Chaumma kamili kuingia Ikulu, Salum Mwalimu apewa kiti
Muktasari:
- Jina la Salum Mwalimu lilipendekezwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho yenye jukumu la kuleta mapendekezo ya jina la mgombea urais Tanzania na Zanzibar katika kikao kilichofanyika jana.
Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Benson Kigaila amemtangaza Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu atakuwa mpeperusha bendera wa chama hicho kwenye mbio za urais wa Tanzania Oktoba 29, 2025.
Kigaila amemtangaza kiongozi huyo kwenye mkutano mkuu wa Chaumma unaoendelea Mlimani City leo Alhamisi Agosti 7, 2025.
Kigaila amesema jina la kiongozi huyo lilipendekezwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho yenye jukumu la kuleta mapendekezo ya jina la mgombea urais Tanzania na Zanzibar katika kikao kilichofanyika jana.
"Baada ya kufanya utafiti na kufikiri kwa kina ni mtu gani anaweza kutuvusha, Halmashauri Kuu ya Taifa ilikuja na jina la Salum Mwalimu, anatufaa kutuvusha kwenye mbio za urais wa Tanzania," amesema Kigaila.
Kulingana na maelezo ya Kigaila amesema mchakato wa kumpata Salum waliopitia hadi kufika kupata, kwanza walifanya utafiti na katika kutafiti huu:"Tuliangalia nani anaweza kutufaa na kutuvusha, tulifanya mazingatio tukimteua mtu anajua matatizo ya Watanzania akiona anaweza kuumizwa na kuyashughulikia."
"Pia tulitafuta mtu asiyekuwa na mawaa, wakukimbiliwa na makundi yote lakini awe anaelewa ilani ya chama bila mashaka yeyote, tumepanga kwenda kuipumzisha CCM, inayofanana na mchezaji aliyeko uwanjani hadi anafikisha dakika 90 hajafunga kwahiyo inafaa kwenda benchi na kusajili mchezaji mpya,” amesema Kigaila.
Baada ya jina hilo kuwasilishwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu na kusomwa kwa wasifu wake, waliulizwa kama wanakubaliana na wajumbe wote walikubali na kumpitisha kuwa mgombea urais.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Salum alikuwa mgombea mwenza wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati mgombea urais akiwa Tundu Lissu. Amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu-Bara wa Chadema.