Yanga yatinga makundi CAFCL baada ya miaka 25

Muktasari:
- Kiu ya miaka 25 kutoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa klabu ya Yanga imekatika leo baada ya kufuta gundu hilo kwa kuifunga Al Merriekh ya Sudan katika michezo yote mwili na kukata tiketi hiyo.
Dar es Salaam. 'Kila Shabiki wa Yanga utakayemgusa saivi ukiuomba ten anakupa haraka upesi' Hii ni kutokana na furaha waliyo nayo baada ya timu yao kufuta gundu la miaka 25 na bila kutinga hatua ya Makundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika wakiiondosha Al Merrikh ya Sudan kwa mabao 3-0.
Yanga ambayo leo ilikuwa kaytika Uwanja wa Chamazi jijni Dar es Salaam iliibuka na ushindi wa bao 1-0 likifungwa na mshambuliaji Clement Mzize akiandika rekodi ya kuifunga nje ndani Wasudani na kuivusha timu hiyo.
Mzize alifunga moja ya mabao mawili yaliyoizamisha Al Merrikh kwenye Uwanja wa nyumbani wa Kigali Pele, jijini Kigali na leo ametupia tena baada ya wageni kuibana Yanga kwa mjuda mrefu wa mchezo huo.
Ushindi huo umeifanya Yanga kutangulia makundi kati ya timu tatu za Tanzania zilizosalia kwenye michuano ya CAF na sasa inazisikilizia Simba na Singida Big Stars ambazo zinashuka uwanjani kesho kuisaka tiketi hiyo na kuiandika nchi historia kwenye michuano hiyo ya CAF.
Yanga ilikuwa timu ya kwanza ya Tanzania kucheza hatua hiyo mwaka 1998 baada ya michuano hiyo kubadilishwa mfumo na tangu hapo ilikuwa ikisota kutafuta nafasi hiyo, hadi Mzize alipofunga bao pekee kwa kichwa akimalizia friikikii ya beki Joyce Lomalisa.
Licha ya kushinda mechi hiyo ya nyumbani, lakini Yanga jasho liliwatoka kutokana na Al Merrikh iliyoshuka uwanjani wakiibana Yanga kwa kufanya mashambulizi makali ya mara kwa mara.
Yanga ikicheza mechi ya tisa ya mashindano chini ya Kocha kutoka Argentina, Miguel Gamondi iliendeleza rekodi ya kuendelea kutoruhusu bao kwani hadi sasa imefungwa bao moja tu lilitokana na penalti kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya michuano ya CAF walipoifunga Asas ya Djibouti kwa mabao 5-1.
Wawakilishi hao wa Tanzania wameungana na TP Mazembe ya DR Congo, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Jwaneg Galaxy ya Botswana, Al Ahly na Pyramids zote za Misri, Petro Atletico ya Angola zilizotangulia mapema kwenye mechi zao zilizopigwa juzi usiku na jana.
Timu hizo zimejihakikisha kuvuna Dola 700,000 (zaidi ya Sh 1.8 Bilioni) kwa kutinga hatua hiyo ya makundi ambayo droo yake inatarajiwa kufanyika mwezi huu na mechi zake kuanza kupigwa mwishoni mwa Novemba kusaka timu za kutinga robo fainali.
DK 45 ZA KIBABE
Kipindi cha kwanza kilikuwa kigumu kwa Yanga wakishindwa kupenya ukuta wa wageni wao waliokuwa wanatumia mfumo wa 4-2-3-1.
Yanga waliuanza mchezo kwa tempo ya chini wakiwasubiria Merreikh wajiachie ili wawaingize kwenye mtego lakini hatua hiyo haikuweza kuwa rahisi kwani wageni walikuwa imara kwa nidhamu ya mchezo.
Moloko ameshuka
Endapo winga wa Yanga Jesus Moloko angekuwa kwenye kiwango bora angeisaidia vizuri timu yake kupata mabao katika kipindi cha kwanza kutokana kupewa mipira mingi lakini pasi zake za mwisho kupotea.
BAO LILIKUWA NJE
Baada ya kumalizika kwa dakika 45 za kwanza kocha Miguel Gamondi alianza kipindi cha pili na mabadiliko akimtoa mshambuliaji Kennedy Musonda nafasi yake ikichukuliwa na mwenzake Clement Mzize ambaye ndiye aliyekuja kufunga bao la kwanza.
Mzize mara baada ya kuingia alifanikiwa kufunga bao la kwanza dakika ya 47 kwa kichwa akimalizia krosi ya Maxi Nzengeli lakini mwamuzi wa pili msaidizi Urbain Ndong kutoka Gabon kibendera chake kilikuwa juu akidai krosi ya Maxi ilichezwa mpira ukiwa umetoka.
Mzize alikuja kufunga bao la pili lililokubaliwa akifunga kwa njia ile ile kwa kichwa akitumia krosi ya beki wa kushoto Joyce Lomalisa.
YAO HAPITIKI
Kama kuna beki alikuwa mwiba kwa Wageni basi ni Yao Akouasi kila walipojaribu kujenga mashambulizi kupitia eneo lake hakupitika na hakukuwa na krosi yoyote iliyopita kwenye eneo hilo, huku Wasudani wakionekana wakimbana zaidi Stephane Aziz KI ambaye jana ilikuwa ni siku yake kwa ajili ya mechi hiyo.
Yanga iliamua kuipa mechi hiyo kuwa ni Siku ya Aziz KI, lakini mchezaji huyo alibanwa vilivyo na kushindwa kufanya makele licha ya kupata nafasi kadhaa mbele ya lango ya Al Merrikh.
Azizi KI alifanya shambulizi Moja la shuti Kali lililogonga besela na kurudi uwanjani kipindi cha pili likiwa ndio tukio lake Bora mpaka anatolewa nafasi yake ikichukuliwa na Pacome Zouzoua.
MASHUTI MAWILI TU
Merrikh hawakuwa na ubunifu wa kuweza kupenya ngome ya Yanga ambapo katika dakika 90 walifanikiwa kupiga mashuti mawili pekee ambayo nayo halikulenga lango, likipigwa kipindi cha kwanza dakika ya 32 na beki Salaheldin Nemer kipindi cha kwanza na lingine likipigwa na Mussa Alli.
Vikosi vilivyoanza:
YANGA: Diarra, Yao, Lomalisa, Job, Bacca, Aucho, Moloko, Mudathir, Musonda, Aziz KI na Maxi
Al MERRIKH: Almustafa, Nemer, Karshoum, Bakhit, Hamza, Tabanja, Alrashed, Wagdi, Altish, Brayan na Ramadan