Yanga, Simba zanukia fainali Kombe la Muungano
Muktasari:
- Yanga ndio bingwa mtetezi wa Kombe la Muungano ambapo msimu uliopita ilitwaa kwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKU katika mechi ya fainali.
Ratiba ya Kombe la Muungano 2026 litakalofanyika Zanzibar kuanzia Jumanne Aprili 21, 2026 imeweka uwezekano wa Yanga na Simba kukutana katika mechi ya fainali.
Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo iliyotolewa leo, Yanga na Simba haziwezi kukutana katika robo fainali wala nusu fainali lakini zinaweza kukutana katika hatua ya mwisho ya mashindano hayo.
Katika robo fainali, Yanga ambayo ni bingwa mtetezi, itakutana na Muembe Makumbi huku Simba ikipangwa kukutana na Mafunzo.
Azam FC itakutana na KVZ na Singida Black Stars itacheza na Mlandege.
Mshindi wa mechi baina ya Yanga na Muembe Makumbi atakutana na Azam au KVZ katika nusu fainali na nusu fainali nyingine itakuwa baina ya mshindi wa Simba dhidi ya Mafunzo na Mlandege dhidi ya Singida Black Stars.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Ahmada Hussein Vuai, amesema kuwa maandalizi yote ya mashindano hayo yamekamilika, na hivyo kuweka mazingira ya mwanzo wa kusisimua.
Vuai amesema kuwa bingwa wa mashindano hayo mwaka huu atapata kitita cha Sh150 milioni.
Kiwango hicho cha zawadi ni mara tatu ya fedha ambazo ilipewa bingwa wa mashindano yaliyopita.
Katika mashindano ya mwaka jana, Yanga ambayo ilitwaa ubingwa huo, ilizawadiwa Sh50 milioni.