Vijana 400 wanufaika na mradi wa uvuvi endelevu kupitia programu ya TangaYetu

Muonekano wa Jongoo bahari baada ya kuvuliwa.
Miaka michache iliyopita, Shali Bakari Zengo na wenzake wa kikundi cha Uvuvi Endelevu walikuwa hawana kazi ya kufanya. “Tulikuwa tunaamka bila kujua pa kwenda,” anasema Shali. Lakini sasa, kupitia mashua ya kisasa (Fiber-glass boat) waliyopewa na programu ya TangaYetu, vijana hawa huamka alfajiri, kwenda baharini kuvua samaki na kurudi na matumaini mapya.
Kupitia mradi wa uwezeshaji vijana kiuchumi kupitia uvuvi, chini ya programu ya TangaYetu, vijana 400 waliwezeshwa kushiriki katika shughuli endelevu za uchumi wa buluu ikiwemo ufugaji wa kaa na majongoo baharii, ukaushaji wa dagaa kwa kutumia vichanja, uvuvi kwa mashua za kisasa, pamoja na kilimo cha mwani na samaki wa maji baridi.
Kwa mujibu wa Simon Mdende, Afisa Maendeleo wa Jiji la Tanga, “Mradi huu uliibua ari mpya kwa vijana na kuwapa zana za kujiendeleza. Tumeona vijana wakihama kutoka kwenye utegemezi hadi kwenye ujasiriamali wa baharini. Ni mfano halisi wa maendeleo jumuishi yanayowezesha vijana.”
Omary Muhammed, Afisa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anaeleza kwamba mradi huu ulitekelezwa kwa vipengele sita vikuu: utoaji wa vifaa vya uvuvi zikiwemo boti 14, kuendeleza mashamba ya samaki, ufugaji wa kaa, ukaushaji wa samaki, kilimo cha mwani na majongoo bahari, pamoja na uboreshaji wa Kituo cha Machui Hatchery kilichopo Tanga.
“Tuliona mafanikio makubwa, hasa kwenye ufugaji wa kaa,” anasema. “Tulitoa mafunzo ya namna ya kutunza kaa na kutumia maji ya chumvi kwa mchakato wa kuyavua magamba (molting), jambo muhimu kwa ufanisi wa ufugaji huu”.

Muonekano wa Kaa baada ya kuvuliwa.
Kwa kikundi cha Shali, mafanikio yamekuwa ya kweli. “Mradi umetufundisha kuendesha mashua, kuitunza, na pia kuweka akiba kwa ajili ya matengenezo. Leo tunaweza kujitegemea,” anasema Shali. Kikundi chake kilipokea mashua za kisasa (Fibre-glass boat) na vifaa vya kuvulia, na sasa wanapata kipato cha kutosha kusaidia familia zao. “Faida kubwa ni kwamba sasa tunaweza kusaidia familia zetu,” anasisitiza Shali.
Mradi haukuishia kutoa vifaa pekee. Vijana walipatiwa pia elimu ya usimamizi wa fedha, ujuzi wa kiufundi, na mbinu bora za uhifadhi wa samaki. Pia walihimizwa kutunza asilimia 20% ya mapato yao kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za baadaye katika bishara yao.
Kwa upande wa kilimo cha mwani na majongoo bahari, zaidi ya wanawake 100 walipewa mafunzo na vifaa vya kuanzisha mashamba ya mwani. Ufugaji wa majongoo bahari ulianzishwa kwa mara ya kwanza katika eneo hilo, na vijana walifundishwa jinsi ya kuandaa mazingira, kuhifadhi maji, na kuendeleza viumbe hao nyeti wa baharini.
Katika Kituo cha uzalishaji na ukuzaji wa viumbe maji cha Machui, vifaa vya maabara, matangi ya maji, na mashine muhimu zilisambazwa ili kusaidia uzalishaji wa kaa na majongoo bahari. Ingawa bado changamoto ya uhai mdogo wa viumbe wachanga ipo, kituo hiki kimekuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa baharini waliopo Tanga.
“Mradi huu umeweka msingi mzuri wa uchumi wa buluu. Vijana sasa wanachangia si tu katika pato la familia, bali pia katika kulinda rasilimali za bahari kwa vizazi vijavyo,” anasema Omary Muhammed, Afisa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Katika kijiji cha Mwarongo, Kikundi cha Wanawake cha Maua kilipokea mashua na kupewa masharti ya kuwahamasisha wasichana kushiriki uvuvi. Matokeo yake, zaidi ya wasichana 50 walishiriki mafunzo na sasa wanavua, hatua muhimu katika kuvunja vizingiti vya kijinsia.
“Kwa sasa tuna akaunti ya kikundi yenye zaidi ya shilingi milioni 4,” anasema Bay Juma, katibu wa kikundi cha Maua. “Ni jambo ambalo hatukuwahi kulifikiria awali.” Hii inaonesha jinsi mradi ulivyojikita si tu katika shughuli za kiuchumi, bali pia uwezeshaji wa wanawake na usawa wa kijinsia.
Katika kikundi cha Vijana cha Chimbachi, vijana walijenga vizimba 4,000 kwa ajili ya kufugia kaa na walivuna kilo 80 za kaa kwa mauzo ya shilingi milioni 1.2. Fedha hizo zilitumika kuendeleza shughuli zaidi na kuongeza uzalishaji. Hii ni mifano hai ya mabadiliko yanayoletwa na uwekezaji katika maarifa, vifaa, na ufuatiliaji thabiti.
Leo hii, kupitia TangaYetu, vijana kama Shali wamebadilisha maisha yao. Wamepata kipato, ujuzi, na matumaini. Bahari kwao si tena mandhari ya kuangalia na kupunga upepo ufukweni, bali ni shamba la ndoto na fursa.
Programu ya TangaYetu inafadhiliwa na Fondation Botnar na kutekelezwa na kampuni ya INNOVEX (www.innovexdc.com) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga—ikiifanya Tanga kuwa jiji ambalo vijana wanastawi.