Yaliyojiri mzunguko wa kwanza Ligi Kuu Bara

Kati ya timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu 2024-2025, ni sita pekee ambazo hazijamaliza mechi zao za mzunguko wa kwanza, zilizobaki kila moja imeshuka dimbani mara tano.
Simba ambayo kwa sasa inaongoza ligi hiyo ikifikisha pointi 34, imecheza mechi 13, bado mbili sawa na Yanga iliyocheza jana Jumapili dhidi ya Tanzania Prisons.
Zingine zenye mechi mojamoja kukamilisha mzunguko wa kwanza ni Singida Black Stars itakayocheza dhidi ya Simba kama ilivyo kwa JKT Tanzania, huku Fountain Gate na Dodoma Jiji zenyewe zitakabiliana na Yanga.
Cha kushutua zaidi ni kwamba, tumeshuhudia mabadiliko ya makocha 12 katika mzunguko wa kwanza hadi sasa huku timu nne pekee zikibaki na makocha walioanza nao msimu ambazo ni Simba (Fadlu Davids), Dodoma Jiji (Mecky Maxime), JKT Tanzania (Ahmad Ally) na Mashujaa (Mohamed Abdallah 'Bares') ambaye huyu ana rekodi yake ya kuwa kocha pekee tangu kuanza kwa msimu uliopita 2023-2024 hadi sasa 2024-2025 ndiye amebaki kwenye nafasi yake, timu zingine zote zikibadilisha katika kipindi hicho.
Wakati mzunguko wa kwanza ukiwa umekamilika kwa timu nyingi, kuna mambo mengi yamejiri ambapo Mwananchi linakuchambulia baadhi huku mengine yakilinganishwa na ilivyokuwa msimu uliopita 2023-2024 kipindi kama hiki.
Ikumbukwe kwamba, Mtibwa Sugar na Geita Gold zilikuwepo na kushuka daraja, Pamba Jiji na KenGold zikichukua nafasi zao. Kwa sasa Mtibwa Sugar na Geita Gold zipo Championship, ligi ambayo Pamba Jiji na KenGold zilikuwa huko msimu uliopita.
Ifahamike kuwa, Singida Fountain Gate iliyokuwa ikitambulika kwa jina hilo msimu uliopita hivi sasa inaitwa Fountain Gate wakati Ihefu inaitwa Singida Black Stars.
POINTI NYINGI
Simba ndiyo timu iliyokusanya pointi nyingi hadi sasa ikiwa nazo 34 baada ya kucheza mechi 13, endapo ikishinda mechi mbili zilizobaki dhidi ya Singida Black Stars na JKT Tanzania, ni wazi itamaliza mzunguko wa kwanza kwa kufikisha pointi 40 ambazo msimu uliopita Yanga ilimaliza nazo kipindi kama hiki.
Hadi sasa Simba ndiyo timu iliyoshinda mechi nyingi ambazo ni 11 sawa na Yanga.
Msimu uliopita katika mzunguko wa kwanza, Simba ilimaliza ikishinda mechi 11 sawa na Azam, wakati Yanga ikishinda 13. Timu iliyoshinda mechi chache zaidi msimu huo ni Mashujaa na Mtibwa Sugar kila moja ikionja ushindi mara mbili.
KICHAPO KIKUBWA
Juzi tulishuhudia Simba ikiichapa Kagera Sugar mabao 5-2 kikiwa ni kipigo kikubwa kwa msimu huu mzunguko wa kwanza, wakati msimu uliopita tulishuhudia mzunguko huo Yanga ikishinda 5-0 mara mbili dhidi ya JKT Tanzania na KMC, kisha 5-1 dhidi ya Simba. Azam nayo ilishinda 5-0 dhidi ya KMC na Mtibwa Sugar.
MABAO MENGI
Timu yenye mabao mengi msimu huu hadi sasa ni Simba ikifunga 28 huku pia ikiruhusu machache zaidi ambayo ni matatu. Iliyoruhusu mabao mengi ni KenGold (27). Msimu uliopita wakati kama huu Azam ndiyo ilikuwa imefunga mabao mengi (38) wakati Yanga ikiruhusu machache zaidi (6). Iliyoruhusu mengi ni Mtibwa Sugar (32).
Pia mzunguko wa kwanza msimu uliopita yalifungwa mabao 269 wakati msimu huu yakifungwa mabao 235 yakiwa pungufu ya mabao 34.
