Chatanda awataka wanawake kusimamia ushindi wa CCM Geita
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa,Mary Chatanda
Muktasari:
- Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda amewataka wanawake kufanya kampeni za kitanda kwa kitanda, nyumba kwa nyumba na kupatana na wenzi wao mapema kuhakikisha wanakipigia kura za kishindo CCM.
Geita. Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda, amewataka wanawake wa Mkoa wa Geita kushirikiana na familia zao kuhakikisha kura za ushindi wa Rais Samia Suluhu Hassan na wagombea ubunge wa CCM zinapatikana kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 29,2025.
Akizungumza leo Septemba 17, 2025 katika mkutano wa kampeni mjini Geita, Chatanda amesema wanawake wana nafasi kubwa ya kuamua hatima ya uchaguzi.
“Wanawake fanyeni kampeni kitanda kwa kitanda, nyumba kwa nyumba. Pataneni na waume zenu na watoto wenu, mshirikiane kuhakikisha kura zinapigwa kwa ajili ya Samia na wagombea wetu,” amesema Chatanda.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicholais Kasendamila amesema wananchi wanapaswa kutumia kura zao kuthamini kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia.
“Tumepewa barabara za lami kilomita 17, mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria unaendelea na ukikamilika utazalisha lita milioni 22 ambazo ni zaidi ya mahitaji ya sasa. Haya yote ni matokeo ya kazi kubwa ya Rais,” amesema Kasendamila.
Mbunge aliyemaliza muda wake, Constantine Kanyasu amewataka wananchi kumpa kura za ndio mgombea wa sasa, Chacha Wambura, ili akamilishe miradi viporo iliyobakia na kuanzisha mingine kwa maendeleo ya wananchi .
“Nilipoingia mwaka 2015 Geita haikuwa na maji, wananchi walitegemea maji ya kununua kwenye matoroli. Leo miradi mingi imeanza, shule zimeongezeka kutoka saba hadi 25 mpya. Ni wajibu wa wananchi kumwamini Chacha akamilishe haya,” amesema Kanyasu.
Mgombea ubunge wa Geita Mjini, Chacha Wambura amesema vipaumbele vyake vitakuwa elimu, afya, barabara, miradi ya kiuchumi na ujenzi wa chuo kikuu kipya.
“Tutahakikisha Geita inakuwa na shule bora, hospitali na vituo vya afya vipya, barabara za lami na taa za mitaani. Pia, chuo kikuu kitakapojengwa kitakuza mzunguko wa fedha na kutoa nafasi ya elimu ya juu kwa vijana wetu,” amesema Wambura.
Kwa mujibu wa takwimu, Geita ina jumla ya majimbo tisa ambapo saba hayana upinzani.