Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matumizi ya Sayansi: Kuboresha huduma za afya ya mimea kwa ajili ya usalama wa chakula na biashara Tanzania

Miongoni mwa zana za kisasa za kisayansi zilizopitishwa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya ufuatiliaji na matumizi ya viuatilifu ni pamoja na ndege zisizo na rubani zinazoonyeshwa hapa kama mfano muhimu wa teknolojia ya kuimarisha afya ya mimea na kulinda usalama wa chakula.




Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Usalama wa Chakula Duniani yenye kaulimbiu “Matumizi ya Sayansi”, Tanzania inaendeleza juhudi zake katika kuhakikisha kuwa mifumo ya chakula inakuwa salama, bora na yenye ushindani wa kimataifa kwa kutumia njia za kisayansi kwenye kilimo na usalama wa chakula.

Kwa msaada kutoka kwa washirika wa kimataifa kama vile Umoja wa Ulaya, Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Tanzania inatekeleza Mradi wa Kuimarisha Huduma za Afya ya Mimea kwa ajili ya Uimarishaji wa Usalama wa Chakula Tanzania (STREPHIT) ambapo ni mpango wa mageuzi unaolenga kuimarisha huduma za afya ya mimea, kulinda mazao ya kilimo na kuboresha nafasi ya Tanzania katika biashara ya chakula kimataifa.

Usalama wa chakula unaanza na sayansi. Maendeleo ya kisayansi yanatuwezesha kugundua vichafuzi katika chakula, kuzuia magonjwa yanayosababishwa na vyakula na kuhakikisha kwamba tunafuata viwango vya usalama vya kimataifa. Kupitia uwekezaji katika mafunzo ya kisayansi, teknolojia za uchunguzi wa wadudu na maabara za kisasa, Tanzania inaiwezesha sekta ya kilimo kuwa na zana za kisasa ili kulinda afya za wananchi na kuimarisha fursa za biashara.

Mapinduzi ya kidijitali yameboresha biashara ya kimataifa, ikiwemo biashara ya kilimo. Kulingana na ripoti ya Mkataba wa Kimataifa wa Kulinda Mimea (IPPC) ya mwaka 2023, takriban vifurushi bilioni 161, sawa na vifurushi 5,102 kwa sekunde, vilisafirishwa duniani kote mwaka 2022. Ongezeko hili la biashara ya mtandao limeleta fursa na changamoto kadhaa.  

Changamoto mojawapo ni kuongezeka kwa mauzo ya mbegu, mimea na pembejeo za kilimo mtandaoni yasiyofuata utaratibu ambazo nyingi husafirishwa moja kwa moja kwa watumiaji bila kupitia taratibu za kawaida za ukaguzi. Jambo hili linatatiza mataifa mengi ikiwemo Tanzania na husababisha uvamizi wa wadudu waharibifu na magonjwa yanayoharibu mazao, kuhatarisha usalama wa chakula na kudhoofisha fursa za kuuza bidhaa za kilimo nje.

Mradi wa STREPHIT umeleta faida kubwa katika kushughulikia changamoto hizi. Kuanzia utoaji wa zana za kisasa za ukaguzi hadi kutoa mafunzo kwa wakaguzi wa udhibiti wa viuatilifu na mbinu bora za ukaguzi, Tanzania inahakikisha kuwa wataalamu wa afya ya mimea wana vifaa vya kutosha vinavyowawezesha kutambua, kutathmini na kupunguza matishio ya usalama wa chakula katika mnyororo mzima wa uzalishaji.

Zaidi ya hayo, mradi huo umewezesha ushirikiano wa kikanda na kuruhusu Tanzania kufanya kazi pamoja na mataifa mengine ya Afrika na taasisi za kimataifa ili kubuni mbinu zinazotumia sayansi na teknolojia kupata mifumo salama ya chakula na biashara za kilimo.

Ndizi ni moja ya vyakula vikuu vinavyolimwa katika zaidi ya mikoa mitano Tanzania. Zao hilo lina jukumu muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula na hutumika kama chanzo kikuu cha kipato kwa wakulima wengi wadogo.

Kadri minyororo ya usambazaji wa chakula duniani inavyozidi kukumbwa na changamoto, Siku ya Usalama wa Chakula Duniani mwaka huu inatumika kama wito wa kuchukua hatua, ikielekeza kuwa, sayansi lazima itumike kuzuia na sio kutatua changamoto za usalama wa chakula. Serikali zinatakiwa kuweka sera zinazoongozwa na mbinu za kisayansi, kuboresha ukusanyaji wa taarifa na kuwekeza katika utafiti na elimu ili kuwa na kanuni zinazotekelezeka kwa vitendo.

Wafanyabiashara na wauzaji bidhaa za chakula nje ya nchi lazima watoe mafunzo kwa wafanyakazi wao kuhusu usalama wa afya ya mimea, wasaidie mipango ya kushirikishana taarifa na watumie mbinu za kisayansi katika utunzaji, usindikaji, uhifadhi na usafirishaji wa chakula, ikijumuisha kufuata kanuni za kimataifa za usafi wa mazingira.

Wateja nao wana jukumu muhimu katika usalama wa chakula. Kwa kufuata viwango vilivyowekwa, kuweka chakula katika hali ya usafi, kukihifadhi katika mazingira salama na kutumia maji salama, kaya zinapaswa kuwa za kwanza katika ulinzi dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na chakula.

Dhamira ya Tanzania katika usalama wa chakula inakwenda zaidi ya afya za wananchi, ni hatua ya kimkakati ya kufungua masoko ya kimataifa. Kadri nchi nyingi zinavyosimamia viwango vya uagizaji wa chakula ili kuhakikisha ufuataji wa kanuni za usalama wa chakula duniani inaongeza kiwango cha mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Kwa kudumisha viwango vya usalama, kuondoa wadudu na vichafuzi na kutumia mbinu za kisayansi, Tanzania inaendelea kuwa nchi shindani kimataifa katika kilimo. Wakati sayansi ikiendelea kuchagiza sera za kitaifa za usalama wa chakula, Tanzania inaendelea kuweka alama kikanda ya namna mikakati inayotekelezeka kwa vitendo inavyoweza kuwalinda walaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuendeleza biashara ya kilimo.

FAO inapoadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwake Oktoba 16, 1945, inaendelea kuhimiza mabadiliko ya mifumo ya kilimo cha mazao ya chakula inayoongozwa na kanuni za uzalishaji bora, lishe bora, mazingira bora na maisha bora, bila kuacha mtu nyuma.

Siku ya Usalama wa Chakula Duniani mwaka huu inatumika kutukumbusha kwamba nyuma ya kila sahani salama ya chakula kuna mtandao shirikishi wa wakulima, wanasayansi, wadhibiti, wafanyabiashara na watumiaji, wanaofanya kazi kwa pamoja kisayansi ili kulinda afya zetu na kuhakikisha maisha endelevu ya baadaye.

Mwandishi

Victor Mapile

Mtaalamu wa Mawasiliano kwa Maendeleo-FAO