Wanahisa wa Benki ya CRDB waridhishwa na uongozi wa Dk Nsekela, wataka aendelee kuingoza benki hiyo
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori (katikati) akiongoza Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB. Wengine pichani ni Dk Donald Mmari, Makamu Mwenyekiti ( kulia), Dk Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB (wa pili kushoto), Fredrick Nshekanabo, Ofisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB (wa kwanza kushoto) na Pascal Mihayo, Katibu wa Benki na Mkurugenzi wa Sheria wa Benki ya CRDB.
Wanahisa wa Benki ya CRDB wameeleza matumaini yao ya kuona Mkurugenzi Mtendaji, Dk Abdulmajid Nsekela akiendelea kuiongoza wa Benki hiyo hata baada ya ukomo wa kawaida wa miaka 10 ya uongozi, wakiamini kuwa bado ana nguvu, maono, uzoefu na uwezo mkubwa wa kuendelea kuipeleka benki hiyo katika hatua nyingine ya mafanikio makubwa zaidi.
Wanahisa hao wanaeleza kuwa sababu kubwa inayowafanya kuwa na imani kubwa na uongozi wa Dk Nsekela ni kiwango kikubwa cha thamani ambacho wamekipata kupitia uwekezaji wao ndani ya Benki ya CRDB katika kipindi chake cha uongozi.
Wakati Dk Nsekela anachukua uongozi wa Benki ya CRDB mwaka 2018, thamani ya hisa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam ilikuwa wastani wa Sh 95 kwa hisa, lakini kufikia Aprili mwaka 2026 thamani hiyo ilikuwa imefikia wastani wa Sh 3,000 kwa hisa, hatua ambayo wanahisa wengi wanaielezea kama moja ya safari kubwa zaidi ya ukuaji wa thamani kuwahi kushuhudiwa katika sekta ya fedha nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Abdulmajid Nsekela akiwasilisha taarifa ya Menejimenti kwa mwaka 2025 katika Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa benki hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimatifa wa Arusha (AICC), Mei 16, 2026.
Kwa upande wa gawio, mwaka 2018 wanahisa walilipwa Shilingi 5 kwa hisa, lakini kutokana na matokeo makubwa ya kihistoria yaliyopatikana mwaka jana 2025, wanahisa walipitisha gawio la Sh 90 kwa kila hisa, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 1000. Benki hiyo pia imeendelea kuwa miongoni mwa kampuni zenye thamani kubwa zaidi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ikiwa na thamani ya soko inayozidi Dola za Marekani bilioni 2.8, jambo ambalo limeendelea kuongeza imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya Tanzania.
Mzee Godfrey Mosha mmoja ya wanahisa waanzilishi wa Benki ya CRDB tokea mwaka 1996 amesema tokea awe mwanahisa hajawahi kushuhudia ukuaji mkubwa wa thamani ya wanahisa na biashara ya benki hiyo kama ambavyo imetokea katika kipindi cha uongozi wa Dkt. Nsekela. “Hakika tumeshuhudia ukuaji wa ajabu na wakihistoria katika sekta ya fedha nchini,” alisema.
“Licha ya faida ya benki yetu kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 1000 tangu Dk Nsekela alipochukua hatamu ya uongozi, jumla ya mali za Benki ya CRDB zimefikia Sh 23.9 trilioni mwaka 2026 kutoka takribani Sh 7.6 trilioni mwaka 2018.
Viongozi wastaafu wa Benki ya CRDB wakifuatilia kwa karibu taarifa ya wakurugenzi na Ripoti ya Fedha kwa mwaka 2025 wakati wa Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB. Kutoka kushoto ni Martin Mmari, Mwenyekiti Mstaafu wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dk Ally Laay, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, na Dk Charles Kimei, Mkurugenzi Mtendaji Mstaafu wa Benki ya CRDB.
