Prime
Yanga yatia mguu dili la Feitoto Simba

Muktasari:
- Lakini klabu ambayo amekuwa akihusishwa nayo zaidi ni Simba, huku wengi wakiamini inaweza kutokea kama ilivyotokea kwa John Bocco na wenzake mwaka 2017. Hata hivyo, Kaizer Chiefs nao wanaelezwa kulazimisha dili hilo tangu mwezi Januari ingawa Azam wenyewe wameamua kulitolea nje.
Tangu atambulishwe na Azam FC Juni 8, 2023, baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu, nyota Feisal Salum almaarufu Feitoto, amekuwa akihusishwa na klabu mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Lakini klabu ambayo amekuwa akihusishwa nayo zaidi ni Simba, huku wengi wakiamini inaweza kutokea kama ilivyotokea kwa John Bocco na wenzake mwaka 2017. Hata hivyo, Kaizer Chiefs nao wanaelezwa kulazimisha dili hilo tangu mwezi Januari ingawa Azam wenyewe wameamua kulitolea nje.
Uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini uwezekano wa Azam FC kumuuza Feitoto ni mdogo na pengine haupo kabisa. Yaani ni sawa tu na kusema haiwezekani. Hii ni kwa sababu mkataba wa mauziano baina ya mchezaji huyo, Yanga na Azam FC ni mgumu sana kutekelezeka hasa kwa klabu za Tanzania na hata Afrika.
Ndani ya mkataba huo wa Feitoto kwenda Azam, Yanga waliweka kipengele kinachoitaka Azam FC kuipatia klabu hiyo Sh1 Bilioni endapo itamuuza Feitoto popote pale.
Hiki peke yake ni kiasi kikubwa sana cha pesa ambacho kiuhalisia Simba haiko tayari kukitoa. Lakini hata kama Simba watajitutumua na kutoa kiasi hicho, itakuwa bado haitoshi.
Habari zinasema Azam FC hawawezi kumuuza Feitoto na hela zote kuwapa Yanga halafu wao wabaki mikono mitupu.
Kama wataamua kumuuza basi ni lazima iwe kwa bei ya juu ili na wao wabaki na kitu mkononi...na hicho kitu ni aidha kilingane na watakachopata Yanga au kizidi.
Maana yake ni lazima wamuuze kwa shilingi bilioni mbili au zaidi...nani wa kutoa pesa yote hiyo, sio tu Tanzania, hata nje ya Tanzania?
Utafiti unaonyesha kwamba licha ya ubora wa staa huyo lakini bahati mbaya kwake timu zenye uwezo wa kutoa kiasi hicho huwa haziangalii sana upande huu wa Afrika, wanaangalia kwingine kabisa.
Timu tajiri zikiwemo Mamelodi Sundowns au timu za Kaskazini kama Al Ahly, haziamini kama mchezaji wa kutoka ukanda huu wa Afrika Mashariki, tena kwa timu kama Azam, anastahili kulipiwa fungu lote hilo.
Wapo tayari kutoa kitita kama hicho kwa mchezaji kutoka Ulaya, Asia au Amerika Kusini...lakini si ndani ya Afrika, tena Afrika Mashariki.
Habari zinasema kwamba kama Simba wanamtaka Feitoto, lazima wasubiri hadi mkataba wake utakapoisha, wampate kama mchezaji huru.
Lakini na hilo ni jambo gumu kwani inaelezwa kwamba tayari Azam Fc wameshamuwekea mkataba wenye ofa nono mezani ambao kwa namna yoyote ni ngumu kuukataa.
Feitoto ambaye mkataba wake utaisha Juni 2026, yupo katika hatua za mwisho za kushauriana na kambi yake juu ya kusaini mkataba mpya au kuangalia changamoto nyingine sehemu nyingine.
Na hata kama ataamua kuondoka, labda aende nje ya nchi kwa sababu hakuna klabu ya ndani inayoweza kufikia angalau nusu ya ofa hiyo.
MSIMU HUU
Hadi sasa, Fei Toto ndiye kinara wa asisti akiwa nazo 12 huku akifunga mabao manne. Katika mahojiano yake na Mwanaspoti hivikaribuni ni kwamba anataka zifike 15 akiwa na imani zitaisaidia timu yake kufikia malengo waliyojiwekea kwani wana washambuliaji wanaozitumia vizuri pasi zake za mwisho.
“Nafurahi kuona nimevunja rekodi ya asisti mapema kukiwa na mechi nyingi bado za kucheza, nimempita Kipre Junior aliyeibuka kinara wa asisti msimu uliopita.
“Malengo yangu nataka kuweka rekodi kubwa zaidi kwa kufikisha asisti 15, kwa kuwa bado timu yangu ina mechi nyingi za kumaliza msimu naamini jambo hili litawezekana,” alisema Fei Toto ambaye huu ni msimu wa pili anaichezea Azam.
Wakati Fei Toto akiyasema hayo, kocha wake, Rachid Taoussi alisema: “Feisal ni mchezaji mzuri mwenye kipaji kikubwa na anaweza kucheza nafasi nyingi, ila mimi napendelea kumtumia kama namba 10.
“Namba anayoichezea inamfanya aweze kutumia ubora wake na kutengeneza nafasi, lakini haina maana nimemzuia kufunga, jambo muhimu kwanza ni atengeneze nafasi kwa wenzake na kufunga akiweza.”
TIMU YA TAIFA 2024
Feisal alicheza mechi 18 za timu ya taifa ndani ya mwaka 2024.
Mechi hizi ni kuanzia za mashindano makubwa kama fainali za AFCON kule Ivory Coast na kufuzu Kombe la Dunia 2026 na AFCON 2025.
Ndani ya mwaka huu Feitoto alifunga mabao mawili, dhidi ya Guinea na dhidi ya Ethiopia.
Mabao haya ni mengi zaidi kwake ndani ya mwaka mmoja, kwani tangu aanze kuchezea timu ya taifa amemfunga jumla ya mabao manne tu.
Kocha wa Wydad Casablanca, Rhulani Mokwena, alikiri waziwazi kwamba yeye ni shabiki mkubwa wa mchezaji huyo na anatamani sana kufanya naye kazı siku moja.
Kocha huyo wa zamani wa Mamelodi Sundowns, aliyasema hayo alipokutana na mchezaji huyo nchini Morocco wakati Azam FC ilipokuwa kwenye maandalizi ya msimu mpya.
Kocha wa Kaizer Chiefs, Nasreddine Nabi, amefanya kila kitu kumpata mchezaji huyo huku timu yake ikituma barua mara mbili ya kuomba kufungua maongezi na Azam FC kumhusu mchezaji huyo, lakini Azam FC haikujibu hata moja.