DCEA wagawa vitanda 160 kwa Nyumba za upataji nafuu Arusha.
Afisa Ustawi na Elimu wa DCEA Kanda ya Kaskazini, Sarah Ndaba, Akizungumza katika makabidhiano hayo, leo may 7,2026
Muktasari:
- Amesema wamefikia uamuzi wa kutoa vitanda na magodoro hayo baada ya kufanya ziara katika nyumba hizo na kubaini changamoto kubwa ya vifaa vya malazi.
Arusha. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imegawa vitanda na magodoro 160 vyenye thamani ya zaidi ya Sh 43 milioni kwa nyumba 19 za upataji nafuu (Sober Houses) mkoani Arusha.
Msaada huo umetolewa kwa ufadhili wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) pamoja na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika kuimarisha ustawi wa jamii na kusaidia mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, leo may 7, 2026, Afisa Ustawi na Elimu wa DCEA Kanda ya Kaskazini, Sarah Ndaba, amesema msaada huo ni juhudi za mamlaka hiyo kuboresha huduma malazi kwa waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya.
Amesema wamefikia uamuzi wa kutoa vitanda na magodoro hayo baada ya kufanya ziara katika nyumba hizo na kubaini changamoto kubwa ya vifaa vya malazi.
Amesema uhaba huo ulikuwa ukiathiri mazingira ya matibabu na mchakato wa upataji nafuu kwa waraibu wanaoendelea na tiba za marekebisho.
“Msaada huu utaongeza utulivu na kuboresha mazingira ya wanaopata matibabu katika nyumba za upataji nafuu. Tutaendelea kufuatilia matumizi yake ili yadumu na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema Ndaba.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Gabriel Makalla, amesema nyumba za upataji nafuu zimekuwa msaada mkubwa kwa vijana na wananchi wanaopambana kuondokana na utegemezi wa dawa za kulevya kwa kuwapatia malezi, ushauri nasaha na mazingira salama ya kuendelea na matibabu.
Amesema kwa sasa Mkoa wa Arusha una nyumba 19 za upataji nafuu zinazohudumia waraibu 505, hivyo msaada huo utaongeza ubora wa huduma na kusaidia waathirika kurejea katika maisha yao ya kawaida.
“Huu ni uwekezaji wa utu na ubinadamu, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha waathirika wanapata huduma bora na matumaini mapya ya maisha, ili kurejea katika hali yao ya kawaida” amesema Mkude.
Amewataka wadau wa sekta binafsi, mashirika na watu binafsi kuunga mkono juhudi za DCEA kwa kusaidia kuboresha huduma zinazotolewa katika vituo vya upataji nafuu.
Naye mratibu wa viongozi wa nyumba hizo amesema msaada huo umekuja wakati muafaka na wanatarajia utasaidia kupunguza changamoto za malazi zilizokuwa zikikabili baadhi ya vituo.
Mmoja wa waraibu wanaoendelea na matibabu, Arafa Walii, amesema msaada huo umeleta faraja kubwa kwa waathirika wanaopambana kurejea katika maisha ya kawaida.
"uraibu unatibika endapo mhusika ataamua kupata matibabu na kuzingatia ushauri wa wataalamu, tunaomba jamii itusaidie tuweze kurudi katika maisha ya kawaida"
"Tunashukuru DCEA kwa kuendelea kutupa nafasi ya kujiamini na kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii, na Tutaendelea kuwa mabalozi wa vijana kuhakikisha hawajiingizi katika janga hili" amesema.