Amana za wateja zimeongezeka kutoka takribani Shilingi trilioni 4.8 mwaka 2018 hadi kufikia Sh 16.2 trilioni, mikopo ikikua kutoka takribani Sh 3.6 trilioni hadi kufikia Sh 14.7 trilioni. Huu ni ukuaji wa ajabu hatupaswi kumuacha kijana huyu aondoke mapema wakati bado ana nguvu za kutupelekea katika mafankio zaidi,” alisema Mzee Mosha katika Mkutano huo Mkuu wa 31 wa Wanahisa.
Taarifa ya mwaka ya Benki ya CRDB inaonyesha ukuaji huu umeifanya Benki ya CRDB kuendelea kuongoza soko la fedha nchini ikishika soko la benki kwa asilimia 28 ya amana zote za wateja nchini, asilimia 27 ya mali zote za sekta ya benki, asilimia 29 ya mikopo iliyotolewa na taasisi za fedha pamoja na asilimia 30 ya faida baada ya kodi miongoni mwa zaidi ya benki 40 zilizopo nchini. Kwa wanahisa wengi, takwimu hizi si tu alama ya mafanikio ya biashara, bali ni ushahidi wa uongozi wenye maono makubwa na uwezo wa kutekeleza mikakati kwa ufanisi.
Katika Mkutano huo Mkuu, sauti ya wanahisa ilikuwa moja; pongezi kwa matokeo yaliyopatikana na matumaini makubwa kuhusu mustakabali wa benki hiyo. Wengi wao walieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka minane iliyopita yanaonyesha wazi namna ambavyo uongozi imara, wenye maono na uthubutu unavyoweza kubadilisha taasisi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori akiwasilisha taarifa yake kwa mwaka 2025 katika Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Benki hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimatifa wa Arusha (AICC), Mei 16, 2026 ambapo Bodi ya Wakurugenzi iliwasilisha pendekezo la gawio la Sh. 90 kwa hisa ambalo lilipitishwa kwa pamoja na wanahisa.
Akizungumza katika mkutano huo Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye alisema “Katika ulimwengu wa fedha duniani kote, Afisa Mtendaji Mkuu kama hana matatizo na anafanya vizuri kwa viwango hivi vya Dk Nsekela huwa hawambadilishi kirahisi kwa sababu ukimbadilisha hisa zinashuka, lakini pia utendaji wa taasisi unaweza kushuka kwa sababu imani ya wateja na wawekezaji wengi mara nyingi ipo kwenye maono na uongozi imara unaonyeshwa na Afisa Mtendaji Mkuu.”
Wanahisa wengi wamekuwa wakitaja mkakati wa biashara wa “Evolve” kama moja ya hatua muhimu zaidi zilizobadilisha sura ya Benki ya CRDB. Kupitia mkakati huo wa miaka mitano (2023/27), Benki hiyo imefanikiwa kuimarisha mifumo ya kidijitali, kuongeza ujumuishi wa kifedha, kupanua huduma zake nje ya mipaka ya Tanzania, kuboresha uzoefu wa wateja na kuongeza thamani kwa wanahisa kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa hapo awali.
Hivi sasa, zaidi ya asilimia 98 ya miamala yote ya benki hiyo inafanyika nje ya matawi, hatua inayoonyesha mafanikio makubwa ya uwekezaji katika teknolojia. Aidha, asilimia 50 ya akaunti mpya sasa zinafunguliwa kupitia majukwaa ya kidijitali huku asilimia 40 ya miamala yote ikifanyika nje ya muda rasmi wa kazi wa matawi. Mabadiliko haya yameifanya Benki ya CRDB kuwa moja ya taasisi za fedha zilizoongoza katika mageuzi ya kidijitali Afrika Mashariki.
Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Fredrick Sumaye akichangia mada katika Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Benki hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimatifa wa Arusha (AICC), Mei 16, 2026.
Benki ya CRDB pia imeendelea kupanua ushawishi wake nje ya Tanzania. Kupitia uwekezaji katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi pamoja na uwepo wake Dubai, benki hiyo imeendelea kuwa daraja muhimu la biashara linalounganisha Afrika Mashariki, Afrika ya Kati, Ghuba ya Uarabuni pamoja na masoko ya Asia. Hatua hiyo imeongeza fursa kwa wafanyabiashara, wawekezaji na wajasiriamali wa Tanzania kupata masoko mapya ya kikanda na kimataifa.
