Sesko atambulishwa rasmi Manchester United
Muktasari:
Mshambuliaji huyo amesaini mkataba wa miaka mitano kuitumikia Man United hadi 2030.
Manchester United imethibitisha kumsajili mshambuliaji Benjamin Sesko kutoka RB Leipzig, na kuibuka kidedea dhidi ya Newcastle United ambao nao walikuwa wakimfuatilia mchezaji huyo.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Slovenia anakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa Man United katika safu ya ushambuliaji, akitanguliwa na Matheus Cunha kwa Pauni 62.5 milioni na Bryan Mbeumo kwa Pauni 65 milioni na nyongeza za pauni milioni 6.
Newcastle ilianza kwa kutoa dau la Euro 75 milioni (Sh217 bilioni) pamoja na nyongeza ya Euro 5 milioni ambalo lilikataliwa na Leipzig, kabla ya kurudi na ofa mpya ya Euro 80 milioni bila nyongeza.
United ilijibu kwa kutoa ofa ya Euro 75 milioni na nyongeza ya Euro 10 milioni.
Newcastle ilipandisha dau hadi Euro 82.5 milioni (Sh240 bilioni) pamoja na nyongeza ya Euro 2.5 milioni dau ambalo Leipzig ililikubali. Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa Slovenia aliweka wazi kuwa anatamani kujiunga na Manchester United, jambo lililorahisisha mazungumzo ya mwisho na kufanikisha makubaliano.
Katika taarifa ya klabu, Man United imesema, “Manchester United ina furaha kuthibitisha kwamba Benjamin Sesko amejiunga na klabu, akisaini mkataba hadi Juni 2030.”
Sesko amesema anavutiwa na historia ya United na mradi wa klabu hiyo kuelekea siku za usoni.
“Nimehisi mazingira ya kifamilia na ari ya mafanikio tangu nilipowasili. Ni sehemu sahihi kufikia kiwango changu cha juu,” amesema Sesko.
Sesko mwenye umri wa miaka 22 ameagana na Leipzig kupitia ujumbe wa shukrani kwenye mitandao ya kijamii, akisema atakumbuka mapenzi na msaada wa mashabiki wa klabu hiyo.
Kwa upande wa Newcastle, kukosa saini ya Sesko ni pigo kubwa hasa ikizingatiwa kuwa Isak bado anatakiwa na Liverpool. Majogoo wa Anfield tayari wamekataliwa ofa ya Pauni100 milioni na huenda ikarudi tena mezani lakini dili linaweza kuwa gumu baada ya United kumalizana na Sesko hatua inayoweza kupunguza uwezekano wa Isak kutua Anfield.
United ilitoka sare ya mabao 2-2 na Everton katika mechi ya kirafiki Jumapili, mabao yakifungwa na Bruno Fernandes kwa penalti na Mason Mount. Amorim alitumia mfumo wa 3-5-2, akiwapanga Cunha na Mbeumo mbele, wakisaidiwa na Fernandes. Kuja kwa Sesko kunatarajiwa kuwasogeza Cunha na Mbeumo nyuma kidogo, huku Fernandes akishuka zaidi katikati.
Aidha, taarifa zinaeleza kuwa United imewasiliana na Brighton kuulizia uwezekano wa kumsajili kiungo mkabaji Carlos Baleba, 21, ambaye alicheza mechi 34 msimu uliopita wa EPL na kufunga mabao matatu. Hata hivyo, dili hilo linaonekana gumu kutokana na msimamo wa Brighton kutotaka kuuza na bajeti ya United kuwa kubwa tayari msimu huu wa usajili.