Arteta azumgumzia kiwango cha Gyokeres
Muktasari:
- Staa huyu wa kimataifa wa Sweden alitua Arsenal baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya washika mitutu hao na Sporting Lisbon iliyokuwa haitaki kumwachia kwa kiasi kidogo cha pesa.
London, England. Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesisitiza mshambuliaji wao mpya, Viktor Gyokeres aliyesajiliwa kwa Pauni 64 milioni atakuwa kwenye 'hali nzuri sana' kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa Ligi Kuu England.
Gyokeres aliyeanza katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Villarreal uliomalizika kwa Arsenal kufungwa mabao 3-2, kwenye uwanja wa Emirates, hakupata nafasi nyingi za kufunga licha ya kuonyesha kujituma.
Staa huyu wa kimataifa wa Sweden alitua Arsenal baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya washika mitutu hao na Sporting Lisbon iliyokuwa haitaki kumwachia kwa kiasi kidogo cha pesa.
Alionyesha kiwango bora akiwa na wababe hao wa Ureno na hadi anaondoka alikuwa ameshafunga mabao 97 katika mechi 103.
Mchezo huo dhidi ya Villarreal ulikuwa wa pili kwa Gyokeres tangu ajiunge Arsenal, mechi ya kwanza ikiwa ni dhidi ya Tottenham na alicheza kwa dakika chache.
Akizungumzia kiwango chake, Arteta alisema mchezaji huyo kwa sasa hana utimamu wa kimwili, lakini anaamini kabla ya msimu kuanza atakuwa fiti na ataonyesha tu makali yake.
"Ilikuwa muhimu sana kwake kuanza mechi na kutengeneza uhusiano na wachezaji wenzake uwanjani. Amekuwa nasi kwa takriban wiki moja tu, lakini niliona mambo mengi mazuri, hasa jinsi alivyojipanga wakati wa kushambulia."
Arteta aliongeza, Gyokeres hakuwa na mazoezi kamili kwa karibu miezi miwili kabla ya kujiunga na timu na hadi kufikia mechi hiyo alikuwa amefanya mazoezi siku tano au sita pekee.
"Kila siku ninavyomwona mazoezini, anazidi kuimarika. Anajenga uhusiano na wachezaji wengine, jambo ambalo ni muhimu kwa mchezaji wa nafasi yake kwani inamsaidia kupata nafasi za kufunga. Tunaamini kufikia Jumamosi atakuwa kwenye hali nzuri zaidi na ataendelea kuwa bora."
Arsenal inatarajiwa kucheza tena dhidi ya Athletic Bilbao kwenye mechi ya Emirates Cup Jumamosi hii, kabla ya mechi yao ya ufunguzi wa EPL dhidi ya Manchester United ugenini Agosti 17.
Arteta pia alisema wanatarajia kurejea kwa Kai Havertz, ambaye alikosa mechi dhidi ya Villarreal kutokana na majeraha madogo.