Kutoka kumsubiri mpaka kumfuata mteja – CRDB Bank Foundation inavyobadili huduma za benki nchini

Ofisa Tathmini na Ufuatiliaji wa CRDB Bank Foundation, Hafsa Msonga (wa kwanza kushoto) akiwa na wasichana waliopata ujauzito wa kwanza katika umri mdogo baada ya kukamilisha mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha inayotolewa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na UNFPA wilayani Bahi mkoani Dodoma.
Nilitaka kufungua akaunti ya benki wakati fulani lakini mahitaji ya nyaraka nilizoambiwa niambatanishe yalinikatisha tamaa. Nikaachana na huo mpango lakini sasa hivi naona ninyi (Benki ya CRDB) mmerahisisha utaratibu wenu, kwa namna hii mtatupata wananchi wengi ambao hatukuwa na vigezo hapo mwanzoni,” anasema Lucas Kapimpiti, mkazi wa Kijiji cha Ikola katika Wilaya ya Tanganyika mkoani Rukwa.
Kijiji cha Ikola kipo umbali wa zaidi ya kilomita 70 kutoka Mpanda, makao makuu ya Mkoa wa Rukwa ambako Kapimpiti angeweza kwenda kufungua akaunti ya benki iwapo angekamilisha masharti yote muhimu kama yanavyotakiwa.
Ili kukamilisha suala hilo angetakiwa kusimamisha shughuli nyingine zote za siku hiyo ili aipate akaunti ya benki kwa ajili ya kutunza fedha zake na kufanikisha miamala mingine muhimu kwake binafsi na biashara ya samaki wakavu anayoifanya.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa (kushoto) akiwa na Mwakilishi Mkazi wa UNFPA nchini, Mark Bryan Schreiner waliposaini mkataba wa makubaliano ya kuwawezesha kujikwamua kiuchumi wasichana waliopata mimba ya kwanza katika umri mdogo.
Changamoto alizokuwa anakabiliana nazo Kapimpiti zinafanana na za Rosemary Igondi, mjasiriamali mdogo anayeendesha biashara ya saluni ya wanawake Chamwino katika Mkoa wa Dodoma. Leo hii changamoto zao zimebaki historia baada ya kuunganishwa na programu ya IMBEJU inayoendeshwa na taasisi ya CRDB Bank Foundation (CBF).
Kampimpiti akinufaika na kampeni ya ‘Imbeju Jiwezeshe’ inayoendeshwa na taasisi hiyo, na Rosemary akinufaika na mpango mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha kwa wanawake waliopata ujauzito katika umri mdogo ambayo CBF inayaendesha kwa kushirikiana na Mfuko wa Idadi ya Watu wa Umoja wa Mataifa (UNFPA).
Kwa umri wake wa miaka 21 sasa, Rosemary anasema “sijawahi kuingia benki ingawa nina jishughulisha kumlea mwanangu mwenye umri wa miaka mitano sasa. Nilianza kujitegemea tangu nikiwa mdogo baada ya kupata ujauzito nikiwa kidato cha tatu. Kipindi hicho sikuwa na nyaraka zozote za kuniwezesha kufungua akaunti ya benki hivyo nikaendelea na harakati nyingine za maisha.”
Rosemary na washiriki wenzake wote 37 hawakuwa na akaunti jambo lililopelekea waandaaji wa mafunzo hayo kuwapa uzoefu tofauti kwa kuwapeleka kati tawi la Benki ya CRDB Chamwino ili wajionee mazingira halisi na waanze kutumia huduma za benki ili kujiongezea fursa za kukuza biashara ndogo wanazozifanya.
“Washiriki 19 kati yao walifungua Akaunti ya Imbeju na baadhi ambao hawaakuwa na kitambulisho cha taifa walisaidiwa na benki baada ya kuwasiliana na NIDA (Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa) kujaza fomu ili wakipate. Walifurahi sana. Ilivutia kuwaona wakiingia benki kwa mara ya kwanza tangu wazaliwe,” anasema Lolabona Lema, Afisa Uwezeshaji Program ya Imbeju - CRDB Bank Foundation.

Wasichana waliopata ujauzito wa kwanza katika umri mdogo wakishiriki kutoa michango yao ya mawazo katika mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha inayotolewa na Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na UNFPA wilayani Bahi mkoani Dodoma.
Baada ya kufungua akaunti yake ya Imbeju, Rosemary anasema hakuwahi kwenda benki ili afungue akaunti kutokana na taarifa alizokuwa anazisikia mtaani kwamba unahitaji kuwa na viambatanisho vingi ili kukamilisha hilo.
