Xavi atabiri mwisho Ronaldo na Messi
Muktasari:
Neymar, Mbappe wametegeneza safu bora zaidi ya ushambuliaji katika kikosi cha PSG msimu huu
Kiungo fundi wa mpira, Mhispania Xavi, anaamini Neymar na Kylian Mbappe ndiyo wachezaji watakaokuja kutamba wakati zama za Lionel Messi na Cristiano Ronaldo zitakapokwisha kwenye kupokezana tuzo ya ubora wa mchezo wa soka duniani.
Ronaldo na Messi wametawala dunia ya mchezo huo kwa miaka 10 sasa huku kila mmoja akishinda tuzo ya Ballon d’Or mara tano.
Neymar, kwa upande wake aliikaribia tuzo hiyo msimu uliopita alipokuwa Barcelona na kwamba msimu huu akiwa PSG amepandisha zaidi kiwango chake cha soka na kuwa staa mkubwa kwenye timu hiyo. Mbappe pia ameibukia vizuri kabisa kutoka Monaco na sasa yupo na Neymar huko PSG.
"Namheshimu sana," alisema Xavi akimzungumzia Neymar.
"Ni mchezaji mahiri, wakati Messi na Cristiano watakaporomoka viwango vyao, atashinda yeye tuzo inayofuata.
"Kipindi ambacho Messi na Cristiano Ronaldo watastaafu, mjadala wa mchezaji gani bora duniani utakuwa kati ya Neymar na Mbappe."