Prime
Wametibua vikosi Simba, Yanga
Muktasari:
- Katika usajili huo, kuna picha tofauti inakwenda kutokea katika vikosi hivyo ambapo hapa tunakuchambulia itakavyokuwa kwa timu hizo za Yanga, Simba na Azam huku ikionekana ni usajili wa kimkakati zaidi.
Kuna siku 34 zimebaki kutoka leo Agosti 4 hadi kufikia Septemba 7, 2025 kwa timu za Ligi Kuu Bara kukamilisha zoezi la usajili kabla ya kuanza kwa mchakamchaka wa ligi hiyo.
Ikumbukwe kuwa, Julai Mosi mwaka huu, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilitangaza kufungua dirisha kubwa la usajili ambalo litafungwa Septemba 7, 2025, huku Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ikisema Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026 itaanza Septemba 16, 2025.
Ukiangalia kinachoendelea kwenye usajili, kila timu inaimarisha kikosi chake ili kufanya vizuri msimu ujao huku zile timu tatu za juu zilizomaliza 2024-2025, zinashindana sokoni.
Katika usajili huo, kuna picha tofauti inakwenda kutokea katika vikosi hivyo ambapo hapa tunakuchambulia itakavyokuwa kwa timu hizo za Yanga, Simba na Azam huku ikionekana ni usajili wa kimkakati zaidi.
AZAM
Kabla ya jana, Azam ilikuwa imetambulisha wachezaji wapya watano wakiwemo wanne wazawa na mmoja wa kimataifa.
Katika usajili wa kikosi hicho ambacho kitaongozwa na kocha mpya, Florent Ibenge raia wa DR Congo, hadi sasa kimegusa maeneo makuu ya uwanjani ambayo ni kipa, beki, kiungo na mshambuliaji.
Katika kipa, ameongezwa Aishi Manula, nyota ambaye aliwahi kuitumikia timu hiyo kuanzia 2012 hadi 2017 alipohamia Simba. Amerejea hapo akitokea Simba kufuatia mkataba wake kumalizika.
Uzoefu alionao Manula, unakwenda kuimarisha eneo la golini ndani ya Azam ambapo msimu uliopita Mustafa Mohamed ambaye alikuwa kipa namba moja aliposhuka kiwango, kulikuwa na shida.
Licha ya chipukizi Zuber Foba kuonekana kufanya vizuri, lakini uzoefu ulimuangusha na kuna wakati aliruhusu mabao rahisi.
Hata hivyo, Manula ana kazi kubwa ya kufanya kwani msimu uliopita 2024-2025 hakucheza mechi yoyote ya kimashindano ndani ya Simba jambo ambalo linabaki kuwa mtihani kwake kudhihirisha bado ana uwezo wa kuipambania timu hiyo kufikia malengo.
Ukija eneo la ulinzi, kuna beki wa kati Lameck Lawi ametua akitokea Coastal Union.
Beki huyo anayecheza timu ya taifa ya Tanzania chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, amekuwa akizivutia klabu kadhaa ambapo msimu uliopita ilibaki kidogo aitumikie Simba, lakini usajili wake uliibua mvutano, akabaki Coastal.
Safari hii ametua Azam kwenda kuimarisha eneo hilo ambalo msimu uliopita kwenye ligi liliruhusu mabao 19, ikiwa ni timu ya tatu kuruhusu mabao mengi nyuma ya Simba na Yanga.
Tulishuhudia mabeki wa kati msimu uliopita ndani ya Azam walicheza Yoro Diaby na Yeison Fuentes ambao walianza mwanzo. Baadaye dirisha dogo akasajiliwa Landry Zouzou.
Uamuzi wa kusajiliwa Lawi, umetokana na kuonekana gepu eneo hilo kwani msimu uliopita ilililazimu benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Rachid Taoussi aliyeondoka wakati mwingine kumtumia kiungo mkabaji Ever Meza kucheza beki wa kati.
Himid Mao, nyota aliyeitumikia Azam kuanzia 2009 hadi 2018 alipotimkia Misri, amerejea kikosini hapo kuimarisha eneo la kiungo mkabaji.
Ever Meza, Sospeter Bajana, James Akaminko, Mamadou Samake na Adolf Bitegeko, ndiyo waliokuwa wakicheza eneo hilo msimu uliopita huku taarifa zikibainisha Bajana hatakuwa na kikosi hicho kufuatia mkataba wake kumalizika, ndiyo maana ameongeza Mao.
Kucheza soka nchini Misri kwa kipindi cha takribani miaka sita katika timu za Petrojet, Enppi SC, Entag El Harby, El Mahalla na Talaea El Gaish, inatosha kumfanya kuwa mchezaji mzoefu, hivyo kuna kitu anakuja kuongeza Azam.
Muhsini Malima ambaye ni nyota wa Kitanzania, ni usajili mpya katika kikosi cha Azam akiwa anacheza eneo la ushambuliaji.
Nyota huyo aliyewahi kucheza Dodoma Jiji na Coastal Union, ametua Azam akitokea Zed FC ya Misri. Amerejea nchi hivyo sio mgeni kwenye Ligi Kuu Bara.
Katika nafasi anayokwenda kuongeza nguvu ndani ya Azam, ameondoka Gibril Sillah aliyemaliza mkataba wake na kutimkia ES Sétif ya Algeria, huku mchezaji huyo akiwa ndiye aliyefunga mabao mengi kwenye ligi msimu uliopita ambayo ni 11.
Hata hivyo, Malima ana kazi kubwa ya kufanya kwani katika kikosi cha Azam eneo la mbele lina wachezaji waliionesha kiwango bora akiwemo Feisal Salum aliyeibuka kinara wa asisti kwenye ligi akipiga 13.