“Hela zangu huwa nazitunza ndani au kwenye simu. Mara chache huwa nampa mtu anitunzie. Ni mtu ninaye mwamini na nikizihitaji ananipa nifanyie shughuli zangu. Ila kuanzia leo nitakuwa napeleka benki hela zote ninazotaka kuzitunza. Nimefurahi kupata akaunti na mimi sasa hivi nafanana na wafanyakazi wa serikalini,” anasema Rosemary huku akicheka kwa furaha isiyomithirika.
Elimu katika mazingira rafiki
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa anasema Watanzania wengi hawana elimu ya fedha ndio maana taasisi anayoiongoza imeweka mkakati wa kuwafuata mahali walipo na kuwaelimisha.
“Maisha yana changamoto nyingi ambazo zinamnyima mtu nafasi ya kujifunza mambo ya msingi ukiwamo ujasiriamali na kupata elimu ya fedha. Kwa vijana wanaokutana changamoto hizi katika umri mdogo hujikuta wakipambana kupata ridhiki ya kila siku hivyo kutofika benki kabisa. Hii ndio sababu CRDB Bank Foundation tunawafuata mahali walipo,” anasema Tully.

Wanawake waliopata ujauzito wa kwanza wakiwa chini ya miaka 18 wilayani Chamwino mkoani Dodoma wakifurahi baada ya kutembelea tawi la Benki ya CRDB baada ya kushiriki mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha. Ziara hiyo iliwapa fursa ya kuingia ndani ya benki kwa mara ya kwanza tangu wazaliwe.
Mkurugenzi huyu anafafanua kwamba changamoto hizi zinawakuta vijana wote ambao unaweza kuwakuta sokoni, migodini, ziwani au kwenye mabwawa makubwa wakivua au kufanya biashara ndogondogo na maeneo mengine ambako watu wanajipatia kipato halali cha kuendesha maisha yao lakini kutokana na majukumu mengi waliyonayo wakakosa nafasi ya kwenda kufungua akaunti benki.
Licha ya udogo wa shughuli wanazozifanya wanawake, vijana na makundi maalumu ambayo CRDB Bank imejielekeza kwao, Tully anasema kuna fursa ya kukua na kujikwamua kiuchumi iwapo watapata mafunzo ya kuendesha shughuli zao kwa mfumo unaoeleweka kisha wakazirasmisha biashara walizonazo.
“Changamoto za kila siku ndizo zinatusaidia kubuni namna ya kukabiliana nazo. Watanzania wengi hawatumii huduma benki sio kwamba hawana vigezo bali wanakosa taarifa sahihi. Benki ya CRDB imeona isiendelee kuwasubiri mpaka watakapokuja wenyewe, kupitia CRDB Bank Foundation tunawafuata popote walipo na kuwahudumia.
Tunaamini utaratibu huu unawarahisishia kupata elimu kwani wanajifunza katika mazingira yao wakiwa wamezungukwa na watu wanaofahamiana. Wanaelewa na kuchukua uamuzi,” anasisitiza Tully.
Mkurugenzi huyo anasema jukumu la kufikisha elimu ya fedha na ujasiriamali kwa wananchi ni kubwa hivyo wanashirikiana na kila mdau ambaye wana maono yanayofanana kuhakikisha wanawafikia wananchi wengi kadri iwezekanavyo.

Ofisa Imbeju wa CRDB Bank Foundation, Lolabona Lema akitoa mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha kwa wanawake waliopata ujauzito wa kwanza wakiwa chini ya miaka 18 wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Katika kufanikisha mkakati huo, Tully anasema wanashirikiana na wabia wa ndani na wa nje akitolea mfano Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawke, Watoto, na Makundi Maalum, Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Kazi Ajira, Vijana, na Wenye Ulemavu, Mfuko wa Idadi ya Watu wa Umoja wa Mataifa (UNFPA), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na Tume ya TEHAMA (ICTC), pamoja na taasisi zinazosimamia vikundi vya kinamama kama vile Buta Vicoba Endelevu, Mbweni Women (MBWE) Group, na Bunju Women (BWE) Group.
“Kuna fursa nyingi ambazo mjasiriamali anaweza kunufaika nazo. Fursa hizi zipo kwenye eneo lake, mkoa mpaka taifa. Lakini sote tunafahamu kwamba Afrika sasa inalo eneo huru la biashara, huko nako Watanzania wanastahili kushiriki kuzichangamkia fursa zilizopo. Wabia tunaoshirikiana tunasaidiana kufungua fursa hizi kuanzia chini kabisa mpaka nje ya mipaka ya taifa letu,” anasema Tully.
