Yanga: Nabi aondoke? Mnaumwa nyie!

Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi.

Muktasari:

Yanga ipo kileleni mwa Kundi D katika Kombe la Shirikisho ikifuatiwa na Monastir ya Tunisia, Real Bamako ya Mali na TP Mazembe ya DR Congo ikishikilia mkia.

Dar es Salaam. Timu ya Yanga juzi usiku ilikuwa uwanjani ikisaka heshima yake ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini nyuma mabosi wao wakafunga mjadala wa hatma ya kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi wakisema jamaa bado yupo sana klabuni.

Timu hiyo iliyopo Kundi D sambamba na Monastir ya Tunisia, Real Bamako ya Mali na TP Mazembe ya DR Congo na akizungumza na Mwanaspoti,  Makamu wa Rais wa Yanga Arafata Haji amefunga mjadala akisema wanajua thamani ya makocha wote walionao na sio Nabi pekee.

Arafat alisema, tayari Nabi anafahamu kuwa mkataba wa kusalia Yanga zaidi uko mezani kwake ni suala la kuamua tu lini asaini kwa kuwa uongozi wao tayari ulishampa uamuzi wao wa kutaka kumbakiza zaidi.

Alisema bado wana malengo makubwa katika kuunda timu bora na kwamba kitu pekee ambacho kinawatofautisha na wapinzani wao wengi ni kuwa na benchi la ufundi pana lenye wataalam bora.

"Nabi kuondoka linawezekana lakini haiwezi kuwa sasa, nadhani hata yeye anaamini yuko katika klabu ambayo hatua chache zijazo anaweza kuwa katika rekodi kubwa zaidi ya mafanikio," alisema Arafat na kuongeza;

"Bado tunamhitaji sana Nabi niwahakikishie mashabiki wetu kwamba kocha wao huyu na mwingine haitakuwa rahisi kwetu kuwaachia, tuna malengo makubwa na hii ni safari tu ya kufika huko. Tunafahamu hizi taarifa za sisi kuwa na kocha bora kama Nabi wengine ni ndoto zao, Yanga tuko katika mafanikio haya kutokana na kutumia nguvu kuwaweka wataalam wote bora kama hawa, utulivu wa namna hii klabu zingine hazina ndio maana wanayumba kila wakati."