Yanga, Simba zafuzu Ligi ya Mabingwa, ubingwa bado
Muktasari:
- Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na pointi 69 huku Simba ikifuata na pointi zake 67.
Dar es Salaam. Yanga na Simba zimekata rasmi tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao baada ya kila moja kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mechi zilizocheza dhidi ya timu za Azam na Mtibwa Sugar kwenye viwanja tofauti leo.
Yanga ambayo imeibuka na ushindi dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar, imefikisha pointi 69 na Simba ambayo imeichapa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, imefikisha pointi 67, pointi ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine 16 kwenye Ligi msimu huu.
Hata hivyo, Azam na Singida Black Stars nazo zimejihakikishia kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
Mabao ya Yanga leo yamefungwa na Ibrahim Abdullah ‘Bacca’, Pacome Zouzoua na Laurindo Dilson ‘Depu’.
Simba kwa upande wake imepata mabao yake kupitia kwa Rushine De Reuck, Selemani Mwalimu na Anicet Oura.
Katika Uwanja wa Airtel Singida, wenyeji Singida Black Stars wameibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Tanzania Prisons.
Pamba Jiji FC imesulubiwa na Mbeya City nyumbani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba ikichapwa mabao 2-0.
Matokeo hayo yameifanya Tanzania Prisons ishuke hadi nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi huku Mbeya City ikipanda hadi nafasi ya 13.
Mtibwa Sugar imeshuka kwa nafasi moja hadi nafasi ya 14.
Matokeo ya mechi za leo
Yanga 3-0 Azam
Mtibwa 0-3 Simba
Singida BS 3-1 Tanzania Prisons
Pamba Jiji 0-2 Mbeya City
TRA United 1-1 Coastal
Dodoma Jiji 0-0 JKT Tanzania
Fountain Gate 0-1 Mashujaa
KMC 2-3 Namungo