Katika umri wa miaka 54 pekee, wengi wanaamini kuwa Dk Nsekela bado ana nguvu, uzoefu, maono na uwezo wa kuendelea kuiongoza benki hiyo kuelekea hatua nyingine kubwa zaidi ya ukuaji. Wanaamini kuwa baada ya mafanikio ya mkakati wa “Evolve” unaotarajiwa kukamilika mwaka 2027, benki hiyo ina nafasi kubwa zaidi ya kufanya mageuzi makubwa katika ukanda wa Afrika ikiwa itaendelea kujengwa juu ya msingi imara wa uongozi, ubunifu na nidhamu ya kiutendaji.
“Tunaimbo Serikali yetu sikivu, itusikilize sisi wanahisa wa Benki ya CRDB kwani bado tunaimani na Dk Nsekela anauwezo wa kutufikisha katika mafanikio makubwa zaidi tunapoelekea kuanza na kutekeleza mkakati mpya wa biashara utakaoanza mwaka 2028/32,” amesema Mzee Chedego moja ya wanahisa waanzilishi huku akisema kwa utendaji alioonyesha Dk Nsekela ni ngumu kwa wanahisa kumuacha aondoke.
Mwanahisa mwanzilishi wa Benki ya CRDB, Godfrey Mosha akitoa mchango wake katika Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Benki hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimatifa wa Arusha (AICC), Mei 16, 2026. Mzee Mosha ni kati ya wanahisa wengi ambao wamependekeza Dk Nsekela kuendelea kuongoza Benki hiyo kutokana na mafanikio makubwa ambayo benki hiyo imeyapata tokea aliposhika hatamu.
Hata hivyo, wanahisa hao wanaheshimu sheria zilizowekwa na serikali pamoja na mamlaka za udhibiti, na kusema kuwa maombi yao ni kwa maslahi mapana ya Benki yao ya CRDB na mustakabali mpana wa sekta ya fedha na Taifa kwa ujumla. Maombi ya wanahisa yameungwa zimeungwa mkono pia na baadhi ya viongozi wastaafu wa sekta ya fedha na wanahisa wakubwa akiwamo Dkt. Charles Kimei pamoja na Dk Ally Laay, ambao wamekuwa wakieleza kuvutiwa kwao na kasi ya ukuaji, uthabiti wa utendaji wa Benki yao.
Katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, Benki ya CRDB imeandika historia mpya kwa kuongoza katika viashiria vyote vikuu vya kiutendaji nchini. Benki hiyo ilirekodi faida baada ya kodi ya Sh 206 bilioni, kiwango kikubwa zaidi kuwahi kufikiwa na benki nchini ndani ya robo ya kwanza.
Kampuni zake tanzu nazo zimeendelea kufanya vizuri ambapo CRDB Bank Burundi ilipata faida ya Sh 12.9 bilioni, CRDB Bank DR Congo faida ya Sh 828 milioni huku CRDB Insurance ikirekodi faida ya Sh 1.8 bilioni. Kwa upande wa CRDB Bank Foundation, imeendelea kuwa chombo muhimu cha uwezeshaji wa wananchi nchini kupitia programu ya IMBEJU, huku zaidi ya wanufaika milioni 1 wakiwezeshwa.
Katika mazingira hayo ya utendaji, wanahisa wameadhimia kuunda jopo la ushauri linaloongozwa na Mzee Gachuma kwa lengo la kuwasilisha maoni yao kwa heshima na kwa kufuata taratibu zote stahiki kwa serikali kuhusu matarajio yao ya kuona uzoefu na maono ya Dk Nsekela yakiendelea kuisaidia benki hiyo katika hatua inayofuata ya ukuaji.
Kwa wanahisa wengi, mjadala huu hauhusu mtu mmoja pekee, bali unahusu uthabiti wa taasisi, mwendelezo wa mafanikio na kulinda kasi ya ukuaji ambayo imeifanya Benki ya CRDB kuwa taasisi ya mfano katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.