Gary Neville: Sesko hajafikia kiwango cha kushindana EPL
Muktasari:
- United bado hawajapata ushindi wowote katika msimu mpya wa Ligi Kuu baada ya kupoteza dhidi ya Arsenal na kutoka sare dhidi ya Fulham.
Manchester, England. Beki wa zamani wa Man United, Gary Neville amesema mshambuliaji mpya Benjamin Sesko ambaye amesajiliwa kwa pauni milioni 74 (Sh 250 Bilioni) akitokea RB Leipzig ya Ujerumani bado hajafika kiwango cha kushindana vilivyo ndani ya Ligi Kuu England.
Neville amebainisha kuwa mashabiki na wachambuzi wengi walikuwa wanataka Sesko aanze mechi, lakini Amorim bado anamuweka benchi na kumtumia kama mchezaji wa akiba.
Hadi sasa, Mslovenia huyo mwenye miaka 22 amecheza dakika chache tu, ikiwemo pia kwenye kipigo cha wiki iliyopita cha 1-0 dhidi ya Arsenal.
“Sesko kwa sasa hayuko sawa kimwili, hana kasi ya kutosha. Ni lazima apewe dakika nyingi zaidi. Amorim atabidi ampe mechi ya Kombe la Carabao dhidi ya Grimsby ili apate dakika 90, kisha awe tayari kuanza dhidi ya Burnley Jumamosi. Haifai mchezaji wa thamani na kipaji kama hicho akibaki tu benchi,” amesema Neville.
Hata hivyo, mchambuzi huyo pia hakuridhishwa na mabadiliko ya Amorim kipindi cha pili, hasa kuwatoa mabeki Leny Yoro na Luke Shaw dakika tano kabla ya mchezo kuisha.
“Huo ulikuwa uamuzi wa ajabu. Kwa kawaida huwezi kubadilisha safu ya ulinzi mwishoni mwa mchezo,” amesema nyota huyo wa zamani wa United.
United bado hawajapata ushindi wowote katika msimu mpya wa Ligi Kuu baada ya kupoteza dhidi ya Arsenal na kutoka sare dhidi ya Fulham. Wana nafasi ya kurekebisha hali ya kikosi chao Jumatano kwenye Kombe la Carabao Cup dhidi ya Grimsby, kabla ya kurejea Old Trafford kuivaa Burnley Jumamosi.
Mbali na United michezo mingine iliyopigwa jana kwenye Ligi Kuu ya England ilizikutanisha Crystal Palace ambayo ilibanwa kwenye Uwanja wake wa nyumbani na kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Brentford.
Everton iliyokuwa ikicheza mechi ya kwanza ya EPL kwenye Uwanja wake mpya wa Hill Dickinson ilifungua dimba hilo kwa kupata ushindi wa mabao 2-0 ikiichapa Brighton.
Mabao ya Everton jana yalifungwa na Iliman Ndiaye katika dakika ya 23 wakati James Garner akiitimisha ushindi huo kwa kuandika bao la pili dakika ya 52 huku mchezaji mpya Jack Grealish aking’aa kwa kutoa pasi zote mbili za mabao.
Arsenal ndiyo vinara kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi sita baada ya kushinda mechi zote mbili sawa na Tottenham wakati Chelsea na Nottingham Forest zikifuata katika nafasi ya tatu na nne zikiwa na pointi nne.
Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa mchezo mmoja utakaopigwa saa 4:00 usiku ambapo Newcastle United itakuwa kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa St. James’ Park kukabiliana na mabingwa watetezi Liverpool.