Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yaongeza baridi kileleni Ligi Kuu

YANGA imeendeleza sherehe kwa mashabiki wake baada ya kufanikiwa kuichapa Coastal Union kwa bao 1-0 kwenye mchezo mkali wa Ligi Kuu Bara.

Ikiwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, Yanga ilionyesha kiwango cha chini kipindi cha kwanza cha mchezo huo, lakini iliporejea kipindi cha pili ilionyesha kiwango cha juu na kuichanganya Coastal Union ambayo msimu huu haina makali chini ya nahodha Ibrahim Ajibu.

Mashabiki wa Yanga ambao dakika ya tano ya mchezo walisimama na kuonyesha ishara ya vidole vitano, wanaona kama ni kawaida yao sasa kupata ushindi kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara, wakiwa wamepoteza mchezo mmoja tu kati ya tisa waliyocheza na hawana sare.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alifanya mabadiliko ya wachezaji watatu kwenye kikosi  chake ambacho kiliichapa Simba Jumapili iliyopita kwa mabao 5-1.

Jana langoni alianza Abutwalib Mshery akichukua nafasi ya Djigui Diarra, beki wa pembeni alicheza Dickson Kibange badala ya Joyce Lomarisa na beki wa kati alianza nahodha Bakari Mwamnyeto badala ya Dickson Job.

Mchezo huo ulitawaliwa na rafu za hapa na pale ambapo hadi dakika ya 70 ya mchezo, wachezaji watatu wa Yanga walikuwa wamepewa kadi za njano na wanne upande wa Coastal.

Clement Mzize ambaye aliingia kipindi cha pili ndiye aliyeifungia Yanga bao pekee kwenye mchezo huo katika dakika ya 71, akipata krosi safi kutoka kwa Jesus Moloko ambaye naye aliingia kipindi cha pili cha mchezo huo na kufunga kwa kichwa safi.

Hilo ni bao la kwanza kwa mshambuliaji huyo kinda kwenye Ligi Kuu msimu huu.

“Nimependa jinsi ambavyo wachezaji wangu wamejituma kwenye mchezo huu nafurahi kuona kuwa tumepata pointi tatu kwenye mchezo huu pamoja na ule uliopita dhidi ya Simba,” alisema Gamondi.

Wakati akisema hivyo, Fikirini Elias kocha wa Coastal Union ambaye timu yake imekusanya pointi saba tu kwenye michezo tisa, alisema timu yake ilicheza vizuri kwenye eneo la ulinzi, lakini wanakubali kuwa wamepoteza kutokana na ubora wa wachezaji wa Yanga.

Na sasa ni dhahiri kuwa Yanga watabaki kileleni mwa msimamo hadi Ligi Kuu itakaporejea tena Novemba 22, ikiwa imekusanya pointi 24 tofauti ya pointi tano dhidi ya Azam iliyopo nafasi ya pili, lakini ikiwa ni tofauti ya pointi sita dhidi ya Simba ambayo inacheza na Namungo leo lakini ikiwa na mchezo mmoja mkononi.