IMBEJU Jiwezeshe ni mguu kwa mguu
Mkuu wa Kuendeleza Biashara Changa wa CRDB Bank Foundation, Fadhil Bushagama anasema wameelekeza nguvu kubwa kuhakikisha wanamfikia kila Mtanzania na kumpa elimu anayostahili ili kukuza biashara aliyonayo na kumpa maarifa anayostahili kwa ajili ya kuzisimamia fedha anazozipata kutoka kwenye shughuli zake.
Ili kufanikisha azma hiyo, anasema CRDB Bank Foundation inaendelea kuendesha mafunzo katika maeneo tofauti nchini kupitia wataalamu wake wanaozunguka mikoani. Kampeni hiyo ya kuzunguka miikoani, anasema ilianza Agosti 2024 katika mikoa ya nyanda za juu, kanda ya kusini, kanda ya Dares Salaam na sasa ipo katika kanda ya ziwa.
“Mwanzo tulikuwa tunatoa elimu katika kumbi maalumu lakini tuligundua tunahitaji kwenda mtaani ili kuwafikia watu wengi zaidi. Sasa hivi tumetanua wigo, tunawafuata kwenye maeneo yao iwe sokoni au stendi. Tunaongea na mtu mmojammoja akiwa kwenye eneo lake la kazi. Hii inakuwa rahisi kwake kufanya uamuzi kwa sababu anaelimika huku anaendelea kuwahudumia wateja wake,” anasema Bushagama huku akitolea mfano wa Lucas Kapimpiti, mkazi wa Kijiji cha Ikola katika Wilaya ya Tanganyika mkoani Rukwa ambaye amenufaika na mkakati huo.
Mfumo huu mpya, Bushagama anasema unawapa fursa wale wasio na wasaidizi kwenye biashara zao kuelimika na kuanza kuweka mipango ya kukuza kile wanachokifanya kwani sio kila mtu anaweza kuicha biashara yake japo kwa muda mfupi.
“Watu wanakimbizana kila wakati. Kwa hizi biashara ndogo, unaweza kukuta mtu mmoja tu ndio kila kitu. Hawezi kuiacha hata kwa dakika mbili akaenda kusikiliza semina. Kwa mfano mmachinga au bodaboda huwezi kumtoa kwenye biashara yake ukampeleka mahali akakae kwa saa moja mbili kwani akifanya hivyo atakuwa anapishana na hela. Hawa tunaongea nao wakiwa kwenye biashara zao. Tunawafungulia akaunti na watakapokuwa tayari wanakuja tawini kuomba mtaji wezeshi,” anasema.
Ili kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye shughuli za uchumi, CRDB Bank Foundation inatoa mafunzo ya ujasiriamali ili kumwezesha mshiriki kufahamu namna ya kuiinua biashara yake kutoka hatua moja kwenda nyingine, kutanua biashara anazozifanya ama ndani ya sekta aliyomo au kuingia kwenye sekta nyingine pia.
Vilevile, CBF inatoa elimu ya fedha ili kumwezesha mfanyabiashara mchanga kujua namna ya kusimamia fedha anazozipata kwa ajili ya matumizi yake binafsi, kuendeleza biashara yake na kukabiliana na changamoto ya kifedha inayoweza kujitokeza.
Baada ya kutoa elimu hii, kwa yule aliye tayari anaweza ufungua Akaunti ya Imbeju ili kuianza safari ya kuwa na taarifa rasmi za mapato na matumizi. Baada ya kukamilisha hatua hizi mihumu. Mhusika anaweza kuomba mtaji wezeshi unaoanzia shilingi 200,000 mpaka shilingi milioni 10 kwa wanawake. Ukomo wa mtaji wezeshi unaweza kuvuka hata shilingi milioni 30 kwa biashara na miradi bunifu ya vijana. Hii ni ile iliyobuniwa na vijana na ikathibitishwa na COSTECH au ICTC kwamba inayo manufaa kwa jamii.
Tangu kuanzishwa kwa programu ya Imbeju mwaka 2023, CRDB Bank Foundation imefanikiwa kutoa elimu ya fedha na mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake na vijana zaidi ya 800,000 kote nchini, na mitaji wezeshi ya takribani Shilingi bilioni 20. Uwezeshaji huu umefanyika kupitia miradi mbalimbali chini ya programu hiyo ikiwamo IMBEJU Ng’ara ambayo ni mahsusi kwa ajili ya wanawake, IMBEJU Buni kwa ajili ya biashara changa za vijana, na IMBEJU Kilimo kwa ajili ya wakulima wadogo.