Balama aitabiria Yanga makubwa CAF

Muktasari:
- Mwananchi ilipata fursa ya kuzungumza na kiungo huyo ambaye alizungumzia mwenendo wa waajiri wake hao wa zamani huku akithibitisha kuwepo kwa mabadiliko ndani ya klabu hiyo.
Nyota wa zamani wa Yanga Balama Mapinduzi ‘Kipenseli’ ameelezea hisia zake kuhusu mwenendo wa Yanga msimu huu baada ya mechi ya Ligi Kuu ya jana kumalizika Yanga ikiifunga Mashujaa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Mwananchi ilipata fursa ya kuzungumza na kiungo huyo ambaye alizungumzia mwenendo wa waajiri wake hao wa zamani huku akithibitisha kuwepo kwa mabadiliko ndani ya klabu hiyo.
“Ni kweli Yanga imebadilika inacheza vizuri tofauti na msimu ule niliokuwepo mimi, kiukweli nmejisikia faraja kucheza na moja kati ya timu zangu za zamani na pia namshukuru Mungu kwani nilicheza vizuri licha ya kuwa nje kwa kipindi kirefu kutokana na majeraha,” alisema Balama anayeichezea Mashujaa.
Kuhusu mwenendo wa Yanga katika michuano ya kimataifa nyota huyu alisema bado Yanga ina nafasi ya kufanya vizuri kwenye michezo inayofuata.
“Kwenye mechi za kimataifa bado Yanga ina nafasi ya kufanya vizuri kwenye makundi kwani wametoka kupata sare ugenini na TP Mazembe ambapo walionyesha kiwango kizuri na wanaendelea kuwa bora, na nina imani watashinda mechi zao zilizobaki.”
Kipenseli hakuishia hapo, alielezea matukio mawili ambayo hawezi kuyasahau alipokuwa akiitumikia miamba hiyo ya Jangwani akikumbuka bao alilowahi kufunga kwenye mchezo dhidi ya Simba.
“Kiukweli lile ni tukio ambalo lilinipa furaha sana na katika maisha yangu ya mpira sijawahi kupata furaha kama ile, kwani kumfunga mtani kulinifanya nijisikie vizuri na iliniongezea kujiamini uwanjani.
"Tukio la pili ambalo sitalisahau ni ile siku ambayo nilipata majeraha yaliyonifanya kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu, ni tukio ambalo lilinifanya niumie sana.”
Kuhusu mpango wa kuchezea timu kubwa siku zijazo Balama alisema :“Ni ndoto ya kila mchezaji kuwa na hamu ya kuchezea timu kubwa hata mimi bado nina matumaini siku moja nitacheza tena kwenye timu kubwa iwe hapa Tanzania au kimataifa.”