Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dabi ya Kariakoo, ukipigwa umeumia

Dar es Salaam. Bado hata nusu ya msimu haijafika lakini timu itakayopoteza mechi kati ya Simba na Yanga leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa  11:00 jioni itajiweka katika hesabu ngumu za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Ubora na muendelezo wa kufanya vizuri katika mechi dhidi ya timu nyingine, unalazimisha kila timu kuhakikisha inapata ushindi leo ili isitoe mwanya kwa mwenzake kumtangulia kileleni mwa msimamo wa ligi jambo litakaloleta ugumu katika kumshusha na kuamua ubingwa hapo baadaye.

Ushindi kwa wageni Yanga, utawafanya wazidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi ambapo watafikisha pointi 21 na hivyo kuondoka katika presha ya kupitwa na Simba ambayo ina faida ya kuwa na mchezo mmoja zaidi yao mkononi huku wakiwa pointi sawa kwa sasa.

Kama Simba itaibuka na ushindi, itakuwa faida kubwa kwao kwani wataitangulia Yanga kwa pointi tatu huku wakibakiwa na mechi moja zaidi mkononi ambayo nayo wakishinda, watakuwa na uhakika wa kuongoza msimamo wa ligi kwa pengo la pointi sita mbele ya watani wao ambao ndio washindani wao wakuu katika mbio za ubingwa.

Matokeo ya sare hapana shaka yataifanya vita ya ubingwa baina yao kuzidi kuwa ya moto ingawa kwa namna fulani yatakuwa na faida kwa Simba.


Usikimbie mechi mapema

Kwa shabiki atakayetazama mechi uwanjani au yule ambaye ataiangalia kupitia luninga, ushauri pekee anaoweza kupatiwa ni kusubiri hadi dakika 90 zimalizike vinginevyo anaweza kusikia matokeo ya kushangaza tofauti na aliyoaacha pindi alipoacha kutazama kutokana na uwezo wa kufunga ambao timu hizo zimeonyesha katika vipindi tofauti vya mechi msimu huu.

Timu hizo kila moja imeonyesha makali ya kufumania nyavu katika muda wake ambapo Yanga wameonekana kuwa mwiba kwa safu za ulinzi za timu pinzani katika kipindi cha pili wakati Simba ni hatari katika kipindi cha kwanza.

Katika mechi sita ilizocheza hadi sasa, Simba imefunga mabao 16 ambapo katika kipindi cha kwanza imefumania nyavu mara 11 ikiwa sawa na asilimia 68.75 huku mengine matano sawa na asilimia 31.25 ikifunga katika dakika 45 za mwisho.

Katika mechi saba ilizocheza hadi sasa, Yanga imefunga mabao 20 ambapo katika dakika 45 za pili imefunga mabao 12 sawa na asilimia 60 huku kipindi cha kwanza ikiwa imefumania nyavu mara nane sawa na asilimia 40.

 Tofauti na watani wao wa jadi, safu ya ulinzi ya Yanga imekuwa na uwiano sawa wa kuruhusu mabao katika kila kipindi ambapo kati ya mabao manne ambayo imeruhusu hadi sasa, mawili yamefungwa katika kila kipindi cha mchezo.


Arajiga safi kotekote

Refa kutoka Manyara, Ahmed Arajiga ndiye aliyepangwa na kamati ya waamuzi ya TFF, kuchezesha mechi hiyo ya watani wa jadi leo.

Historia inaonyesha refa huyo amekuwa na historia tamu na chungu kwa kila timu kwani mechi mbili alizowahi kuzichezesha, kila moja imeonja kipigo mbele ya mwenzake tena ushindi ukiwa ni wa bao 1-0, zote zikiwa ni katika Kombe la Shirikisho la Azam  (ASFC).

Alichezesha mechi ya fainali ya ASFC, Julai 25, 2021 mkoani Kigoma ambayo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililopachikwa na Lwanga Taddeo.

Mwaka uliofuata, Mei 28, Arajiga akiwa ‘pilato’ wa mechi ya nusu fainali ya ASFC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Feisal Salum.

Taarifa iliyotolewa na Ofisa habari wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Karim Boimanda, Arajiga atasaidiwa na Mohammed Mkono na Kassim Mpanga, refa wa akiba akiwa ni Ramadhan Kayoko huku kamishina wa mchezo akiwa ni Hosea Lugano.

Ni mechi yenye hadhi ya kimataifa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya maofisa walioteuliwa kuisimamia wengine wakiwa ni Lisobine Kisongo (daktari), Aaron Nyanda (ofisa masoko), Fatma Abdallah (ofisa protokali), Karim Boimanda (ofisa habari), Hashim Abdallah (ofisa usalama), Iman Mabrouk (mratibu wa mechi), Ramadhan Misiru (mkuu wa kituo) na Hafidh Badru (mratibu msaidizi wa mechi).


Mbabe kusakwa

Mbali na kiu ya kuziongoza timu zao kupata pointi tatu, kila kocha anataka ushindi katika mchezo huo ambao utakuwa na maana kubwa kwa kibarua chake ndani ya timu anayoifundisha.

Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ anasaka ushindi ambao utamfanya azidi kuboresha historia yake ya kutamba dhidi ya Yanga akiwa na Simba na hata kabla hajajiunga na timu hiyo.

Mbrazil huyo amepata ushindi mara zote nne ambazo amekutana na Yanga, tatu akishinda ndani ya dakika 90 huku mara nyingine moja akipata ushindi kwa mikwaju ya penalti baada ya mechi kumalizika kwa sare tasa katika muda wa kawaida wa mchezo.

Kwa kocha wa Yanga, Miguel Gamondi atakuwa anasaka ushindi wa kwanza dhidi ya Simba tangu alipoanza kuinoa timu yake ambapo kabla ya hapo alipoteza kwa mikwaju ya penalti 3-1 katika mashindano ya Ngao ya Jamii yaliyofanyika Tanga, Agosti mwaka huu.


Robertinho, Gamondi heshima juu

Makocha Robertinho wa Simba na Gamondi wa Yanga kila mmoja ameonyesha hamu ya kupata ushindi katika mechi hiyo huku wakionyesha kutoa heshima kwa timu pinzani.

“Wapinzani wangu wana wachezaji wazuri sana eneo la kiungo, nami nataka niwazuie wasicheze kutoka eneo hilo, nitachagua wachezaji sahihi wa kazi hiyo, kesho (leo) watacheza wachezaji wangu bora eneo hilo la kiungo.

“Natokea Brazil nchi ya mpira na nimecheza mpira kwenye kiwango cha juu na najua kuna presha ila mimi napenda presha kama hizi za Dabi. Kabla ya mechi kila shabiki anajua mpira na mbinu pia, ila baada ya matokeo kila mtu hajui kitu na timu inabaki ya kuwa ya kocha,” alisema Robertinho.

Kwa upande wake, Gamondi alisema,” nimewaandaa wachezaji wangu kama naenda kucheza mechi zingine hakuna kitu cha ziada kwenye mchezo wa kesho (leo) kikubwa hii ni mechi na mpira ni mchezo wa makosa kwa hivyo atakayefanya makosa atafungwa.

“Sijawahi kufungwa mchezo wowote dhidi ya Simba. Tulitoka suluhu pale Tanga kwa hivyo sina rekodi yoyote ya kuvunja mbele ya Simba na kitu kikubwa kwangu ni mchezo wa kesho timu kushinda na sio kuweka rekodi zangu binafsi.”