Siku ya Hedhi Salama 2025: Safari ya ujenzi wa mazingira salama kwa hedhi kwa kila mwanamke na msichana

Mkurugenzi Mkazi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga.
Katika kuadhimisha Siku ya Hedhi Salama Duniani mwaka 2025 chini ya kaulimbiu “Kwa Pamoja kwa Hedhi Salama," WaterAid Tanzania imeweka wazi malengo yake ya kuhakikisha kila mwanamke na msichana nchini anaishi katika mazingira yanayomuwezesha kujistiri kwa staha na usalama wakati wa hedhi.
Mazingira salama kwa ajili ya hedhi sio tu wazo lililopo hewani, bali ni lengo linalotekelezeka ambalo msingi wake unaanzia kwenye upatikanaji wa uhakika wa maji safi, vyoo vyenye staha, sehemu za kujistiri na taarifa sahihi.
Kuanzia mashuleni, vituo vya afya hadi maeneo ya masoko, WaterAid Tanzania inapambana kupaza sauti, kuboresha upatikanaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira, na kuhakikisha kuwa hedhi haiwi kikwazo katika elimu, mahala pa kazi au ushiriki wa wanawake na wasichana katika jamii zao.
Mkurugenzi Mkazi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga amefanya mazungumzo na mwandishi wa gazeti hili kuhusiana na siku hiyo na alikuwa na majibu yafuatayo:-
Kaulimbiu ya Siku ya Hedhi Salama ya mwaka huu ni "Kwa Pamoja kwa Hedhi Salama." Mazingira salama kwa hedhi yanabeba tafsiri gani kwa WaterAid Tanzania?
Anna: Mazingira salama kwa hedhi ni ile hali ambayo kila mwanamke na msichana anaweza kujistiri kwa usalama, staha na usafi – hali inayoongeza kujiamini kwao bila kulazimika kukatisha masomo, kusimama kufanya kazi au kuishi kwa uhuru katika jamii. Kwa WaterAid Tanzania, hii inamaanisha wanawake na wasichana wanaweza kupata huduma muhimu kama maji safi, vyoo rafiki kwa makundi ya jinsi zote, na taarifa sahihi kuhusu afya ya hedhi.
Wanawake na wasichana wanaposhindwa kuhudhuria masomo au kuingia kazini kwa sababu ya hedhi, hupoteza fursa ya kujifunza, kujipatia kipato, na kuleta mabadiliko. WaterAid Tanzania tunahakikisha shule, vituo vya afya na maeneo ya umma yanapata huduma muhimu kama maji safi, vyoo bora, vifaa vya kunawa mikono, maeneo ya faragha kwa ajili ya kujistiri wakati wa hedhi, na taarifa sahihi zenye msaada vyote hivi kwa njia endelevu.
Miundombinu ya umma inaposaidia afya ya hedhi, wasichana wataweza kuhudhuria shule mara kwa mara na wanawake wataweza kwenda kazini na kuishi kwa staha katika jamii. Tunaamini hili ni jambo muhimu kwa kufanikisha usawa wa kijinsia na maendeleo jumuishi nchini mwetu.
Kwa nini rasilimali maji ni muhimu katika kufikia hedhi salama?
Anna: Maji ni msingi wa hedhi salama. Kupitia maji, wanawake na wasichana wanaweza kunawa mikono, kusafisha miili yao, na kujihisi safi na huru wakati wa hedhi. Bila maji safi, kujistiri wakati wa hedhi huwa ni jambo hatarishi, linalokosesha amani na linaloweka rehani utu wa mtu. Mashuleni, sehemu za kazi, masoko, na vituo vya afya, upatikanaji wa maji ya uhakika ni msingi wa mazingira salama ya hedhi.
Linapokuja suala la hedhi salama, kwa nini unadhani vyoo bora vinamuwezesha mwanamke au msichana kushiriki na kujitokeza mahala popote mbele ya jamii?
Anna: Vyoo bora ambavyo ni salama, safi, vyenye faragha na vinavyopatikana kwa urahisi vinamwezesha msichana au mwanamke kujistiri wakati wa hedhi bila uwoga wala aibu. Tunapokuwa na vyoo vyenye maji na sehemu za kutupa taulo za kike, tunaonyesha utu na ulinzi.
Wasichana wana uwezekano mkubwa wa kuhudhuria masomo na kubaki shuleni, na wanawake kuendelea kufanya kazi na kushiriki katika masuala ya kijamii kwa uhuru. Ni hatua rahisi lakini yenye nguvu katika kuelekea usawa wa kijinsia na ushirikishwaji.
Swali: Tuambie zaidi kuhusu jitihada za WaterAid Tanzania, hususan zinazohusiana na afya ya hedhi mashuleni na katika vituo vya afya
Anna: WaterAid Tanzania tunahakikisha shule na vituo vya afya vina maji safi, vyoo bora na usafi binafsi. Mashuleni, tumejenga vyoo rafiki kwa makundi ya jinsi zote vyenye vituo vya kunawa mikono na maeneo ya faragha kwa ajili ya hedhi salama. Katika vituo vya afya, kazi yetu ni kuhakikisha wafanyakazi wa kike, wagonjwa na walezi wanakuwa kwenye mazingira salama wanapojistiri wakati wa hedhi. Jitihada hizi zimeongeza mahudhurio, faraja, na utu hususan kwa wasichana balehe na wanawake.
Tuambie zaidi kuhusu MHM kwa wasichana shuleni na namna klabu za SWASH zinavyosaidia kubadilisha hali iliyopo
Anna: Usimamizi wa Hedhi Mashuleni (MHM) una nafasi muhimu katika kuwafanya wasichana wabaki darasani, kuongeza ufaulu na kujiamini. Klabu za SWASH (Vikundi vya Huduma za Maji Safi, Vyoo Bora na Usafi Binafsi Mashuleni) huhamasisha usafi, huongeza uelewa kuhusu hedhi, na kutoa msaada wa rika.