Pape Doudou Diallo unaweza kusema ni kama Azam imekuwa siriazi sana katika usajili wake kwani imemshusha mshambuliaji aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Senegal msimu uliopita akiitumikia Linguère de Saint-Louis kwa mkopo akiwa anamilikiwa na Generation Foot.
Nyota huyo alifunga mabao 11 katika Ligi Kuu ya Senegal, ametua Azam kuimarisha eneo la ushambuliaji ambalo ukimuondoa Sillah aliyefikisha idadi kama hiyo kwenye Ligi Kuu Bara, hakuna mshambuliaji mwingine aliyefanya vizuri zaidi.
Alikuwepo Nassor Saadun aliyefunga mabao manane, Zidane Sereri (5), Jhonier Blanco (2), na Alassane Diao (1). Wengine ni Adam Omar Adam ambye alitolewa kwa mkopo kwenda Tanzania Prisons na Franklin Navarro ambaye dirisha dogo alitimkia Union Magdalena.
YANGA
Katika maboresho ya kikosi chake kuelekea msimu ujao, hadi jana ilikuwa imetambulisha wachezaji wapya saba ambapo mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara nguvu kubwa imeweka katika kiungo na ushambuliaji.
Katika wachezaji saba iliosajili, viungo ni watatu, washambuliaji watatu na beki mmoja ambaye pia ana uwezo wa kucheza eneo la kiungo.
Balla Moussa Conté alikuwa mchezaji wa kwanza kusajili na Yanga akiwa anacheza eneo la kiungo mkabaji.
Katika eneo hilo la kiungo cha ukabaji pia ameongezwa Abdulnassir Mohamed Abdullah 'Casemiro', huku Lassine Kouma akiwa ni kiungo mshambuliaji.
Kuondoka kwa Khalid Aucho na Jonas Mkude katika kiungo mkabaji, ndio wamesajiliwa Conte kuziba pengo la mchezaji wa kimataifa na Casemiro akichukua nafasi ya mzawa.
Nafasi ya Stephane Aziz Ki, amekuja Kouma, huku Offen Chikola anayecheza winga, unaweza kusema ni mipango ya kuimarisha eneo la kushambulia.
Abubakar Nizar Othman ‘Ninju’ ni beki anayecheza kati na kulia, pia ana uwezo wa kucheza kiungo mkabaji.
Kule mbele kwenye eneo la ushambuliaji kuna Andy Bobwa Boyeli na Celestin Ecua.
Rekodi za Ecua aliyekuwa Mchezaji Bora (MVP) wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu uliopita kwa kiasi fulani unaweza kuipa jeuri Yanga kufuatia kuondoka kwa Kennedy Musonda ambaye hakuwa na nafasi kubwa ya kucheza kikosini hapo.
Yanga imeimarisha eneo hilo la ushambuliaji ambapo walioingia wana kazi kubwa ya kufanya kwani Clement Mzize na Prince Dube, walifanya kazi kubwa msimu uliopita.
Mzize aliibuka kinara wa mabao kwa wazawa akifunga 14, huku Dube akifunga 13 yakiwa ni matatu nyuma ya kinara Jean Charles Ahoua wa Simba.
Yanga katika mashindano yote msimu uliopita ilifunga jumla ya mabao 136 ikiwa ndiyo timu iliyokuwa na mabao mengi zaidi ambapo Ngao ya Jamii (5), Ligi Kuu Bara (83), Ligi ya Mabingwa Afrika (22), Kombe la FA (22) na Kombe la Muungano (4), hivyo msimu ujao kuna kazi kubwa ya kufikia idadi hiyo ya mabao mbali na kubeba mataji.
SIMBA
Baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo, Simba inaendelea kujiimarisha kuona msimu ujao inarudisha utawala wake kwani nayo ilibeba taji hilo mara nne mfululizo kabla ya Yanga kukita mizizi.
Simba hadi kufikia jana, ilikuwa imetambulisha nyota wapya sita wa eneo la beki wa kati, kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji na mshambuliaji wa mwisho.
Unaweza kupongeza zaidi eneo la ushambuliaji lililoongezewa nguvu kufuatia namba nzuri za wachezaji waliopo hapo.
Usajili mpya ni Jonathan Sowah ambaye msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara alicheza mechi 14 na kufunga mabao 13.
Anakwenda kuungana na Steven Mukwala na Leonel Ateba ambao nao kila mmoja alifunga mabao 13. Kama Ateba hataondoka kutokana na kuripotiwa kuna ofa mezani, basi Simba itauanza msimu ikiwa na washambuliaji watatu waliomaliza msimu na jumla ya mabao 39.
Pia katika eneo la ushambuliaji, Simba imemshusha viungo washambuliaji Morice Abraham na Mohamed Bajaber, pia viungo wa ukabaji Alassane Kante na Hussein Daudi Semfuko.
Viungo waliondoka ni Fabrice Ngoma, Augustine Okejepha, Debora Fernandes Mavambo na Omary Omary.
Kule kwenye ulinzi yupo Rushine De Reuck ambaye ni beki wa kati kufuatia kuondoka Che Malone Fondoh, lakini pia Hussein Kazi ambaye hakuwa na nafasi, naye ameondoka.
Mabeki wengine walioondoka ni Kelvin Kijili (beki wa kulia), Mohamed Hussein (beki wa kushoto) na Valentin Nouma (beki wa kushoto). Pia kipa Aishi Manula hali inayofanya Simba kuingia sokoni kuziba nafasi hiyo.