CRDB Insurance inavyokuza ujumuishi wa huduma za bima kupitia ubunifu wa wanawake
Mkurugenzi Mkuu wa CRDB Insurance, Wilson Mnzava (aliyeketi) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wanawake wa kampuni hiyo wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
Sekta ya bima Tanzania inaendelea kukua kwa kasi, ikichochewa na mageuzi ya kiuchumi, maendeleo ya teknolojia na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kujikinga dhidi ya majanga ya kifedha.
Katika muktadha huu, ujio wa kampuni kama CRDB Insurance unaashiria hatua mpya katika safari ya kuifanya bima kuwa huduma jumuishi, bunifu na inayogusa maisha ya Watanzania wengi zaidi.
Kwa mujibu wa takwimu za sekta, mchango wa bima katika pato la taifa bado ni mdogo. Hii inaonesha kuwa bado kuna fursa kubwa ya ukuaji, hasa kupitia ubunifu katika utoaji wa huduma na bidhaa za bima.
Uwezeshaji wa wanawake na ubunifu kazini
CRDB Insurance imewekeza kwa makusudi katika kuwawezesha wanawake ndani ya taasisi. Kupitia mazingira jumuishi ya kazi, kampuni imekuwa ikihamasisha wanawake kuibua mawazo mapya, kushiriki katika uongozi na kuleta ubunifu unaoboresha huduma kwa wateja.
Kwa sasa, kampuni ina jumla ya wafanyakazi wanawake 17 na inaendelea kujitolea kukuza, kuendeleza na kuwasaidia wanawake katika ngazi zote ili waweze kufikia nafasi mbalimbali za kitaaluma na uongozi. Katika kutekeleza dhamira hiyo, kampuni imewezesha wafanyakazi wanawake kushiriki katika programu mbalimbali za maendeleo ya taaluma na uongozi, zikiwemo:
Programu ya Mafunzo ya Kiufundi katika Bima (General Insurance) iliyofanyika Pune, India, programu ya Maendeleo ya Viongozi Wakuu (Executive Development Program), programu ya ATE Female Future inayolenga kukuza usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi na programu ya Ulezi na Ushauri (He4She Mentoring Program).
Mazingira haya ya kazi yanayounga mkono wanawake yamechochea pia ubunifu na uvumbuzi miongoni mwa wafanyakazi wanawake.
Mfano halisi ni mfanyakazi mmoja kijana wa kike aliyebaini pengo kubwa la uelewa wa bima katika jamii. Akihamasishwa na utamaduni wa taasisi unaoruhusu mawazo mapya, alibuni kampeni ya kipekee ya mitandao ya kijamii inayojulikana kama “Kibango.”
Kupitia ubunifu huu, ujumbe mfupi lakini wenye nguvu kuhusu bima huandikwa kwenye kibango, kisha mfanyakazi hupiga picha akiwa ameshika kibango hicho na picha hiyo kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii ya CRDB Insurance kila Jumamosi. Mbinu hii imefanikisha kuwasilisha elimu ya bima kwa njia rahisi na inayoeleweka kwa watu wengi.
Baadhi ya jumbe zilizowahi kushirikiwa ni pamoja na:
“Unasave picha kwenye cloud lakini biashara yako haina backup.”
“Kufuli siyo bima.”
“Gari ikiungua utalala nyumbani, nyumba ikiungua utalala kwenye gari?”
“Ajali hutokea siku ambayo huna pesa.”
“Biashara yako ina CCTV camera lakini haina bima.”
“Mchango wa harusi ni 200,000 lakini bima ya nyumba ni 177,000 majuto ni mjukuu.”
“Kibango” lilipata umaarufu mkubwa mtandaoni, likivutia ushiriki wa watu wengi kutokana na urahisi wake, ucheshi na ujumbe mzito wa kielimu. Ubunifu huu umevutia hata taasisi nyingine kuiga mbinu hiyo, jambo linaloonesha athari chanya na upekee wake.
Kwa ujumla, mfano huu unaonesha namna mazingira bora ya kazi yanayowawezesha wanawake yanaweza kufungua ubunifu, kuwapa nafasi ya kutoa mawazo yao, na kusaidia taasisi kufikia jamii kwa njia mpya na zenye tija.
