Pointi tatu za dhahabu, Yanga, Azam kitaumana
Muktasari:
- Mchezo unaosubiriwa kwa hamu ni ule utakaochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar baina ya wenyeji Yanga na Azam FC.
Dar/mikoani. Siku sita za presha katika Ligi Kuu ya NBC zinaanza leo kwa mechi nane ambazo zitakazochezwa katika viwanja tofauti nchini, zikitegemewa kuanza kutoa muelekeo wa mbio za ubingwa, vita ya kushiriki mashindano ya kimataifa na vita ya kuepuka kushuka daraja.
Mechi hizo zote nane za leo, zitaanza katika muda mmoja ambapo zitachezwa kuanzia saa 10:00 jioni na hili litafanyika pia katika raundi ya 29 na ile ya mwisho ya ligi.
Mchezo unaosubiriwa kwa hamu ni ule utakaochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar baina ya wenyeji Yanga na Azam FC.
Timu hizo zinakutana baada ya siku tatu tu tangu zilipokutana katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB ambao Azam iliibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Pamoja na hamu ya kulipiza kisasi, kuvuna pointi tatu leo kutaiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa ligi kwani itafikisha pointi 69 na kuendelea kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Ukiondoa kuendeleza ubabe kwa Yanga, Azam FC inahitajika kupata ushindi katika mechi ya leo ili iendelee kuweka hai matumaini yake ya kutwaa ubingwa na kupata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kwani ushinndi wa leo utaifanya ifikishe pointi 61.
Mchezo mwingine utakuwa katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro leo baina ya wenyeji Mtibwa Sugar dhidi ya Simba.
Ili iendelee kuweka hai matumaini yake ya kutwaa ubingwa, Simba iliyo katika nafasi ya pili na pointi 64, inapaswa kupata ushindi leo na kinyume na hapo, itaisafishia njia Yanga.
Pia Simba ikipata ushindi leo, itahitaji pointi moja tu katika mechi mbili zilizosalia ili ifuzu Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Mtibwa iliyo katika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 27, inaweza kujikuta ikiangukia katika nafasi ya pili kutoka mkiani iwapo itapoteza huku Tanzania Prisons na Mbeya City zikishinda mechi zao.
Katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Pamba Jiji itaikaribisha Mbeya City wakati Singida Black Stars ikiwa mwenyeji wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Airtel Singida.
Kwa Mbeya City, kupoteza mechi ya leo kutazidi kuiweka katika mazingira magumu ya kubaki Ligi Kuu kwani itaendelea kushika nafasi ya 15 ambayo ipo hivi sasa ikiwa na pointi 25 huku Pamba ikihitaji angalau sare ili inusurike rasmi kushuka daraja.
Singidas Black Stars inahitaji pointi tatu za mchezo wa leo ili ijihakikishie rasmi kucheza Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao wakati ushindi kwa Tanzania Prisons ni lazima leo ili iweke hai ndoto ya kusalia Ligi Kuu.
Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, TRA United itaikaribisha Coastal Union na kwenye Uwanja wa Black Rhino, Karatu mkoani humo, wenyeji Fountain Gate watacheza na Mashujaa FC.
Katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, wenyeji Dodoma Jiji FC wataikaribisha JKT Tanzania na katika Uwanja wa KMC Complex, kutakuwa na mechi baina ya KMC na Namungo FC.