HAT TRICK
Tumeshuhudia hat trick moja pekee msimu huu hadi sasa ikifungwa na Prince Dube aliyefanya hivyo wakati Yanga ikishinda 3-2 dhidi ya Mashujaa, Alhamisi iliyopita ikiwa ni mechi yao ya 12. Kabla ya hapo, zimecheza mechi zaidi ya 100 hakukuwa na hat trick na ilionekana tunaweza kumaliza mzunguko wa kwanza kwa timu zote bila ya kushuhudia hilo likitokea, lakini Dube akavunja mwiko huo.
Msimu uliopita kulikuwa na hat trick tatu mzunguko wa kwanza ikiwemo ya mapema iliyofungwa na Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam katika mchezo wa kwanza dhidi ya Tabora United wakati Azam ikishinda 4-0. Akafuatia Jean Baleke aliyekuwa Simba, kisha Stephane Aziz Ki wa Yanga akafunga nyingine dhidi ya Azam kabla ya Kipre Junior wa Azam naye kufunga dhidi ya Mtibwa Sugar.
CLEAN SHEET
Moussa Camara wa Simba anaongoza kwa kuwa na clean sheet nyingi ambazo ni 10 katika mechi 13 alizocheza, anafukuzia rekodi ya Ley Matampi aliyekuwa Coastal Union ambaye msimu uliopita hadi unamalizika alikuwa nazo 15, bado tano kumfikia. Camara anafuatiwa na Patrick Munthary wa Mashujaa mwenye nane, wakati Djigui Diarra (Yanga) na Metacha Mnata (Singida Black Stars) kila mmoja anazo saba.
WALIOJIFUNGA
Katika mabao 235, sita yametokana na wachezaji kujifunga huku Azam na Dodoma Jiji zikiongoza kwa kujifunga mabao mawili kila mmoja. Azam waliojifunga ni Yannick Bangala na Mohamed Mustafa, wakati Dodoma Jiji ni Daniel Mgore (Dodoma Jiji) na Dickson Mhilu (Dodoma Jiji). Wengine ni Fredy Tangalo (KMC) na Kelvin Kijili (Simba).
PENALTI 36
Tayari zimepigwa penalti 36, kati ya hizo ni nne pekee hazikufungwa, huku Simba, Tabora United na Namungo zikiongoza kwa kupata penalti nyingi ambazo ni tano kila mmoja. Simba imefunga zote kupitia Jean Charles Ahoua (2) na Leonel Ateba (3), Tabora United imekosa moja ikifunga nne wakati Namungo ikikosa mbili na kufunga tatu. KenGold ndiyo timu iliyopigiwa penalti nyingi ambazo ni sita na zote zimejaa nyavuni, yenyewe ikipata moja na kufunga.
MSIMAMO 2024-2025 MZUNGUKO WA KWANZA
P W D L F A PTS
1.Simba 13 11 1 1 28 3 34
2.Yanga 13 11 0 2 23 6 33
3.Azam 15 10 3 2 22 7 33
4.Singida BS 14 9 3 2 20 9 30
5.Tabora Utd 15 7 4 4 19 19 25
6.Fountain Gate 14 6 2 6 23 25 20
7.Mashujaa 15 4 7 4 13 11 19
8.JKT Tanzania 14 4 7 3 9 8 19
9.KMC 15 5 3 7 10 20 18
10.Coastal Union15 4 5 6 15 16 17
11.Dodoma Jiji 14 4 4 6 13 16 16
12.Namungo 15 4 2 9 9 18 14
13.Pamba Jiji 14 2 6 6 7 14 12
14.Kagera Sugar 15 2 5 8 10 19 11
15.TZ Prisons 15 2 5 8 6 17 11
16.KenGold 15 1 3 11 10 27 6
ILIVYOKUWA 2023-2024 MZUNGUKO WA KWANZA
P W D L F A Pts
1.Yanga 15 13 1 1 36 6 40
2.Simba 15 11 3 1 31 14 36
3.Azam 15 11 2 2 38 12 35
4.KMC 15 5 7 3 15 16 22
5.Singida FG 15 5 5 5 17 17 20
6.Coastal Union 15 5 5 5 11 11 20
7.Dodoma Jiji 15 5 4 6 13 13 19
8.Namungo 15 4 6 5 13 12 18
9.TZ Prisons 15 4 5 6 14 18 17
10.Kagera Sugar 15 4 5 6 9 16 17
11.Ihefu 15 4 4 7 13 19 16
12.JKT Tanzania 15 4 4 7 12 19 16
13.Geita Gold 15 4 4 7 10 17 16
14.Tabora Utd 15 3 7 5 10 17 16
15.Mashujaa 15 2 4 9 11 21 10
16.Mtibwa Sugar 15 2 2 11 16 32 8