Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri ajitosa sakata la uongozi Yanga

Dar es Salaam. Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amesema njia sahihi kwa Yanga kutatua migogoro na wanachama wake ni kukaa meza moja na kufikia muafaka.

Ndumbaro amesema hayo baada ya kuibuka mvutano uliotokana na wanachama wawili wa Yanga waliotajwa kwa majina ya Juma Ally na Geofrey Mwaipopo kushinda kesi ya kutolitambua Baraza la Wadhamini la Yanga linaloongozwa na Mwenyekiti Kapteni Mstaafu George Mkuchika na wajumbe ambao ni Mama Fatma Karume, Dk Mwigulu Nchemba, Tarimba Abbas na Antony Mavunde ambalo liliingia katika nafasi hiyo kupitia katiba ya 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2011.

Hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Agosti 2, 2023, inalitambua Baraza la Wadhamini la Klabu ya Yanga kwa mujibu wa katiba ya mwaka 1968 ambayo ilifanyiwa marekebisho 2011 na siyo la sasa.

“Mimi niwashauri viongozi na wanachama wa Yanga kuwa migogoro haina tija na inarudisha nyuma maendeleo. Pia migogoro inawaondoa viongozi na wanachama katika ‘reli’ ya kufanya maandalizi ya timu ambayo ina jukumu kubwa la kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.

“Nawashauri Yanga kukaa meza moja na kutatua hiki kinachoendelea, endapo kila mmoja atakuwa anazungumzia kona yake, itachukua muda kumaliza. Wanachotakiwa sasa ni kufanya mjadala wa pamoja na wajue namna ya kumaliza changamoto hiyo. Hii ndiyo njia bora na sahihi zaidi,” alisema Ndumbaro ambaye kitaaluma ni mwanasheria.

Pia Waziri Ndumbaro aliwakumbusha viongozi wa Yanga na klabu zingine kufuata taratibu za kisheria wanapofanya mabadiliko ya uongozi kwa mujibu wa katiba.

“Pia viongozi wanatakiwa kufuata sheria, kanuni, taratibu, au maagizo yaliyowekwa (Compliance). Ni wakati wa klabu kufanya kazi zake kwa kufuata masharti na miongozo iliyowekwa na mamlaka husika. ni muhimu kwa viongozi wa klabu zote. Hii itasaidia kuondoa matatizo kama haya,” alisisitiza Ndumbaro.

Alisema kuwa taratibu zipo wazi, lakini inaonekana kufuatwa inakuwa shida, jambo ambalo linatoa mwanya kwa watu wengine kufanya wanayoona yanafaa.

Kwa sasa, uongozi wa Klabu ya Yanga chini ya Rais, Injinia Hersi Said unasubiri uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuwasilisha maombi ya kuongezewa muda wa kufanya mapitio ya kesi  ambayo uamuzi wake unauondoa uongozi wa sasa madarakani.

Mkurugenzi wa Sheria wa Yanga, Simon Patrick alisema wamechukua  hatua hiyo kutokana na ukweli kuwa hawakujua kufunguliwa kwa kesi hiyo mpaka kuamuliwa kwake na baada ya kukubaliwa ombi lao, pia watawasilisha maombi ya kufanya marejeo ya kesi hiyo iliyofunguliwa na Juma Ally na Geofrey Mwaipopo dhidi ya Wajumbe wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo.

Alisema wameamua kufanya hivyo kwa sababu suala hilo ni la kisheria ukizingatia kuwa muda wa kufanya marejeo na kukata rufaa umekwisha bila ya wao kuwa na taarifa kutokana na ukweli kwamba uongozi haukuwa na wito wa mahakama.