Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gyokeres afungua ukurasa wa mabao Arsenal

London, England. Viktor Gyokeres amefungua ukurasa wake wa mabao ndani ya Arsenal baada ya kufunga bao lake la kwanza katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Athletic Bilbao katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Emirates.

Straika huyo aliyenunuliwa kwa pauni milioni 64 kutoka Sporting Lisbon alitikisa nyavu kwa kichwa akimalizia krosi ya Martin Zubimendi, kabla ya kusherehekea kwa mtindo wake maarufu wa kuweka mikono usoni.

Gyokeres pia alihusika kwenye bao la pili, akimpasia mpira Declan Rice aliyemnyookea Gabriel Martinelli ambaye alimsetia pasi ya mwisho Bukayo Saka kufunga.

Dalili kwa Gyokeres

Mashabiki walipiga kelele muda mrefu wakihitaji straika halisi. Tofauti na mchezo wa waliopoteza 3-2 dhidi ya Villarreal, safari hii Gyokeres alikuwa sehemu ya mchezo kwa asilimia kubwa huku akishambulia kwa kasi.

Ni aina ya mshambuliaji ambaye Mikel Arteta amekuwa akikosa kwa muda mrefu.

Zubimendi naye yumo

Usajili wa Martin Zubimendi tayari ulikuwa umewasha moto Emirates, Arsenal ikiwapiku Liverpool, Man City na Real Madrid.

Alionyesha kiwango cha juu akinyakua mipira kwa kasi, kuanzisha mashambulizi, na kupiga pasi zenye macho. Krosi yake kwa Gyokeres ilikuwa mfano halisi wa uwezo wake wa kuona nafasi na kuipenyeza pasi kwa usahihi.

Nico Williams, ambaye Arsenal walimuwinda majira haya ya joto, aliwasili Emirates lakini kwa jezi ya Bilbao. Winga huyo wa kushoto alisaini mkataba mpya wa miaka minane kuendelea kucheza Bilbao hadi 2035, akizima matumaini ya Arsenal.

Saliba, Gabriel warudi kivingine

Kabla ya pambano na Manchester United Jumapili, mashabiki wa Arsenal walipata habari njema baada ya Gabriel kuanza bega kwa bega na William Saliba.

Gabriel, aliyefanyiwa upasuaji wa nyama za paja Aprili, alionekana imara bila kuogopa changamoto. Ushirikiano wake na Saliba ulihakikisha Bilbao hawapati nafasi nyingi za kufika langoni.

Havertz afunga

Kai Havertz, aliyekosa sehemu kubwa ya msimu uliopita kwa jeraha, alirejea uwanjani akiwa amejengeka zaidi kimwili. Dakika 11 tu baada ya kuingia, alitumia nguvu na ujanja kuwapenya mabeki wawili na kufunga bao safi.

Kurejea kwake kunampa Arteta chaguo jingine kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati, na ushindani wa nafasi hiyo sasa utakuwa mkali kati yake na Gyokeres.