Yanga yamtimua Pedro, Moalin apewa usukani
Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Gonçalves. Picha na Yanga
Muktasari:
- Pedro Goncalves ameiongoza Yanga katika michezo 33 ya mashindano tofauti ambapo imeibuka na ushindi katika mechi 23 imetoka sare saba na imepoteza mechi tatu.
Dar es Salaam. Dakika chache baada ya Yanga kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC, uongozi wa timu hiyo leo Jumatano, Mei 6, 2026 umetangaza kumfuta kazi Kocha Mkuu wa timu hiyo, Pedro Goncalves raia wa Ureno.
Taarifa ya Yanga imeeleza kuwa benchi la ufundi la timu hiyo litakuwa chini ya Abdihamid Moalin hadi mwishoni mwa msimu.
“Uongozi wa Klabu ya Young Africans Sports Club unapenda kuutaarifu umma kuwa umemfuta kazi Kocha Mkuu wa kikosi cha kwanza Pedro Gonçalves.
“Uongozi wa Klabu unamshukuru Kocha Pedro Gonçalves kwa mchango wake alioutoa ndani ya klabu yetu na unamtakia kila la kheri katika majukumu yake yajayo.
“Katika kipindi hiki kikosi chetu kitakuwa chini ya uongozi wa Kocha Abdihamid Moalin pamoja na Kocha Patrick Mabedi hadi mwisho wa msimu,” imesema taarifa ya Yanga.
Ingawa Yanga haijafafanua sababu za kuachana na Goncalves, uamuzi katika masuala ya kiufundi na kiwango kisichoridhisha cha timu hiyo katika baadhi ya mechi msimu huu kinaonekana kuichochea hadi ikafikia kumuonyesha mlango wa kutokea.
Goncalves amekuwa akilaumiwa kwa kufanya mabadiliko ya kikosi ambayo yamekuwa yakionekana kutokuwa na tija kwa timu lakini pia kutocheza vyema katika baadhi ya mechi kunaonekana kumponza.
Mfano katika mechi dhidi ya KMC leo, Kocha huyo alijikuta akizomewa na mashabiki wa timu hiyo baada ya kufanya mabadiliko ya kumtoa Yao Attohoula na kumuingiza Bubah Jammeh katika dakika ya 62 ya mchezo.