkurugenzi wa Jukata, Bob Wangwe alisema mipango hiyo ni mizuri inayowezekana kama Tanzania ingekuwa na mazingira sahihi ya kidemokrasia yanayoruhusu ushindani sawa wa vyama vya siasa.

“Kinyume chake, ilani hizi za vyama vya upinzani zinabaki kuwa ndoto za alinacha,” alisema Bob Wangwe ambaye pia ni mwanaharakati wa haki za binadamu.

Mkurugenzi wa Cilao, Odero alisema jambo la msingi sio tu kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya bali jambo la msingi na la lazima ni kuwa na mtizamo wa aina gani ya Katiba ambayo watanzania wanaitaka.

“Na ili kujibu na kutibu tatizo hili ni lazima kuwa na muafaka wa Taifa maana Taifa ambalo limegawanyika linaweza kuwa na Katiba mpya kwa jina, lakini tabia ya Katiba hiyo ikawa udikteta wa mawazo ya chama kimoja,”alisema Odero.

“Muhimu tuwe na muafaka wa Taifa ili kuzuia yaliyotokea kwenye mchakato maarufu kama Tume ya Warioba na kwenye Bunge Maalumu la Katiba ambalo lilitawaliwa ubinafsi wa vyama vya siasa,”alisisitiza mkurugenzi huyo.

Mussa Juma ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Wanahabari ya Usaidizi Jamii za Pembezoni(Maipac), alisema ilani ya ACT-Wazalendo ni nzuri kwa kuwa, waliyoyaandika ni madai ya Watanzania wengi ila tatizo ni utekelezaji wake.

Petroa Ahmam, Mkurugenzi wa Shirika la Messo alisema chama kinachoingia kwenye uchaguzi ambao sheria za uchaguzi hazijafanyiwa marekebisho ni kuhadaa Watanzania na kushindwa kulinda na kusimamia misingi muhimu ya demokrasia.

Alizitaja sheria hizo kuwa ni zile zinazosimamia uteuzi na uapishwaji wa mawakala na wateuliwe na vyama na Tume ipewe nakala ya taarifa tu na matokeo yabandikwe kwenye sehemu wazi au ubao wa kituo cha kupiga kura.

“Mawakala wabaki na vifaa vyao vya mawasiliano ili wawe huru kuripoti muda wote nini kinaenda sawa na nini hakiendi sawa.  ACT-Wazalendo kuingia kwenye chaguzi za aina hiyo ni kuhadaa Watanzania na kushindwa kulinda na kusimamia misingi muhimu ya demokrasia,”alisisitiza Ahman.