Dube aiongoza Yanga kuichakaza Tanzania Prisons

Muktasari:
- Yanga inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 33 sawa na Azam iliyopo nafasi ya tatu huku kinara ikiwa ni Simba yenye pointi 34.
Dar es Salaam. Prince Dube ameendelea kuwa mwiba kwa mabeki wa timu pinzani baada ya leo kuiongoza Yanga kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Nyota huyo kutoka Zimbabwe, jana alifunga bao moja na kupika lingine kwa Clement Mzize akihusika na mabao sita ya timu hiyo katika mechi tatu mfululizo baada ya kufanya hivyo dhidi ya TP Mazembe, kisha dhidi ya Mashujaa na leo, akifikisha mabao sita ambapo amefunga matano na kupiga pasi moja ya mwisho.
Yanga ilikuwa ya moto kuanzia mwanzo tu wa mchezo ambapo ilimaliza dakika 45 za kwanza ikiwa mbele kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Clement Mzize dakika ya 12 akimalizia pasi ya mwisho ya Dube kisha beki Ibrahim Abdulah 'Bacca' akishindilia bao la pili dakika ya 41 kwa mguu akimalizia mpira uliogonga besela kufuatia pigo la adhabu ndogo la Stephanie Aziz KI.
Wakati Prisons wakiendelea kujiuliza, walijikuta wanaruhusu bao la tatu kupitia mshambuliaji Dube aliyewekewa pasi safi na Aziz KI.
Sio kipindi cha kwanza wala Cha pili Prisons ilionekana kushindwa kuhimili presha ya Yanga ambao muda wote iliwalazimisha wageni kupoteza mpira kwa soka lao la kukaba kwa kasi.
Kipindi cha pili Bacca akafunga bao la nne dakika ya 83 ambalo lilionekana akifunga kwa mkono akimalizia shambulizi la kona lakini mwamuzi Abdallah Mwinyimkuu kutoka Singida hakuweza kuona kwa usahihi.
Bao hilo linakuwa la nne kwa Bacca msimu huu akiendelea kuwa beki aliyefunga mabao mengi kwenye timu yake na hata Ligi Kuu.
Ushindi huo umeifanya Yanga isogee hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikifikisha pointi 33.
Simba inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 34 na Azam FC yenye pointi 33 inashika nafasi ya tatu.