Yanga yagoma kuingia vyumbani, yatumia mjengo wa kifahari
Baadhi ya Mabausa wa Yanga wakiwa katika geti la moja ya nyumba ambayo kikosi hicho cha Wananchi kimetumia kujiandaa na mechi ya Watani wa Jadi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo
Dar es Salaam. Katika hali iliyozua gumzo miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka, kikosi cha Yanga kimetumia nyumba ya jirani kubadilishia nguo badala ya vyumba rasmi vya Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Nyumba hiyo iliyotumika ni ya kifahari yenye rangi nyeupe inayong’aa, likiwa limezungukwa na fensi yenye nyaya za umeme juu yake.
Nyumba hiyo ambayo inatazamana na geti kuu la uwanja huo, iligeuka kuwa sehemu ya maandalizi ya timu hiyo.
Awali, Simba walikuwa wa kwanza kuwasili uwanjani, wakionyesha utulivu na maandalizi saa 10:25 jioni.
Dakika 20 baadaye ndipo msafara wa Yanga uliwasili lakini ukaingia katika sintofahamu ya muda mfupi.
Katika hekaheka hiyo kulikuwa na mkanganyiko katika uratibu wa kuingiza timu hiyo uwanjani huku baadhi ya maofisa wa usalama ikiwemo makomandoo wakionekana kufunga njia kwa muda.
Msongamano ulijitokeza kwa muda mfupi katika geti kuu, ndipo Yanga walipoelekea kwenye nyumba nyeupe ya jirani, wakiingia kwa uharaka, wakitumia eneo hilo kama sehemu ya kujipanga kwa mechi hiyo.
Tukio hilo liliwaacha mashabiki na wadau wengi wakishangaa huku wengine wakilitafsiri kama ishara ya timu hiyo ya Wananchi kutokuwa na imani na vyumba vya kubadilishia nguo vya uwanja huo ingawa hakuna hata mmoja aliyekuwa tayari kuongea lolote.
Vikosi vilivyoanza
Simba: Djibrilla Kassali, Shomari Kapombe, Nickson Kibabage, Olivier Toure, Rushine De Reuck, Yusuph Kagoma, Libase Gueye, Neo Maema, Elie Mpanzu, Inno Loemba na Clatous Chama.
Yanga: Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Damaro Camara, Max Nzegeli, Duke Abuya, Prince Dube, Allan Okello na Pacome Zouzoua