Simba yaiongezea ugumu Fountain Gate Ligi Kuu
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Libasse Gueye akishangilia baada ya kufunga bao dhidi ya Fountain Gate.
Muktasari:
- Katika mechi 10 za hivi karibuni za Ligi Kuu, Fountain Gate imepata ushindi mara moja, sare tatu na imepoteza mechi sita.
Dar es Salaam. Simba imezidi kuiweka Fountain Gate kikaangoni katika Ligi Kuu ya NBC baada ya leo Jumatano, Aprili 15, 2026 kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi yao katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.
Matokeo hayo yameifanya Fountain Gate iendelee kubakia katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi na pointi zake 16 ilizokusanya katika michezo 18.
Mabao ya Simba katika mchezo huo yamefungwa na Clatous Chama, Libasse Gueye na moja la kujifunga la Shaban Mgunda.
Bao la Chama katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza ni la kwanza kwa kiungo huyo mshambuliaji ndani ya jezi ya Simba tangu alipojiunga nayo katika dirisha dogo la usajili Januari mwaka huu.
Kwa upande wa Gueye, bao lake ambalo alipachika katika dakika ya 53 likiwa la pili kwa Simba katika mechi ya leo, limekuwa la kwanza kwa winga huyo kutoka Senegal baada ya kucheza mechi tisa mfululizo bila kufumania nyavu tangu alipofanya hivyo katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya KMC, Februari 11, 2026.
Bao lingine la Simba katika mchezo wa leo lilikuwa la kujifunga la Shaban Mgunda wa Fountain Gate katika dakika ya 71 alipokuwa katika harakati za kuokoa shuti la Elie Mpanzu.
Ushindi wa leo umeifanya Simba izidi kujichimbia katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 39.
Ligi Kuu ya NBC itaendelea tena kesho kwa uwepo wa mechi mbili zitakazochezwa katika viwanja na miji tofauti nchini.
Katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, Mashujaa FC itakabiliana na Singida Black Stars kuanzia saa 10:00 jioni.
Yanga itaialika Mbeya City katika Uwanja wa KMC Complex kuanzia saa 12:30 jioni.