Waarabu wamrudia tena Bruno Fernandes
Muktasari:
- Kinachoelezwa ni mikutano ya kimazungumzo baina ya mabosi wa klabu hiyo ya Saudia na kambi ya Fernandes yameshaanza kufanyika.
MANCHESTER, ENGLAND: Naodha wa Manchester United, kiungo fundi wa boli, Bruno Fernandes amewekwa tena kwenye rada za Al-Ittihad ya Saudi Arabia ikihitaji huduma yake kabla ya dirisha hili la majira ya kiangazi kufungwa.
Kinachoelezwa ni mikutano ya kimazungumzo baina ya mabosi wa klabu hiyo ya Saudia na kambi ya Fernandes yameshaanza kufanyika.
Fernandes, 30, aligomea timu nyingine ya Saudi Arabia, Al-Hilal dirisha hili, lakini ishu ya Al-Ittihad kuzungumza na mawakala wa kiungo huyo imedaiwa ni jambo linaloendelea vizuri.
Al-Ittihad inapambania kwa nguvu zote ili kupata huduma ya Mreno huyo kwenye kikosi chao. Na kinachoelezwa ni Fernandes ameitaka miamba hiyo ya Saudi Pro League kumlipa mshahara wa Pauni 33 milioni kwa mwaka.
Hata hivyo, Fernandes alikiri wazi ataondoka Old Trafford kama tu klabu itaamua kumuuza ili kupata pesa.
Fernandes alisema: “Siku zote nimejaribu kuwa mkweli. Mara zote nimekuwa nikisema nitakuwa kwenye klabu hiyo hadi hapo watakaponiambia niondoke.
“Nipo tayari kufanya vizuri, kuirudisha klabu kwenye nyakati zake bora. Siku ambayo klabu itaona inatosha, inataka kuachana na mimi, nitaelewa, maana soka ndivyo lilivyo. Lakini, kwa upande wangu, siku zote nimekuwa nikiheshimu maneno yangu.”
Uhamisho wa kwenda Al-Ittihad utamfanya Fernandes kwenda kuungana na mastaa wengine wakiwamo Karim Benzema, Moussa Diaby na N’Golo Kante.
Man United ipo bize kwenye dirisha hili la usajili ikiwa ni kuboresha kikosi chao ili kumfanya kocha Ruben Amorim kuwa na kikosi bora. Klabu hiyo imetumia zaidi ya Pauni 200 milioni kunasa huduma za mastaa Bryan Mbeumo, Matheus Cunha na Benjamin Sesko.