Dube awaamsha mastaa Yanga

Muktasari:
- Juzi kwa mara ya kwanza Dube alifanikiwa kufunga mabao yake kwenye Ligi Kuu Bara tangu alipojiunga na Yanga akitokea Azam, hata hivyo aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga hat trick msimu huu wa 2024/2025.
Mshambuliaji Prince Dube ameshaliamsha balaa baada ya kutupia kwa kasi tena akianza na hat trick kwenye ligi hatua hiyo imekuwa faraja pia kwa mastaa wenzake ndani ya kikosi hicho wakisema jamaa atafunga sana.
Juzi kwa mara ya kwanza Dube alifanikiwa kufunga mabao yake kwenye Ligi Kuu Bara tangu alipojiunga na Yanga akitokea Azam, hata hivyo aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga hat trick msimu huu wa 2024/2025.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, nahodha msaidizi wa Yanga beki Dickson Job ameliambia Mwananchi kwamba kila mmoja ndani ya kikosi hicho alikuwa anasubiria nyakati kama hizi kuona Dube anaonyesha makali yake kwa kufunga mabao.
Job alisema Dube ni mshambuliaji mwenye uwezo na akili kubwa ambapo wakati wote akiwa kwenye ukame wa kufunga walikuwa wanampa moyo kwamba mabao yatakuja na kwamba aendelee kujituma kama ambavyo anafanya mazoezini.
"Hakuna asiyejua makali ya Dube ndio maana yupo klabu hii kubwa kwani ana akili kubwa sana ya mpira na kipaji kikubwa, lakini katika soka inatokea kuna wakati washambuliaji wanakutana na wakati mgumu kama hiki alichokutana nacho," alisema Job na kuongeza;
"Unajua sio kwamba alikuwa hafungi kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa tulimuona anafunga ilikuwa imebaki kufunga katika ligi tu, tukiwa mazoezini pia alikuwa anafunga vizuri ila kwenye mechi mnamuona anapata shida.
Tulichokuwa tunafanya ni kumtia moyo kwamba aendelee kupambana na sio yeye tu hata wengine huwa tunawapa moyo kwa kuwa tunajua wana uwezo, kwenye timu tunashirikiana kwa kuwa sisi wote tunapigania lengo moja sasa naona mabao yamerudi ni hatua kubwa kwake na timu yetu kwa ujumla."
Wakati Job akisema hayo kiungo wa timu hiyo, Pacome Zouzoua alisema anaamini mabao ambayo Dube ameyafunga juzi dhidi ya Mashujaa yatamrudishia hali ya kujiamini na kufunga mabao mengi zaidi.
Pacome alisema kasi ya Dube katika timu yao ina umuhimu mkubwa ambapo inawarahisishia wao kama viungo kutoa pasi kwa wakati muafaka.
"Ukiangalia bao ambalo nilimtengenezea alikimbia kwa wakati sana na akajiweka sehemu ambayo mabeki hawakushtuka kasi yake ni kitu bora sana, tuna washambuliaji wenye kasi sana hata Mzize (Clement) Musonda (Kennedy).
"Nadhani sasa atakuwa anaendelea kufunga mabao zaidi kwa kuwa ile hali ya kujiamini itakuwa imerejea kwa nguvu ni mshambuliaji mwenye juhudi na anajua kufunga."