Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga ilivyoboresha rekodi ya 2021 ya kutopoteza mechi

Muktasari:

  • Yanga itakutana na Polisi Tanzania, Mbeya City na itamaliza msimu kwa kuvaana na Mtibwa Sugar jijini Dar es Salaam Juni 29.

Ikiwa imesaliwa na mechi tatu tu kuhitimisha msimu, kuna kila uwezekano wa Yanga kuboresha rekodi yao ya langoni ya mwaka jana na nia yao ni dhahiri; wanataka wasipoteze mechi hata moja.

Na isitoshe hawajapoteza mchezo hadi wanatwaa ubingwa na sasa wanataka kumalizia msimu bila ya kuonja kipigo, kitu ambacho Simba walitibuliwa na Kagera Sugar katika mechi ya mwisho mbele ya Rais John Magufuli.

Yanga wamebakiza mechi tatu kutimiza hilo.Baada ya kucheza mechi 25, Yanga haijaruhusu kipigo hata kimoja, baada ya kushinda mechi 20 na kutoka sare mechi saba.

Ikishinda mechi zote tatu zilizosalia itakuwa imeboresha rekodi yake kwa kupata ushindi mara mbili zaidi ya mwaka jana iliposhinda mechi 21 tu.

Na ikiwa haitapata sare nyingine na kubakiwa na sare saba tu, itakuwa imeboresha rekodi yake kwa mechi mbili zaidi baada ya mwaka jana kutoka sare mechi 11.

Lakini rekodi iliyo bora zaidi ni ile ya kupoteza mchezo. Mwaka jana, Yanga ndiyo timu iliyopoteza mechi chache kulinganisha na timu nyingine 17 kwenye Ligi Kuu, wakiwemo waliokuwa mabingwa wa msimu huo, Simba.

Moja ya mechi hizo tatu za Simba ni pale walipokubali kipigo cha bao 1-0 mbele ya Yanga, bao lililofungwa kwa mkwaju wa mbali na Zawadi Mauya baada ya mechi iliyopangwa awali kutofanyika kutokana na mkanganyiko wa muda.

Msimu huo, Yanga ilitumia makipa wawili tofauti, Metacha Mnata na Faroukh Shikalo huku Ramadhan Kabwili akigusa mechi chache. Ngome haijabadilika sana, ikiongozwa na Bakari Mwamnyeto na Dickson Job katikati.

Lakini Djigui Diara na Abdallah Msheri wamejitahidi kumaliza mechi nyingi bila ya kuchafua gazeti kiasi cha wote wawili kuruhusu mabao saba tu, huku Diara akiwa na clean sheets 15 na Msheri 10.

Yanga walipoteza mechi mbili tu, walipofungwa mabao 2-1 na Coastal Union jijini Tanga na pia kulazwa bao 1-0 na Azam jijini Dar es Salaam.

Simba walipoteza mechi tatu lakini wakanufaika kwa pointi walizopata katika mechi nyingi walizoshinda. Katika mechi 34 za msimu uliopita, Simba ilishinda mechi 26 na kutoka sare mechi tatu tu, ikiwemo ya duru la kwanza dhidi ya Yanga iliyoisha kwa sare ya bila kufungana.

Timu nyingine iliyopoteza mechi chache ilikuwa Azam FC ambayo ilipata vichapo vinne tu, wakati timu zilizosalia zilipoteza mechi kuanzia tisa na kuendelea.

"Ligi bado ni ngumu na Yanga inahitaji kuendeleza wimbi la ushindi katika mechi zinazokuja," alisema kocha Nasredine Nabi mwezi Januari kabla ya kuvaana na Coastal Union katika mechi ya raundi ya 12 ya Ligi Kuu ya soka msimu huu.

“Tunahitaji kukunjua misuli ili kuboresha matokeo yetu kwenye ligi. Kila mechi ni ngumu na tunahitaji kushinda, kushinda na kushinda ili tutwae ubingwa."

Na ndivyo timu yake iliyofanya hadi sasa baada ya kushinda mechi 20 na kuurejesha ubingwa Jangwani. Lakini katika sare saba zinazotia doa rekodi yao msimu huu, zimo sare tatu mfululizo ambazo zilionekana kama zingewatibulia nia yao ya kurejesha ubingwa Jangwani msimu huu.

Wimbi hilo la sare lilihusisha mechi dhidi ya Prisons, Ruvu Shooting na Simba, mechi zilizoisha bila ya nyavu kutikiswa, lakini vigogo hao wenye makao yao makuu katika makutano ya Mtwaa wa Twiga na Jangwani walizinduka katika mechi dhidi ya Namungo waliposhinda kwa mabao 2-1, Fiston Mayele na Feisal Salum wakitikisa nyavu.

Pia mabingwa hao wapya wa Bara walilazimishwa sare na Simba katika mchezo wa kwanza, na sare nyingine zilikuwa dhidi ya Biashara United, Namungo na Mbeya City.

Pamoja na kuboresha sehemu nyingi, bado upande wa ufungaji haujakuwa bora zaidi licha ya mshambuliaji Mcongo, Fiston Mayele kuibuka kuwa tishio kwa timu pinzani kiasi cha kuonekana kusukiwa mikakati mingi ya kumdhibiti.

Msimu huu, hadi sasa Yanga imefunga mabao 45 na kuruhusu saba tu, hali inayoifanya iwe na tofauti ya mabao 38. Msimu uliopita ilifunga mabao 52 na kuruhusu 21. Hata hivyo mabao hayo ni katika mechi zote 34, wakati msimu huu imeshacheza mechi 25 tu.

Yanga itakutana na Polisi Tanzania, Mbeya City na itamaliza msimu kwa kuvaana na Mtibwa Sugar jijini Dar es Salaam Juni 29.