Yanga yagawa dozi ugenini, ikikaribia raundi ya pili
Muktasari:
- Yanga iliishia hatua ya makundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita baada ya kuvuna pointi nane katika michezo sita ambapo ilipata ushindi mara mbili, sare mbili na kupoteza michezo miwili.
Dar es Salaam. Yanga imejiweka katika mazingira mazuri ya kutinga raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2026/2026 baada ya leo, Ijumaa, Septemba 19, 2025 kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Wiliete De Benguela ya Angola.
Mabao ya Yanga katika mchezo huo yamefungwa na Aziz Andabwile aliyefumania nyavu katika dakika ya 32 na mengine mawili yamepatikana katika kipindi cha pili yakifungwa na Edmund John katika dakika ya 72 na Prince Dube katika dakika ya 81.
Matokeo hayo yameifanya Yanga ihitaji sare au ushindi wa aina yoyote katika mchezo wa marudiano itakaocheza Dar es Salaam wiki ijayo ili itinge raundi ya pili ya awali ya mashindano hayo lakini hata ikipoteza kwa matokeo ya utofauti wa bao moja au mawili itasonga mbele.
Ni maajabu tu ambayo Wiliete Benguela inayategemea ili isonge mbele kwani inapaswa kupata ushindi wa utofauti wa mabao manne au kupata ushindi wa mabao 3-0 ili ijaribu kupenya kupitia mikwaju ya penalti.
Katika mchezo wa leo, Yanga ilianza na kikosi ambacho kilikuwa na mabadiliko kidogo kufananisha na kile kilichoanza dhidi ya Simba, Jumanne iliyopita.
Beki na nahodha Bakari Mwamnyeto alianza kikosini kuchukua nafasi ya Dickson Job, Mamadou Doumbia alianzishwa akichukua nafasi ya Mudathir Yahya na Clement Mzize alianza badala ya Maxi Nzengeli.
Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Yanga katika mechi za kimashindano msimu huu huku ikiwa haijaruhusu bao ambapo mchezo uliopita iliifunga Simba kwa bao 1-0 katika mechi ya Ngao ya Jamii.
Kikosi cha Yanga kilichoanza leo kiliundwa na Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Aziz Andabwile, Clement Mzize, Duke Abuya, Dube, Doumbia na Pacome Zouzoua.
Ikiwa Yanga itasonga mbele, itakutana na mshindi wa mechi mbili zitakazozikutanisha Elgeco Plus ya Madagascar na Silver Strikers ya Malawi.