Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilio cha mastaa Bara na Kanuni ya usajili

Dar es Salaam. Baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu Bara, wamekuwa hawazifahamu kanuni zinazowahusu moja kwa moja, huku wengi wao wakiomba elimu zaidi kutoka kwa wahusika ili kuwa salama.

Hilo limebainika kufuatia  mahojiano na baadhi ya wachezaji walioonesha kutokuwa na uelewa wa kuwa wanachama wa Chama cha Wachezaji wa Mpira wa Miguu Tanzania (SPATA) ambacho zamani kilitambulika kama SPUTANZA, ambapo kanuni za Ligi Kuu toleo la 2025, imeweka wazi ulazima wa wachezaji kuwa wanachama wa chama hicho.

Kanuni ya 69:2 kuhusu Maombi ya Usajili, inasema: "Mchezaji yeyote wa Ligi Kuu anapaswa kuwa mwanachama wa Chama cha Wachezaji wa Mpira wa Miguu Tanzania (SPUTANZA) kabla ya kukamilisha usajili wake kwenye klabu ya Ligi Kuu." Licha ya hivyo, wengi wao wanapoulizwa kuhusiana na hilo huwaomba viongozi husika kuwapa elimu zaidi hali inayoonesha hawana uelewa na jambo hilo.


WACHEZAJI

Kipa wa Dodoma Jiji, Ally Salim anasema kuna haja viongozi wa chama watembelee kila klabu, ili kuwapa elimu sahihi wachezaji ili wajue waanzie wapi kulipa ada ya uanachama na umuhimu wa wao kuwa sehemu ya SPATA.

"Ili kuondoa kauli ya wachezaji hawajitambui, uongozi wa SPATA una jukumu la kutembelea kila klabu mwanzoni mwa msimu ili kutoa elimu elekezi ya wachezaji kujua wanaanzia wapi, ndiyo maana wengi wakipata changamoto wanakimbilia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nadhani ndiyo wanatoa muongozo wa wapi wachezaji waende ili kupata haki zao," anasema Salim na kuongeza;

"Mfano mzuri katika chama cha magolikipa Tanzania, viongozi wanajitahidi kutuunganisha kwa pamoja kupitia mwenyekiti wetu Juma Kaseja ndiyo maana kipo imara na kila mtu anajua umuhimu wake."

Mshambuliaji wa KMC, Darueshi Saliboko aliye na mabao matatu Ligi Kuu Bara msimu huu, anasema: "Kiukweli nafahamu kama kuna chama hicho, lakini wachezaji wengi hatujui maana ama faida zake, hivyo viongozi waje katika klabu watuelekeze naamini kila kitu kitakwenda sawa."

Aliyekuwa nahodha wa Tanzania Prisons, Benjamin Asukile ambaye sasa ni meneja wa timu hiyo, anasema: "Sikuwahi kuwa mwanachama wakati nacheza, kitu kikubwa nadhani elimu inatakiwa ili wachezaji waelewe kiundani faida zake."

Kiungo mshambuliaji wa Singida Black Stars, Offen Chikola anasema: "Kikubwa tunahitaji elimu, hakuna mchezaji ambaye hatapenda kuwa sehemu ya kitu ambacho kitasaidia maslahi yake."

Beki wa zamani wa Yanga, Abdallah Shaibu 'Ninja' na sasa anacheza Transit Camp ya Ligi ya Championship, anasema: "SPATA ni chama muhimu ila elimu kubwa inahitajika ili mchezaji kuelewa anapaswa kufanya nini."

Kiungo wa kati wa Singida Black Stars, Ahmed Bakari 'Pipino' anasema anatambua uwepo wa chama hicho kwamba kinasimama kutetea haki za wachezaji, ila hajui uwepo wa kanuni inayowahusu moja kwa moja kwamba ni wanachama.

"Viongozi waangalie ni jinsi gani ya kutufikishia elimu, kuna wakati mwingine wachezaji tunafanya makosa bila kujua, kwani mpira wa miguu kwa sasa una sheria nyingi, sasa wakipatikana watu wa kututetea ni jambo la msingi, tunahitaji elimu ili tuelewe kwa kina na hilo litatusaidia kuondokana na migogoro isiyokuwa na faida," anasema Pipino.


MAKOCHA

Kocha wa Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship, Zubery Katwila anasema kuna haja wachezaji wakajua umuhimu wa chama cha SPATA kabla hawajakumbwa na changamoto pia viongozi waweke nguvu kutoa elimu.

"Wakati msimu ukiwa unatakiwa kuanza kila timu inakuwa inapewa fomu za afya zinaitwa medical check up, wafanye vivyo hivyo na viongozi wa SPATA kuleta fomu ili wachezaji wajaze na wajue umuhimu wa hilo, wakati nacheza mimi nilikuwa mwanachama kipindi hicho kilikuwa kinaitwa SPUTANZA na kipindi kile mwenyekiti Mussa Kisoki alikuwa anatembelea kila klabu na amefanya kazi kubwa ya kutatua migogoro ya wachezaji na klabu," anasema Katwila na kuongeza:

"Kwa sasa nimejiunga na Chama cha Waalimu wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) kwa sababu najua umuhimu wake, ndiyo maana nasisitiza hilo kwa wachezaji na elimu iendelee kutolewa hata katika mitandao ya kijamii."

Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally anasema: "Niwaombe viongozi wa SPATA wakipata nafasi wajiunge na sisi kuja kutupa elimu lakini kukiwa na kanuni inayohusu wachezaji moja kwa moja, mara nyingi menejimenti inakaa na wachezaji kuwaelekeza, ila hilo linahitaji msisitizo zaidi wajue faida zake."

Kwa upande wa Kocha wa Dodoma Jiji, Amani Josiah anasema: "Mara nyingi zinapokuja kanuni zinazohusu moja kwa moja wachezaji wanaelekezwa lakini ni muhimu viongozi wa SPATA kutoa elimu ya msisitizo ili wajue umuhimu wake, hilo litasaidia."


KAULI YA SPATA

Mchezaji wa zamani wa Mecco ya Mbeya na Taifa Stars, Abeid Kasabalala ambaye kwa sasa ni mtendaji msaidizi wa Chama cha Wachezaji (SPATA) zamani SPUTANZA, anasema wana kazi ya kutoa elimu kwa wachezaji ili kuelewa umuhimu wa hilo.

"Kanuni hizo ni hai, tunawaomba Wanahabari kuwaelimisha wachezaji kujua umuhimu wa SPATA, wasisubiri hadi wapate changamoto ndipo waanze kututafuta, tunahitaji kuwa na data zao kamili ili tunapotaka kutatua matatizo yao tunakuwa na kila kitu cha kusimama nacho," anasema kiongozi huyo na kuongeza;

"Kila kitu kilichopo katika kanuni ya 69 (2) kipo sawa isipokuwa tumefanya maboresho machache ya kuwaongeza viongozi wa timu na manahodha wa timu za Ligi Kuu na Championship kuhudhuria katika mkutano mkuu wa chama unaofanyika kwa mwezi mara moja na kwa mwaka huu tunatarajia kufanya Desemba.

"Lengo la kuwajumuisha ni kuwapa nafasi ya kuleta changamoto wanazokutana nazo katika majukumu yao na sisi kujua tunaanzia wapi kuyatatua, ndiyo maana ukisoma vipengele vya vitu gani mchezaji anatakiwa kuvifanya utaelewa tunahitaji data zake zote."