Klabu hizi husaidia kuvunja ukimya, kurahisisha mazungumzo kuhusu afya ya hedhi, na kuhakikisha mazingira ya shule yanakidhi mahitaji ya wasichana – na wavulana pia. Katika maeneo yenye klabu za SWASH, tumeona ongezeko la kujiamini miongoni mwa wasichana na mahudhurio ya mara kwa mara shuleni hata wakati wa hedhi, pamoja na kuboresha utamaduni wa kuzingatia usafi miongoni mwa wanafunzi.
Changamoto zipi jamii inakutana nazo kuhusu hedhi salama, hususan wanawake walioko kwenye jamii hizo? Na WaterAid Tanzania inakabiliana nazo vipi?
Anna: Maeneo mengi ya umma kama masoko, vituo vya mabasi na vituo vya kijamii hayana maji safi wala vyoo vinavyofanya kazi. Hii inawafanya wanawake washindwe kujistiri wakati wa hedhi wakiwa kazini au katika shughuli zao za kila siku, hivyo wanalazimika kubaki nyumbani au kutumia njia mbadala ambazo ni hatarishi.
WaterAid hivi karibuni tumekabidhi vyoo rafiki kwa makundi ya jinsi zote katika masoko mawili ya Ngaramtoni, jijini Arusha. Hatua hii imeongeza kujiamini, usalama na ushiriki wao wafanyabiashara wanawake katika uchumi.
Ungependa watu waelewe nini kuhusu afya ya wanawake hususan katika Siku ya Hedhi Salama Duniani kwa mwaka 2025? (Wito kwa jamii)
Anna: Wanawake wanahitaji huduma bora: Kampeni ya What Women Want ilipohoji wanawake milioni 1.2 duniani kote, ikiwemo Tanzania, kuhusu kile wanachotaka kutoka kwenye huduma za afya ya uzazi na mama, walitaja huduma zenye staha, maji safi, vyoo bora na usafi wa mazingira kama vipaumbele vyao vya msingi.
Kwa kuwa wanawake wako hatarini kupata maambukizi, hivyo kuhimiza hedhi salama kunachangia kuimarisha afya yao kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na afya ya uzazi na afya ya vijana balehe.
Kama ungepata nafasi moja ya kutoa rai kwa Mamlaka zenye nafasi ya kushughulikia jambo hili, ingekuwa ni ipi?
Anna: Serikali zina uwezo wa kuleta mabadiliko ya kweli. Na vyombo vya habari vina uwezo wa kuzifanya zisikilize kero. Ninatoa wito kwa wadau wa maendeleo katika sekta za afya, elimu, jinsia na WASH pamoja na Serikali ya Tanzania kuwekeza fedha katika maji safi, vyoo bora, huduma za usafi katika shule, maeneo ya umma na vituo vya afya — ili kila mwanamke na msichana aweze kujitokeza na kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi kwa mafanikio mahala popote, muda wowote ule.
Hadithi za mafanikio
Safari ya binti mmoja: Kutoka kuwa na aibu hadi kuwa na ndoto
Katika shule ya msingi iliyopo katika kijiji cha Laghanga, ipo habari ya binti mmoja ambaye alikuwa anakosa amani pindi tu mzunguko wake wa hedhi unapofika. Shuleni kwao hakukuwa na maji safi, vyoo vilikuwa vichafu mno na hakukuwa na vyumba maalumu vya wasichana kujistiri.
Leo hii, kila kitu kimebadilika. Nyuma ya haya mabadiliko yote yupo Shirika la WaterAid Tanzania, kupitia mradi wao usambazaji huduma za maji safi, vyoo bora na usafi wa mazingira (WASH) ambapo shule yao imebahatika kupata vyoo rafiki kwa makundi ya jinsi zote, vyumba vya kubadilishia taulo za kike, vituo vya kunawia mikono na huduma za uhakika za maji safi.
Sauti ya mwalimu aliyevunja ukimya
Katika Wilaya ya Kisarawe, yupo mwalimu aliyeamua kupaza sauti katika jamii ambayo kuzungumzia masuala ya hedhi ni mwiko mpaka pale sherehe za kimila zitakapofanyika (ngoma).
Kupitia klabu za shule za mradi wa WASH, hivi sasa anaelimisha vijana (wasichana na wavulana) kuhusu masuala ya hedhi salama. Uthubutu wake umekuwa na mchango mkubwa katika kujenga uelewa wa vijana kuhusu afya ya hedhi.
“Licha ya uwepo wa mila ya ‘ngoma’ inayozuia mazungumzo kuhusu hedhi, mimi hukaa na wasichana na kuzungumza nao. Kupitia klabu ya WASH, navunja ukimya. Wasichana wanapata taarifa sahihi kunakowajengea kujiamini na kuuliza maswali,” anasema Grace.
Uwezeshaji wanawake maeneo ya masoko
Jitihada za WaterAid Tanzania haziishii mashuleni, bali zinakwenda hadi kwa wanawake na wasichana waliopo maeneo ya masoko. Wilayani Arusha, kwenye maeneo ya Oltrumet na Olmotony, vyoo viwili vya kisasa (vyoo rafiki kwa makundi ya jinsi zote) vilijengwa vikihudumia watumiaji wa masoko zaidi ya 1000 kila siku.
Vyoo vina nafasi kwa wanawake na wasichana katika masoko kutumika wakati wa mizunguko yao ya hedhi vikiwa na maeneo ya kuhifadhia taka, kuvifanya kuwa si tu vyoo bali ni ishara ya utu, afya na fursa.