Ubunifu kama injini ya mabadiliko
Katika dunia ya leo, ubunifu si chaguo bali ni hitaji. CRDB Insurance imewekeza katika teknolojia na mifumo ya kisasa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za bima kwa wateja mbalimbali.
Kuanzia matumizi ya teknolojia hadi ushirikiano na sekta ya benki (bancassurance), kampuni imeweza kupanua wigo wa huduma zake kwa ufanisi mkubwa. Aidha, kampuni inafanya kazi kwa karibu na mawakala (agents) na madalali wa bima (brokers) ili kusogeza huduma karibu zaidi na wateja na kutoa ushauri wa kitaalamu.
Mchanganyiko huu wa ubunifu na ushirikiano umeiwezesha CRDB Insurance kuimarisha huduma zake na kuchangia ukuaji wa sekta ya bima nchini.
Bidhaa na huduma za CRDB Insurance
CRDB Insurance inatoa huduma mbalimbali zinazolenga kukidhi mahitaji ya watu binafsi, wafanyabiashara na taasisi. Miongoni mwa bidhaa hizo ni;
Bima ya Magari: Bima hii ya hulinda magari dhidi ya uharibifu, wizi na madai ya wahusika wengine, hivyo kumhakikishia mmiliki wa gari usalama wa kifedha na utulivu wa moyo.
Bima ya Moto na Hatari Shirikishi: Bima hii hulinda mali dhidi ya majanga kama moto, radi, milipuko na hatari nyingine zinazofanana, hivyo kulinda uwekezaji na mali dhidi ya majanga yasiyotegemewa.
Bima ya Uhandisi: Hizi ni bima maalum zilizoundwa kwa ajili ya miradi ya ujenzi, hitilafu za mitambo na kusimama kwa shughuli za biashara, zikilenga kupunguza hatari zinazohusiana na shughuli za kihandisi.
Bima ya Usafirishaji Majini: Bima hii hutoa ulinzi kwa mizigo na vyombo vya usafiri wakati wa safari za majini, na kuhakikisha fidia dhidi ya hasara au uharibifu unaoweza kutokea wakati wa usafirishaji.
Bima ya Safari: Hutoa kinga ya kwa watu binafsi na familia wanaosafiri kwenda nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na gharama za matibabu, kufutwa kwa safari na msaada wa dharura, hivyo kutoa amani ya akili wakati wa safari.
Bima ya Dhima: Hulinda dhidi ya wajibu wa kisheria unaotokana na madai ya watu wengine, ikiwa ni pamoja na majeraha ya mwili, uharibifu wa mali na gharama za kisheria.
Bima ya Kilimo: Ni bima maalum kwa wakulima na wafanyabiashara wa sekta ya kilimo, ikijumuisha hasara ya mazao, vifo vya mifugo na hatari nyingine za kilimo, hivyo kusaidia uthabiti wa kifedha katika sekta hiyo.
Huduma hizi zimeundwa kwa mtazamo wa ubunifu ili kukidhi mahitaji ya sekta mbalimbali za uchumi, ikiwa ni pamoja na sekta ya nishati, biashara na kilimo.
Tofauti ya CRDB Insurance na watoa huduma wengine
Kinachoifanya CRDB Insurance kuwa ya kipekee ni; Moja ni muunganiko wa nguvu ya benki na bima katika jukwaa moja. Kupitia mfumo wa benkibima, kampuni inawafikia wateja kwa urahisi zaidi.
Pili ni utambuzi wa Chapa; kutambulika kwa chapa kumeleta urahisi wa ufikiaji wa huduma kupitia mawakala, matawi na madalali pamoja na huduma bora kwa wateja.
Tatu; matumizi ya mifumo ya kidijitali yamerahisisha upatikanaji wa huduma lakini pia CRDB Insurance imejipambanua kwa uwezo wa kulipa madai stahiki kwa wakati, kwa kutumia njia rafiki na za haraka za malipo, jambo linaloongeza imani na kuridhika kwa wateja.
Mwisho; Tangu kuanzishwa kwake kama kampuni kamili ya bima mwaka 2023, imeonyesha ukuaji wa haraka, ikinufaika na uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika benkibima. Kwa kuunganisha teknolojia, ubunifu wa bidhaa na rasilimali watu, CRDB Insurance inaendelea kuwa kinara wa mabadiliko katika sekta ya bima nchini.